Waziri wa Fedha na Mipango Dk.
Philip Mpango akielezea waandishi wa habari kuhusu ukuaji wa uchumi wa
nchi na mambo mbalimbali yanayohusu masuala ya kiuchumi alipozungumza na
wanahabari katika wizara hiyo leo jioni soma taarifa kamili ya waziri
huyo hapa chini.
………………………………………………………………..
Nashukuru kupata fursa ya
kuzungumza nanyi leo kuhusu hali ya uchumi wa Taifa kwa kipindi cha
Julai – Desemba, 2016 na matarajio hadi Juni 2017. Nitajitahidi kutumia
lugha rahisi ili wananchi wa kawaida waweze kuelewa mambo ya msingi
kuhusu mwenendo wa uchumi wa nchi yetu.
Ustawi wa Uchumi Unapimwaje?
Ustawi wa uchumi wa Taifa
unapimwa kwa kuangalia viashiria mbalimbali. Kwa kifupi, ustawi wa
uchumi unapimwa kwa kuangalia kama shughuli mbalimbali za kiuchumi
zinaongezeka au zinapungua au kama zimedumaa.
Shughuli muhimu zinazoangaliwa
ni pamoja na uzalishaji wa chakula na mazao mbalimbali ya kilimo, mifugo
na uvuvi; uzalishaji wa bidhaa za viwandani na migodini; ujenzi wa
miundombinu; uwekezaji; mwenendo wa bei, biashara na masoko; utoaji wa
huduma mbalimbali kwa jamii ikiwa ni pamoja na elimu, afya, maji,
mawasiliano, usafiri na usafirishaji, utalii na huduma za kifedha; na
kiwango cha utekelezaji wa bajeti ya Serikali.
Aidha, uchambuzi na tathmini ya
hali ya uchumi wa Taifa inafanyika kwa kulinganisha viashiria na malengo
yaliyowekwa au kwa kuangalia vigezo vinavyokubalika kimataifa au kwa
kulinganisha na mwenendo wa viashiria vya kiuchumi katika nchi nyingine.
Vilevile, afya ya uchumi inapimwa kwa kutumia vigezo vya jumla, vya
kisekta na kimaeneo.
- VIASHIRIA MBALIMBALI VYA MWENENDO WA UCHUMI WA TAIFA
- Ukuaji wa Pato la Taifa
Ukuaji wa uchumi (kasi ya
kuongezeka au kupungua kwa uzalishaji wa bidhaa na huduma katika nchi)
ni mojawapo ya vitu vinavyotazamwa katika kutathmini afya ya uchumi wa
Taifa. Kiashiria kinachotumika kupima ukuaji wa uchumi ni ukuaji wa Pato
la Taifa yaani thamani ya bidhaa na huduma zilizozalishwa katika nchi
katika kipindi kinachorejewa ikilinganishwa na kipindi kilichopita.
Takwimu za ukuaji uchumi zinaonesha kuwa uchumi wa Taifa umeendelea
kukua na Tanzania imebaki kuwa miongoni mwa nchi za bara la Afrika
Kusini mwa Jangwa la Sahara ambazo uchumi wake unakua kwa kasi kubwa
zaidi. Mwenendo wa ukuaji wa uchumi kwa baadhi ya nchi jirani na kisekta
umeoneshwa katika jedwali la 1 na la 2.
Jedwali1: Ukuaji wa Pato la Taifa Katika Baadhi ya Nchi za Kiafrika
NCHI | 2015 | 2016 |
Burundi | -4.0 | -0.5 |
Kenya | 5.6 | 6.0 |
Rwanda | 6.9 | 6.0 |
Tanzania | 7.0 | 7.2 |
Uganda | 4.8 | 4.9 |
Zambia | 3.0 | 3.0 |
Malawi | 2.9 | 2.7 |
Congo DRC | 6.9 | 3.9 |
Afrika Kusini mwa Sahara | 3.4 | 1.4 |
- Mfumuko wa bei
Kiashiria kingine cha jumla ni
mfumuko wa bei ambao unapima mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma
zinazotumiwa na kaya nchini. Mfumuko wa bei ulipungua kutoka asilimia
6.5 Januari 2016 hadi asilimia 5.5 Juni 2016 na kupungua zaidi hadi
asilimia 4.5 Septemba 2016 na baadaye kupanda kidogo mwezi Novemba na
kufikia asilimia 4.8. Maana yake ni kuwa bei za bidhaa na huduma
ziliongezeka kwa kasi ndogo zaidi ikilinganishwa na kipindi cha nyuma.
