Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Bi. Sihaba Nkinga
…………………………………………………………………….
NA HASSAN SILAYO-MAELEZO
Mkoa wa Mara ni Moja ya Mikoa
ambayo kwa kiasi kikubwa imekuwa ikiendelea na utamaduni wa kukeketa
watoto wa kike jambo ambalo ni kinyume na haki za mtoto na sheria
mbalimbali duniani.
Kila mwaka takribani watoto
milioni mbili wako katika hatari ya kukeketwa ambako kwasasa Tanzania
ina asilimia 32 ya hali ya ukeketaji suala ambalo Serikali hairidhiki
nalo.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Bi. Sihaba Nkinga alifanya
ziara ya siku 2 Mkoani Mara katika Wilaya za Tarime na Musoma.
Katika ziara hiyo Bi. Sihaba
ambayo alimuwakilisha Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu katika mahafali ya 9 ya Kituo
cha kulea watoto waliokimbia ukeketaji cha Masanga (ATFGM) katika kata
ya Masanga Tarime Vijijini.
Katika hotuba yake Katibu Mkuu
Bi. Sihaba alionesha kushangazwa na vitendo vya ukeketaji vinavyofanywa
na wenyeji wa Mkoa wa Mara na kuviita ni vitendo vya kikatili dhidi ya
watoto wa kike, kwani inakatisha ndoto na matarajio ya watoto hao.
Akitoa kauli ya Serikali Bi.
Sihaba alisema kuwa Serikali itawachukulia hatua kali za kisheria
watakaogundulika kuendeleza vitendo vya ukeketaji kwani ni kinyume na
Sheria ya Nchi na nikinyume na mikataba mbalimbali ya Kimataifa
iliyojielekeza katika kulinda haki mbalimbali za mtoto.
Akionesha kudhamiria kukabiliana
na tatizo la ukeketaji katika mkoa wa Mara Katibu Mkuu Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Bi. Sihaba Nkinga alikutana
na Wazee wa kimila kutoka Koo tano za Bukenye, Nyabasi, Bukira,
Butimbaru, Buhunyaga.
Katika mazungumzo hayo
yaliyolenga kuweka mikakati ya kukomesha tamaduni ya ukeketaji mkoani
Mara, Mzee wa kimila kutoka Koo ya Bukenye Mzee Elias Maganya alisema
kuwa walishapata elimu kutoka kwenye Jukwaa la Kulinda Utu wa
watoto(CDF) na changamoto ni jinsi ya kuzifikia koo nyingine Mkoani huko
ili kuwezesha kuondoa kabisa mila hiyo.
Mzee Elias alisema kuwa sasa ni
jukumu la Serikali kuona umuhimu wa kuwawezesha kutembea Koo hadi Koo
kwa ajili ya kuelimisha jamii kuhusu madhara ya ukeketaji.
Naye Mzee wa Kimila kutoka Koo ya
Bukira Mzee Sinda Nyangore ameishauri Serikali na mashirika mengine
kutoa elimu katika vipindi vyote vya mwaka na kuacha utaratibu wa kutoa
elimu katika msimu wa ukeketaji kwenye koo mbalimbali.
Aidha,Mzee kutoka koo ya
Butimbaru Mwita Nyasibora alishauri mpango wa kutoa elimu kwa jamii
kuhusu madhara ya ukeketaji yafanyika kwa wakati wote badala ya kusubiri
kipindi cha ukeketaji ndipo serikali na asasi nyingine za kiraia
kujitokeza kutoa elimu.
Akijibu hoja hizo Bi. Sihaba
Nkinga amesema kuwa, kweli upo umuhimu wa kutekeleza suala hilo la
kupeleka elimu juu ya madhara ya ukeketaji ili kuweza kuwasaidia watoto
wakike katika koo hadi koo kwani tofauti na hapo lengo kusudiwa haliwezi
kufikiwa na itakuwa ni tofauti na malengo ya serikali katika kupambana
na tamaduni ya ukeketaji.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya
Tarime Bw. Glorius Luoga katika hotuba yake aliyoitoa katika mahafali
hayo, aliyataja majina ya mangariba maarufu ambao wanatafutwa na vyombo
vya dola kwa vitendo vya ukeketaji katika maeneo mbalimbali wilayani
Tarime.
Mkuu wa Wilaya huyo pia, alisema
ofisi yake imeshawapeleka katika vyombo vya Sheria baadhi ya watu
wanaojihusisha na vitendo vya ukeketaji na kuahidi kuendelea
kuwachukulia hatua kali za Kisheria wale watakaoendelea na vitendo hivyo
vya ukeketaji.
Aidha, Bw. Luoga alioneshwa
kuchukizwa na aina ya wazazi na walezi wanaolazimisha kuwatahiri watoto
wa kiume kwa mara ya pili baada ya tohara salama kwani kitendo hicho ni
sawa na kumjeruhi mtoto.
Akiongea na wahitimu, wazazi,
walezi na mangariba wastaafu, Mkuu wa Wilaya ya Bunda Bi. Lydia
Bupilipili alisema, wazazi na walezi wanapaswa kuona umuhimu wa
kuwapeleka watoto wa kike shuleni ili waweze kutimiza ndoto
walizojiwekea katika maisha yao.
Akiongea mbele ya Mkurugenzi wa
Kituo cha Kulea Watoto waliokimbia Kukeketwa cha (ATFGM-Massanga) Sister
Stella Mgaya aliishukuru Serikali ya Wilaya na Wizara ya Afya kupitia
Maafisa Maendeleo ya Jamii kwa ushirikiano wanaoupata pale wanapohitaji.
Aidha, Sister Stella Mgaya
alisema kuwa kituo hicho kimekuwa kikikumbwa na changamoto nyingi
ikiwemo kuwa na idadi kubwa ya watoto kituoni hapo baada wanaokataliwa
na wazazi/walezi pindi wanapotoka kituoni hapo hivyo kuongeza gharama ya
kuwapeleka shuleni, Sister Mgaya
Wakisoma risala kwa mgeni rasmi
wahitimu wa kituo cha kulea watoto cha masanga walitoa maombi yafuatayo
kwa Katibu Mkuu Bi. Sihaba Nkinga waliomba kuendelezwa kielimu pindi
wanapomaliza kituoni hapo wakati mwingine wanakataliwa na kutengwa na
wazazi/walezi wao.
Aidha, Watoto hao waliiomba pia
serikali kukamata wazazi/walezi wanaowalazimisha kukeketwa pindi
wanapotoka kituoni hapo na kuendelea na kuutilia mkazo utaratibu wa
kuchukuliwa hatua kali za kisheria kwa wazazi,walezi na mangariba
wanaojihusisha na kazi ya ukeketaji ikiwemo kifungo cha miaka 5-10 jela.
Rai yangu kwa watanzania na hasa
makabila yanayoendeleza mila ya ukeketaji wa watoto wa kike ni kuacha
tamaduni hii ambayo ni kinyume na sheria za nchi na hata mikataba
mbalimbali ya kimataifa inayolenga kumlinda mtoto wa kike. Pia ni muda
wa kujikita katika kumuendeleza mtoto wa kike kielimu ili waweze
kutimiza malengo na ndoto walizojiwekea kwani “Tanzania Bila ukeketaji
inawezekana”
No comments :
Post a Comment