Watafiti wakiwa lango kuu la kuingia katika shamba
la jaribio la mahindi yaliyoboreshwa kwa kutumia Teknolojia ya uhandisi
jeni (GMO), chini ya mradi wa Wema katika Kituo cha Utafiti wa Kilimo
cha Makutupora mjini Dodoma. Watafiti hao walikuwa wameongoza na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Charles Tizeba kutembelea shamba hilo.
Mshauri
wa Jukwaa la Bioteknolojia Tanzania (OFAM), Dk. Nicholaus Nyange
(kulia), akitoa mada ya matumizi ya Bioteknolojia ya kisasa katika sekta
ya kilimo mbele ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Charles Tizeba
mjini Dodoma.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech), Dk.Hassan Mshinda (kulia), akitoa maelezo mbele ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Charles Tizeba (wa pili kushoto), alipotembelea
shamba la jaribio la mahindi yaliyoboreshwa kwa kutumia Teknolojia ya
uhandisi jeni (GMO) lililo chini ya mradi wa Wema katika Kituo cha
Utafiti wa Kilimo cha Makutupora mjini Dodoma juzi.
Msafara ukielekea kwenye shamba hilo la majaribio.
Waziri
Tizeba (wa sita kutoka kushoto), akiwa katika picha ya pamoja na
watafiti wa kilimo mbele ya shamba hilo la majaribio ya mbegu za mahindi
katika kituo cha kilimo cha Makutupora mkoani Dodoma.
Watafiti na Waziri Tizeba wakijadiliana mbele ya shamba hilo.
Na Dotto Mwaibale, Dodoma
MATUMIZI ya Bioteknolojia ya Kisasa katika Sekta ya Kilimo nchini yataleta mafanikio makubwa kwa wakulima na taifa kwa ujumla.
Hayo
yalielezwa na Mshauri wa Jukwaa la Bioteknolojia Tanzania (OFAM), Dk.
Nicholaus Nyange wakati akitoa taarifa kwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na
Uvuvi, Charles Tizeba alipotembelea shamba la jaribio la mahindi
yaliyoboreshwa kwa kutumia Teknolojia ya uhandisi jeni chini ya mradi wa
Wema katika Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Makutupora mjini Dodoma.
“Matumizi
ya Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo Tanzania ni muhimu hasa katika
kipindi hiki ambacho maeneo mengi ya nchi yanakabiliwa na ukame
kutokana na tabia nchi” alisema Dk.Nyange.
Alisema
taaluma ya uhandisi jeni inawezesha kuhamisha jeni kutoka kwa kiumbe hai
kimoja na kuingiza katika kiumbe hai kingine ili kupata sifa lengwa na
kutengeneza bidhaa kwa matumizi mbalimbali.
Akizungumzia
kuhusu usalama wa matumizi ya Bioteknolojia hapa nchini alisema ni vema
kuanza mchakato wa kuendeleza mazao yaliyofanyiwa mabadiliko ya
kijenetiki (GMO) ambayo yameleta mafanikio makubwa katika nchi nyingine
kwa mfano mahindi yanayostahimili ukame na bungua muhogo unaostahimili
ugonjwa wa batobato na michirizi kahawia, migomba yenye ukinzani dhidi
ya ugonjwa wa mnyauko na pamba yenye ukinzani kwa wadudu waharibifu.
Dk.
Nyange alisema Changamoto kubwa iliyopo katika matumizi ya teknolojia
hiyo ni kuongezeka kwa upotoshaji kutoka kwa wanaharakati na wapinzani
kutokana na
ufahamu
na uelewa wa watafiti, viongozi, wanasiasa na umma kwa jumla kuhusu
masuala ya taaluma hiyo kuwa bado ni mdogo ukiwemo uwekezaji mdogo
katika utafiti na maendeleo.
No comments :
Post a Comment