Mwenendo huu wa kushuka mfumuko
ulichangiwa na kasi ndogo ya ongezeko la bei za chakula nchini, kushuka
kwa bei za mafuta ya petroli katika soko la dunia, utekelezaji madhubuti
wa sera za bajeti na fedha, na utulivu wa thamani ya Shilingi. Kupanda
kwa mfumuko wa Bei mwezi Novemba kulitokana na kupungua kwa upatikanaji
wa bidhaa za chakula (mbogamboga, unga wa mahindi na ngano) pamoja na
mkaa.
Mfumuko wa bei katika nchi za
Jumuiya ya Afrika Mashariki: Wastani wa mfumuko wa bei uliendelea
kubakia katika wigo wa tarakimu moja. Hata hivyo, mwezi Novemba 2016,
karibu nchi zote zilikuwa na ongezeko la mfumuko wa bei kutokana na
kuyumba kwa ugavi wa chakula katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki
na kupanda kwa bei za mafuta katika soko la dunia. Nchini Uganda,
mfumuko wa bei uliongezeka kufikia asilimia 4.6 Novemba 2016
ikilinganishwa na asilimia 4.1 Oktoba 2016. Aidha, mfumuko wa bei nchini
Kenya ulipanda na kuwa asilimia 6.68 ikilinganishwa na asilimia 6.47
katika kipindi hicho.
Matarajio kwa mwaka 2017 ni
kubaki na mfumuko wa bei katika kiwango cha tarakimu moja. Hata hivyo
upungufu wa mavuno ya mazao ya chakula uliojitokeza kwa baadhi ya nchi
za ukanda wa kusini mwa Afrika unaweza kusababisha shinikizo la mfumuko
wa bei katika siku za usoni.
- Thamani ya shilingi
Thamani ya shilingi ya Tanzania
dhidi ya Dola ya Kimarekani imeendelea kuimarika. Shilingi imekuwa
ikibadilishwa kwa kati shilingi 2,167 hadi 2,199 kwa dola moja ya
Marekani.
Hali hii ilitokana na kuwa sera
thabiti za uchumi pamoja na mwenendo mzuri wa urari wa mapato ya fedha
za kigeni hususan kutokana na mauzo ya bidhaa za viwandani, utalii na
huduma mbalimbali.
- Mwenendo wa Sekta ya Kibenki
Tathmini ya hali ya mabenki yetu inaonesha kuwa mabenki yetu ni imara na salama, yakiwa na mitaji na ukwasi wa kutosha:
Kiwango cha mitaji
kikilinganishwa na mali iliyowekezwa (total capital to total risk
weighted assets and off-balance sheet exposures) kilikuwa asilimia 18.68
kikilinganishwa na kiwango cha chini kinachotakiwa kisheria cha
asilimia 12.0.
Hali ya ukwasi hupimwa kwa
kuangalia uwiano kati ya mali inayoweza kubadilishwa kuwa fedha taslimu
na amana zinazoweza kuhitajika katika muda mfupi (liquid assets to
demand liabilities). Uwiano huu ulikuwa asilimia 37.46 ukilinganishwa na
uwiano wa chini unaohitajika kisheria wa asilimia 20.
Amana za wateja katika mabenki
zilipungua kidogo kutoka shilingi trilioni 20.73 mwezi Desemba 2015
kufikia shilingi trilioni 20.57 mwezi Septemba 2016. Miongoni mwa sababu
zilizochangia kupungua kwa amana kwenye mabenki ni pamoja na uamuzi wa
Serikali kuhamisha sehemu ya fedha za taasisi na mashirika ya umma
kutoka mabenki ya biashara kwenda Benki Kuu ya Tanzania. Hata hivyo
amana za serikali kwenye mabenki ya biashara ni asilimia 3 tu ya amana
zote za mabenki.
Upatikanaji wa huduma za kifedha
kwa wananchi wasiofikiwa na mabenki umeendelea kuongezeka kutokana na
ubunifu wa mipango ya utoaji wa huduma za malipo ya rejareja kupitia
simu za mikononi, pamoja na huduma za uwakala wa mabenki (agent banking
services).
