*Jumla ya sh. bilioni 29 zililipwa mwaka jana
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema Serikali imelipa jumla ya sh. bilioni 29 kwa watumishi
mbalimbali wa umma wakiwemo walimu ikiwa ni sehemu ya madeni yao.
Alitoa kauli hiyo jana (Jumamosi,
Januari 21, 2017) wakati akizindua vyumba vitatu vya kisasa vya madarasa
katika shule ya sekondari Iwawa iliyoko wilayani Makete.
Waziri Mkuu alisema Serikali
imedhamiria kumaliza madeni ya watumishi hao, ambapo hadi kufikia
Novemba mwaka jana jumla sh. bilioni 29 zililipwa kwa watumishi 31,000.
Alisema kwa sasa Serikali
imejipanga kuhakikisha hakuna madeni mapya yanayozalishwa hivyo
amewataka watumishi wa umma na wananchi kuendelea kuiunga mkono
Serikali.
Hata hivyo alisema Serikali
inaendelea na mikakati ya kuboresha sekta ya elimu kwa kujenga mazingira
bora ya kufundishia na kujifunzia.
“Tumeanza mradi wa ujenzi wa
nyumba za walimu katika halmashauri nchini. Hapa Makete tumeleta sh.
milioni 557 kwa ajili ya ujenzi huo,” alisema.
Alisema nyumba hizo za walimu
zinazojengwa katika maeneo mbalimbali hususan ya vijijini ni za kisasa
ambazo zinalenga kuwaondolea changamoto ya makazi.
Waziri Mkuu alisema Serikali
inafanya jitihada za dhati za kuhakikisha kila Mtanzania anapata elimu
kwa kuwa elimu ni kichocheo cha maendeleo ya jamii.
“Tumedhamiria kumpatia elimu kila
Mtanzania, hivyo halmashauri zihakikishe kila kijiji kinakuwa na shule
ya msingi na lazima ziwe na darasa la awali,” alisema.
Naye Mkuu wa Shule hiyo, Mwalimu
Novatus Msivala aliishukuru Serikali kwa kugharamia ujenzi wa vyumba
hivyo vitatu vya madarasa na matundu 10 ya vyoo pamoja na uingizaji wa
maji kwenye vyoo na utengenezaji wa madawati 46.
Alisema ujenzi huo umegharimu sh.
milioni 95 ambao utasaidia kupunguza msongamano kwa wanafunzi. Kwa sasa
Serikali na wananchi wanaendelea kukamilisha ujenzi wa vyumba viwili vya
madarasa na ofisi ya walimu.
Katika hatua nyingine jana Waziri
Mkuu alitimiza ahadi yake ya kumpatia laptop mwanafunzi Ally Alijai wa
Chuo kikuu cha SAUT tawi la Songea mkoani Ruvuma.
Ahadi hiyo aliitoa mwanzoni mwa
mwezi huu alipokuwa katika ziara yake kikazi mkoani Ruvuma, lengo likiwa
ni kuendeleza kipaji cha utunzi wa vitabu kwa mwanafunzi huyo.
Alisema mwanafunzi huyo alionyesha
umahiri mkubwa katika utungaji wa kitabu ambacho kinaweza kutumika
kufundishia katika shule za sekondari.
Hata hivyo Waziri Mkuu alisema
tayari kitabu hicho kimeshawasilishwa Taasisi ya Elimu Tanzania (TEA)
kuona kama kinaweza kuanza kutumika kwa kufundishia. Mwanafunzi huyo
alishukuru kwa zawadi hiyo na kuahidi kutunga vitabu vizuri zaidi.
No comments :
Post a Comment