Sunday, January 22, 2017

MKOA WA PWANI UNA ZIADA YA CHAKULA NA HAKUNA NJAA-NDIKILO


Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
MKOA wa Pwani, una ziada ya chakula zaidi ya tani 503,711.5 huku vyakula vikiwa vimejaa kwenye masoko hivyo hakuna njaa.
Aidha mkoa huo una mfumko wa bei za vyakula katika masoko mbalimbali kutokana na kupanda kwa gharama za nafaka katika mikoa ya Mbeya,Kagera,Iringa na Morogoro.
Hayo yalibainika ,katika ziara ya siku moja ya mkuu wa mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo,alipotembelea soko la Mailmoja,Mlandizi na Chalinze kujionea hali ya chakula.
 Katika masoko hayo mchele wa kawaida kwa sasa unauzwa kg kwa sh.1,500 hadi 2,000 ,mchele super 2,200,unga sh,1600 ,mahindi 1,100 ,maharagwe kg sh.2,000 hadi 2,400 ,na viazi mbatata gunia sh.130,000 badala ya 60,000.
Mhandisi Ndikilo alisema,msimu wa kilimo 2015/2016 mkoa ulilenga kulima hekta   205,467 za mazao ya chakula zilizotarajiwa kuzalisha tani1,039,565.
 “Mkoa pia ulilenga kulima hekta 158,242 za mazao mbalimbali ya biashara na kutarajiwa kuzalisha tani 837,108 “alisema.
Mhandisi Ndikilo,alisema hekta 144,241 za mazao ya chakula zililimwa na kuzalisha tani 773,279 huku hekta 85,850 za mazao ya biashara zililimwa na kuzalisha tani 566,283.
Alitoa angalizo kuhusiana na upungufu wa utomwili (Protini) ambao hutokana na uzalishaji mdogo wa mazao ya jamii ya mikunde.
Mkuu huyo wa mkoa ,alisema upungufu wa mazao jamii ya mikunde, hauna athari kwani hufidiwa na mazao yatokanayo na mifugo, uvuvi na mazao ya jamii hiyo kutoka mikoa mingine.
Mhandisi Ndikilo,alizielekeza halmashauri za wilaya 
kuwajengea uwezo wakulima kutambua umuhimu wa uvunaji bora, utunzaji wa chakula na kiasi cha chakula kinachohitajika kaya kwa mwaka mzima.
 Alisisitiza endapo kutatokea janga la njaa kwa mkoa ,basi wakulima watumie fedha walizopata kwenye mazao ya biashara kama korosho.
Alisema wakulima wa zao la biashara la korosho katika msimu unaoisha walipata sh.bil.33 kwa tani 12,000 walizouza, hivyo watumie fedha hiyo kununua chakula ili kununua chakula na kukabiliana hali hiyo.
Mhandisi Ndikilo,alikemea kutumia nafaka kwenye shughuli zisizo za lazima,ngoma na kutengeneza pombe .
Nae afisa kilimo kutoka sekretarieti mkoani hapo,Judith Mushi,alisema hali ya chakula kimkoa ni ya wastani lakini tatizo ni wananchi kulalamikia hali ngumu ya maisha.
Alihimiza kupanda mazao yanayostahimili ukame na kukomaa haraka ikiwa ni sanjali na muhogo, mtama, viazi vitamu na kunde.
Judith aliwashauri wafugaji wauze sehemu ya mifugo yao ili kujinunulia chakula badala ya kukaa na mifugo mingi bila tija.
Mfanyabiashara wa nafaka katika soko la Chalinze, Saidi Ally, alisema wafanyabiashara wanapandisha bei za vyakula kutokana na kununua bidhaa mbalimbali kutoka mikoani kwa gharama kubwa.
Alisema kwasasa pia wanagombania bidhaa hizo kwani zinashushwa magunia machache kwasababu kilimo cha vuli na masika (hasa mazao ya chakula) haukuwa mzuri .
Mkuu wa mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo,akiangalia hali ya chakula katika masoko mbalimbali Mailmoja,Chalinze na Mlandizi ili kujiridhisha kuwa hakuna njaa mkoani hapo.
(Picha na Mwamvua Mwinyi)

No comments :

Post a Comment