Benki zilizopata msukosuko:
Katika kipindi cha Julai – Septemba 2016, CRDB na TIB Development Bank
zilipata hasara. Hasara ilisababishwa na tengo kwa ajili ya mikopo
chechefu (provision for loan losses). Aidha, Twiga Bancorp imewekwa
chini ya uangalizi wa BOT, jambo ambalo si geni. Crane Bank Ltd ya
Uganda imewekwa chini ya usimamizi wa Benki Kuu ya nchi hiyo Oktoba 2016
kama ilivyokuwa Imperial Bank Kenya, Oktoba 2015. Licha ya hali hiyo,
benki nyingi zikiwamo CRDB na TIB Development Bank, zimebaki kuwa na
mitaji na ukwasi wa kutosha kwa mujibu wa Sheria. Aidha ni vema
kukumbuka kwamba jumla ya benki na taasisi za fedha nchini kote ni 66 na
zina matawi 783. Hivyo, kwa benki tatu (3) tu kupata msukosuko katika
robo moja ya mwaka si sababu ya kuzua taharuki!
Mwenendo wa mabenki katika nchi
nyingine Afrika: Kupungua kwa mikopo kwa sekta binafsi katika miezi ya
hivi karibuni siyo kwa Tanzania pekee. kwa mfano kiwango cha ukuaji cha
ukuaji wa mikopo kwenda sekta binafsi katika nchi jirani ya Kenya
kilipungua kutoka asilimia 19.7 kati ya Julai na Oktoba 2015 hadi
kufikia asilimia 4.1 katika kipindi kama hicho katika mwaka huu 2016.
Aidha huko Uganda mikopo kwa sekta binafsi ilipungua kutoka asilimia
25.2 mwezi September 2015 hadi asilimia -1 mwezi September 2016. Pia
mwenendo usioridhisha ulijitokeza katika mikopo chechefu katika nchi
hizo jirani na kusababisha baadhi ya mabenki hususan Crane Bank ya
Uganda na Imperial Bank ya Kenya, kuwekwa chini ya uangalizi. Hali ni
mbaya zaidi kwa nchi kama Nigeria na Ghana zinazouza mafuta.
Ujazi wa fedha kwa tafsiri pana
zaidi (M3) ulikua kwa asilimia 4.5 katika kipindi cha mwaka ulioishia
Oktoba 2016 (au ongezeko la shilingi bilioni 547.3) ikilinganishwa na
ukuaji wa asilimia 16.6 (au ongezeko la shilingi bilioni 3,084.6) kwa
mwaka ulioishia Oktoba 2015. Ukuaji mdogo unatokana na usimamizi
madhubuti wa matumizi sambamba na kupungua kwa fedha za misaada na
mikopo kutoka nje.
Kwa upande wa mikopo kwa shughuli
za biashara na za binafsi ilikuwa asilimia 39 ya mikopo yote. Mikopo
kwa sekta binafsi iliongezeka kwa shilingi bilioni 1,550.5 hadi shilingi
bilioni 16,654.4 katika mwaka unaoishia Oktoba 2016, sawa na ukuaji wa
asilimia 10.3 ikilinganishwa ongezeko la shilingi bilioni 2,977.6 au
ukuaji wa asilimia 24.6 katika kipindi kinachoishia Oktoba 2015. Katika
kipindi cha Julai – Oktoba 2016 mwenendo wa riba za amana na za mikopo
umekuwa wa kupanda na kushuka. Wastani wa riba za amana ulikuwa asilimia
9.49 ukilinganisha na wastani wa asilimia 9.08 katika kipindi kama
hicho mwaka 2015. Aidha, wastani wa jumla wa riba za mikopo ulikuwa
asilimia 15.85 ikilinganishwa na asilimia 16.11 katika kipindi kama
hicho mwaka 2015. Mwenendo wa riba za mikopo unategemea mambo mbalimbali
kama vile, gharama ya fedha (cost of funds), gharama za uendeshaji wa
benki husika (bank’s operational cost), kiwango cha faida (profit
margin), mfumuko wa bei na vihatarishi vinavyotokana na sifa za mkopaji
(risk premium). Viwango vya riba katika masoko ya fedha vimeendelea
kutegemea nguvu ya soko na hali ya ukwasi unaotokana na sera za fedha na
kibajeti.
- Sekta ya Nje na Akiba ya Fedha za Kigeni
Hadi kufikia Novemba 2016, nakisi
ya urari wa biashara ya bidhaa, huduma na uhamishaji mali nchi za nje
(current account deficit) ilipungua kwa asilimia 52.5 na kufikia nakisi
ya dola za Kimarekani milioni 1,904.2, kutoka nakisi ya dola za
Kimarekani milioni 4,008.3 katika kipindi kama hicho mwaka 2015.
Kupungua huko kulitokana na ongezeko la thamani ya madini hususan
dhahabu, bidhaa asilia, mapato yatokanayo na utalii, pamoja na kupungua
kwa thamani ya bidhaa zilizoagizwa kutoka nje ya nchi hususan bidhaa za
mitaji, na bidhaa za matumizi ya kawaida. Katika kipindi hicho thamani
ya bidhaa na huduma zilizouzwa nje ya nchi ziliongezeka kwa asilimia 6.4
na kufikia dola za Kimarekani milioni 8,502.8 wakati thamani ya bidhaa
na huduma toka nje zilipungua kwa asilimia 15.4 na kufikia dola za
Kimarekani milioni 9,846.0.
Hadi mwezi November 2016, akiba
ya fedha za kigeni ilifikia dola za Kimarekani milioni 4,254.1 ambazo
zinatosheleza kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa takriban
miezi 4. Wakati huo huo, rasilimali za fedha za kigeni za mabenki (gross
foreign assets) zilikuwa kiasi cha dola za Kimarekani milioni 777.0
Hivyo, akiba ya fedha za kigeni imeendelea kuwa ya kuridhisha.
Jedwali 2: Viashiria vya Ustawi wa Uchumi
ENEO | KIASHIRIA | JUL – SEPT 2015 | OCT – DES 2015 | JUL – SEPT 2016 | OCT – DES 2016 | 2016 | |
Ukuaji wa Uchumi | Ukuaji wa Pato la Taifa | 6.3% | 9.1% | 6.2% | 8.0% | 7.2% | |
Sekta zenye mchango mkubwa ktk Pato la Taifa | Kilimo (35.8%); Ujenzi (12.4%); Biashara (9.7%) | Kilimo (28.3%); Ujenzi (11.0%); Biashara (10.7%); Viwanda (6.3%) | Kilimo (24.7%); Ujenzi (14.6%); Biashara (10.3%); Viwanda (7.3%); Madini (5.2%) | ||||
Sekta zilizokua haraka | Ujenzi (17.6%); Usafirishaji & Uhifadhi (10.6%); Mawasiliano (9.1%); Huduma za kifedha (8.4%); Madini (8.0%) | Madini (15.750; Ujenzi (13.8%); Huduma za kifedha (12.6%); Mawasiliano (10.2%); Viwanda (9.5%) | Madini (19.9%); Mawasiliano (14.3%); Usafirishaji (12.2%); Nishati (11.8%); Huduma za kifedha (8.7%); | ||||
Sekta zilizokua polepole | Kilimo (2.7%); | Kilimo (0.3%) | |||||
Bei, Biashara na Masoko | Mfumuko wa bei | 5.3% | 6.6% | Jul (5.1%)
Ago (4.9%) Sep (4.5% |
Okt (4.5%), Nov (4.8%) | 5.5% | |
Nakisi kwenye Biashara ya Nje (US$ Milioni) | |||||||
Mwenendo wa Sekta ya Fedha | Akiba ya fedha za Kigeni (US$ milioni) | 3,999.3 | 4,093.7 | 4,096.0 | 4,254.1 | 4,654.2 | |
Kiwango cha Kubadilisha Fedha (Tshs; 1US$) | 2,150.0 | 2,148.5 | 2,175.32 | 2,170.97 | |||
Uwiano wa mikopo na Amana za wateja katika mabenki | 77.16 | 78.88% | 71.16% | ||||
uwiano wa jumla ya mitaji na mali iliyowekezwa (Total capital/Total risk weighted assets) | Sept (18.68%) | 19.4% (Des) | Sept (18.68%) | 12% | |||
uwiano wa raslimali inayoweza kubadilishwa kirahisi kuwa fedha taslim na amana zinazohitajika katika muda mfupi (Liquid assets/Demand liabilities) | Sept (37.46%) | Des (37.18%) | Sept (37.46%) | 20% | |||
Riba za Mikopo ya mwaka mmoja | Sept (14.4%) | Okkt (14.27%) | Sept (13.4%) | Okt (13.23%) | |||
Riba za amana za mwaka mmoja | Sept (10.6%) | Okt (10.95%) | Sept (11.5%) | Okt (11.46%) | |||
Amana za wateja | Sept (Tshs19.892 trillion) | Okt (Tshs19.995 trillion) | Sept (Tshs20.73 trillion) | Okt (Tshs20.98 trillion) | |||
Mikopo chechefu | Sept (6.62) | Des (6.64) | Sept (8.26) |
- MWENENDO WA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA SERIKALI 2016/17
- Mwenendo wa Mapato
Katika mwaka wa fedha 2016/17
Serikali ilipanga kukusanya na kutumia shilingi bilioni 29.539.6.
Katika kipindi cha miezi mitano ya kwanza ya mwaka 2016/17, makusanyo
ya ndani ikijumuisha mapato ya Halmashauri yalifikia shilingi bilioni
7,018.7 sawa na asilimia 96.4 ya makadirio ya shilingi bilioni 7,281.2
katika kipindi hicho.
- Mapato ya kodi
Mapato ya kodi yalifikia shilingi
bilioni 5,674.7 ikiwa ni asilimia 96.6 ya lengo la kukusanya shilingi
bilioni 5,873.3 kwa kipindi hicho. Aina za kodi zilizofanya vizuri ni
pamoja na kodi ya Ongezeko la thamani ndani, ushuru wa forodha na ushuru
wa bidhaa nje. Hii ilitokana na usimamizi thabiti wa makusanyo kwenye
malimbikizo ya kodi, ukaguzi na uchunguzi wa marejesho ya kodi ya
Ongezeko la Thamani (VAT returns) na kodi ya mapato uliofanyika katika
kipindi hicho, kupanua wigo wa kodi kwa kusajili walipa kodi wapya,
pamoja na utekelezaji wa mikakati ya kuongeza makusanyo ya kodi.
- Mapato yasiyotokana na kodi
Mapato yasiyotokana na kodi
yalifikia shilingi bilioni 1,133.4 sawa na asilimia 0.2 zaidi ya lengo
la kukusanya shilingi bilioni 1,130.6. Sababu za kuvuka lengo ni
kutokana na kuongezeka kwa mapato yasiyo ya kodi yanayokusanywa na TRA
ikijumuisha kodi ya majengo pamoja na kufanya vizuri kwa Wizara na Mikoa
zinazokusanya maduhuli.
- Aina za kodi ambazo hazikufikia lengo
Aidha, aina za kodi ambazo
hazikufikia lengo ni pamoja na ushuru wa bidhaa ndani, kodi ya Ongezeko
la Thamani (VAT) nje, kodi ya mapato na kodi nyingine hasa ushuru wa
stamp (stamp duty) na Departure fee.
Sababu zilizopelekea kutokufikiwa kwa malengo la ukusanyaji wa mapato ya kodi:
- Kushuka kwa mauzo ya bidhaa mbalimbali kama vile saruji, bia, vinywaji baridi na bidhaa nyinginezo za jumla na rejareja kumesababisha makampuni mengi kutopata faida ilivyotarajiwa na hivyo kupunguza wigo wa ukusanyaji wa kodi;
- Mabenki makubwa yalifanya marekebisho ya makisio yao ya kulipa kodi kutokana na kushuka kwa mapato ya riba;
- Kupungua kwa uchimbaji wa madini, mafuta na gesi asilia ambako kuliathiri kodi ya zuio na kodi ya mapato;
- Ajira kutoongeza kama ilivyotarajiwa baada ya kusitisha ajira mya ili kupisha zoezi la kubaini watumishi hewa serikalini;
- Baadhi ya kampuni kupunguza bei katika baadhi ya bidhaa kama vile bia ili kuongeza mauzo yao;
- Kuongezeka kwa malimbikizo ya Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye sekta ya uzalishaji wa umeme hususan IPTL na Symbion Power Ltd;
- Matumizi hafifu ya mashine za kielektroniki (EFD);
- Kupunguza kwa ulaji wa bidhaa zinazotozwa kodi na ushuru wa bidhaa husuan bia, vinywaji vikali na vinywaji baridi;
- Matatizo ya kifedha yaliyokumba kampuni za usafirishaji wa anga pamoja na kupungua kwa idadi ya wasafiri hususan wa sekta ya umma (departure charges); na
- Kushuka kwa uingizaji wa bidhaa kutoka nje.
Hatua za kuimarisha ukusanyaji wa kodi ili kufikia malengo katika kipindi kilichobaki cha mwaka 2016/17:
- Kupanua wigo wa kodi kwa kuendelea kusajili na kuhakiki taarifa za walipakodi kwenye mifumo ya kikodi ya TRA;
- Kuendelea kushirikiana na Taasisi nyingine za ndani na nje ya nchi kwa kubadilishana taarifa;
- Kuendelea kusimamia na kuhamasisha matumizi sahihi ya mashine za kielektroniki za kutolea risiti (EFDs);
- Kudhibiti udanganyifu katika ukadiriaji wa kodi kwa kuendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwa walipakodi;
- Kuimarisha ukaguzi wa kodi (tax audit);
- Kudhibiti na kusimamia bidhaa zinazopitia hapa nchini kwenda nchi jirani (transit) kwa kutumia mfumo wa kufuatilia mizigo (electronic cargo trackin system);
- Kuboresha ukaguzi wa mizigo bandarini; na
- Kudhibiti biashara ya magendo hususan katika Bahari ya Hindi, mipaka na njia zisizo rasmi kati ya nchi yetu na nchi jirani.
- Misaada na Mikopo Yenye Masharti Nafuu
Katika mwaka 2016/17 Washirika wa
Maendeleo waliahidi kuchangia bajeti ya Serikali kwa kiasi cha shilingi
bilioni 3,600.8, ambapo kati ya hizo, misaada ya Kibajeti ni shilingi
bilioni 483.0, Mifuko ya Kisekta ni shilingi bilioni 372.1 na miradi ya
Maendeleo ni shilingi bilioni 2,745.7. Jumla ya misaada na mikopo nafuu
iliyotolewa kwa kipindi cha Julai hadi Novemba 2016 ni shilingi bilioni
603.9 sawa na asilimia 21.5 ya lengo la shilingi bilioni 2,806.3 katika
kipindi hicho.
Misaada: Kati ya Julai hadi
Novemba 30, 2016, misaada ya kiasi cha shilingi bilioni 287.5 ilitolewa,
sawa na asilimia 28.4 ya lengo la shilingi bilioni 1,012.6 kwa kipindi
hicho. Kati ya kiasi hicho, misaada ya kibajeti (General Budget Support)
ni shilingi billioni 36.1 ambazo zote zimetolewa na EU tu; na kiasi
kilichopokelewa kwa ajili ya mifuko ya kisekta (Basket Funds) ni
shilingi bilioni 58.4, sawa na asilimia 61 ya lengo ya shilingi bilioni
95.5 kwa kipindi hiki cha marejeo. Aidha, misaada kwa ajili ya miradi
ya maendeleo kwa kipindi hicho ilifikia shilingi bilioni 193.1, ambayo
ni asilimia 21 ya lengo la shilingi bilioni 917.1 kilichotarajiwa
kupokewa kwa kipindi hicho.
Mikopo nafuu iliyopokelewa kutoka
kwa washirika wa maendeleo kwa ajili ya miradi ya maendeleo kati ya
Julai hadi Novemba, 2016 ni shilingi bilioni 316.4. Kiasi hiki ni sawa
na asilimia 17.6 ya lengo la shilingi bilioni 1,793.7. Aidha, katika
kipindi hicho, hakuna mikopo nafuu iliyopokelewa kwa ajili ya mifuko ya
kisekta na programu (GBS).
Sababu za kutofikiwa malengo ya
upatikanaji wa misaada na mikopo nafuu ni pamoja na masharti magumu
yaliyowekwa na wahisani/wakopeshaji. Hata hivyo, Serikali inatarajia
kukamilisha majadiliano na AfDB kati ya mwezi Desemba 2016 hadi Machi,
2017. Aidha, majadiliano na Benki ya Dunia na Umoja wa Ulaya, bado
yanaendelea. Kuhusu fedha za miradi, jitihada zinafanyika katika sekta
husika kukamilisha taarifa za miradi zinazohitajika na wafadhili.
- Mikopo ya ndani
Katika kipindi cha Julai – Oktoba
2016, shilingi bilioni 1,367.2 zilikopwa katika soko la ndani. Kati ya
kiasi hicho, shilingi bilioni 1,305.7 zilikopwa kwa ajili ya kulipia
dhamana na hatifungani za Serikali zilizoiva na shilingi bilioni 61.5
zilikuwa ni malipo ya marejesho (repayment). Kiasi kilichokopwa katika
kipindi hiki ni sawa na asilimia 58 ya kiasi kilichopaswa kukopwa cha
shilingi bilioni 2,232.5.
- Mikopo ya Kibiashara
Katika mwaka 2016/17, Serikali
ilipanga kukopa fedha kutoka kwenye vyanzo vya kibiashara kiasi
cha Dola za Kimarekani milioni 936 sawa na shilingi
bilioni 2,100.9 ili kugharimia miradi mbalimbali ya maendeleo. Hata
hivyo, hadi kufkia Novemba, 2016 Serikali haikukopa kutoka katika chanzo
hiki kutokana na hali ya soko la fedha la kimataifa kutokuwa nzuri hasa
katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2016/17.
Hali hii ilisababishwa na mdodoro
wa kiuchumi katika bara la Ulaya na hivyo kuongezeka kwa gharama za
mikopo mipya na kuathiri upatikanaji wake. Mfano, riba ilipanda kutoka
wastani wa asilimia 6 hadi asilimia 9. Kutokana na sababu hiyo, Serikali
iliahirisha kuendelea na mchakato wa kukopa kutoka kwenye masoko hayo
na badala yake ikajielekeza kukopa kutoka nchi nyingine (China, India,
Korea Kusini, Japan). Aidha, gharama za ukopaji katika masoko ya ulaya
imeanza kuimarika na hivyo Serikali imeanza majadiliano na Benki ya
Credit Suissuie ya Uingereza ili tuweze kukopa dola za kimarekani
milioni 300. Vilevile majadiliano na taasisi nyingine za fedha
kama Kuwait Fund, Abu Dhabi Fund na OPEC yameendelea kwa ajili ya
kugharamia miradi mbalimbali.
- Mwenendo wa Matumizi
Sera za Bajeti ya Serikali kwa
mwaka 2016/17, zililenga kusimamia nidhamu ya matumizi ya fedha za umma
kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu pamoja na miongozo mbalimbali.
Lengo kuu ni kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, kuziba mianya ya
uvujaji wa fedha za umma na kuelekeza kiasi kikubwa cha fedha kwenye
miradi ya maendeleo.
Fedha zilizotolewa Julai – Novemba, 2016
Katika kipindi cha Julai –
Novemba, 2016 jumla ya Shilingi bilioni 9,481.260 zilitolewa na Hazina
kwa Wizara, Idara Zinazojitegemea, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za
Serikali za Mitaa.
- Shilingi bilioni 7,295.455 zilizotolewa kwa ajili ya matumizi ya Kawaida (ikijumuisha makusanyo ya Halmashauri Shilingi 61.047)
- Mishahara ya Watumishi wa Serikali Shilingi 2,834.695,
- Deni la Taifa Shilingi bilioni 3,552.249
- Matumizi Mengineyo Shilingi bilioni 928.511
- Shilingi bilioni 2,185.805 kwa ajili ya Matumizi ya Maendeleo (ikijumuisha makusanyo ya Halmashauri shilingi bilioni 91.571)
- Fedha za ndani Shilingi bilioni 1,749.047
- Fedha za nje Shilingi bilioni 436.758
- Maeneo ya Msingi ambayo fedha zimeelekezwa
Matumizi ya kawaida yaliyopewa kipaumbele zaidi katika utoaji wa fedha kwa kipindi cha Julai – Novemba 2016 ni pamoja na:
- Uboreshaji wa huduma za afya katika ngazi zote ikiwemo ununuzi wa dawa na vifaa tiba Shilingi bilioni 69.346;
- Mitihani ya darasa la nne na saba Shilingi bilioni 33.745;
- Mitihani ya kidato cha pili na nne Shilingi bilioni 31.051;
- Posho ya chakula kwa askari wa vyombo vya ulinzi na usalama;
- Chakula cha wafungwa Shilingi bilioni 7.5;
- Mishahara ya watumishi wa Serikali;
- Elimu msingi bila malipo Shilingi bilioni 93.885 (kwa kutenga shilingi bilioni 18.777 kila mwezi);
- Malipo ya posho na stahili mbalimbali kwa maafisa katika balozi zetu nje shilingi bilioni 23.127;
- Ruzuku ya pembejeo shilingi bilioni 10.00;
- Ununuzi wa chakula cha Hifadhi ya Taifa shilingi biliioni 9.00.
- Deni la kuchapisha Vitabu vya Hati za Kusafiria Shilingi 2.569;
- Uendeshaji wa vikao vya Kamati za Kudumu za Bunge, Mkutano wa Bunge, Posho ya Jimbo kwa Wabunge pamoja na shughuli za Mfuko wa Bunge Shilingi bilioni 31,137;
- Michango ya Taasisi na Jumuiya za Kimataifa Shilingi billion 8.833;
- Ruzuku ya Vyama vya Siasa Shilingi bilioni 7.168;
Aidha, sehemu iliyosalia ya fedha
za Matumizi ya Kawaida ilielekezwa kwenye shughuli za kila siku za
uendeshaji katika Mafungu mbalimbali.
Matumizi ya Maendeleo yaliyopewa kipaumbele kwa kipindi cha miezi mitano ni pamoja na:
- Ununuzi wa ndege mbili za Serikali Shilingi bilioni 103.386 na malipo ya awali ya ununuzi wa ndege 4 shilingi bilioni 91.533;
- Usambazaji wa umeme vijijini Shilingi bilioni 266.493;
- Ujenzi na ukarabati wa barabara Shilingi bilioni 335.931;
- Usambazaji wa maji vijijini na mijini Shilingi bilioni 65.2445;
- Mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu Shilingi bilioni 210.758;
- Mfuko wa Reli Shilingi bilioni 42.404;
- Upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Dodoma na Mwanza Shilingi bilioni 12.353;
- Ujenzi wa majengo ya utawala katika Wilaya mpya na Mamlaka za Serikali za Mitaa Shilingi bilioni 11.00;
- Ujenzi na ukarabati wa ofisi za Halmashauri Shilingi bilioni 30.10;
- Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo Tanzania bara Shilingi bilioni 9.0; na
- Uboreshaji wa miundombinu ya shule za wanafunzi wenye mahitaji maalum Shilingi bilioni 2.5.
- Ulipaji wa Madai mbalimbali
Katika kipindi cha Julai –
Novemba, 2016 madai yaliyohakikiwa ya jumla ya Shilingi bilioni 318.556
yalilipwa, ambapo shilingi bilioni 183.714 ni kwa ajili ya Wakandarasi
na Wahandisi Washauri wa miradi ya barabara; Shilingi bilioni 42.951 kwa
ajili ya ujenzi wa miradi ya maji; Shilingi bilioni 30.00 kwa ajili ya
mikataba ya ulinzi na usalama; Shilingi bilioni 25.00 kwa ajili ya
miradi ya umeme; Shilingi bilioni 15.439 kwa ajili ya wazabuni
mbalimbali; shilingi bilioni 10.00 kwa ajili ya madai ya watumishi;
Shilingi bilioni 7.00 kwa ajili ya matibabu nje ya nchi (Hospitali ya
Apollo, India); Shilingi bilioni 3.150 kwa ajili ya Mtaalam Mwelekezi wa
mipango miji ya jiji la Arusha na Mwanza; na shilingi bilioni 1.302
kwa ajili ya ujenzi wa majengo mbalimbali ya Serikali.
- Deni la Taifa
Deni la Taifa limeendelea
kuongezeka na kufikia dola za Kimarekani milioni 21,087.9 mwishoni mwa
mwezi October 2016, kutoka dola za Kimarekani milioni 19,861.1 mwezi
Desemba 2015.
Deni la nje liliongezeka kwa
asilimia 3.4 na kufikia dola za Kimarekani milioni 16,407.6 mwezi
October 2016 (sawa na asilimia 77.8 ya deni la taifa), kutoka dola za
Kimarekani milioni 15,863.9 mwezi Desemba 2015. Hii ilitokana na
kuongezeka kwa mikopo mipya pamoja na malimbikizo ya malipo ya madeni.
Katika deni hilo la nje, asilimia 83.0 ni deni la Serikali na taasisi za
umma.
Deni la ndani liliongezeka
kufikia shilingi bilioni 10,089.3 mwishoni mwa mwezi Octoba 2016 kutoka
shilingi bilioni 8,597.0 mwezi Desemba 2015. Ongezeko hilo lilitokana na
Serikali kukopa kupitia dhamana na hati fungani kwa ajili ya kugharamia
bajeti ya Serikali kwa mwaka 2015/16, ikichangiwa pia na kupungua kwa
misaada na mikopo kutoka nje.
Deni la Taifa ni himilivu: Pamoja
na kuongezeka huko, deni la Taifa bado ni himilivu. Uchambuzi wa
Uhimilivu wa Deni uliofanyika mwezi Novemba 2016 unaonesha kuwa
viashiria vya deni la nje na deni lote la umma viataendelea kuwa chini
ya ukomo wa uhimilivu katika kipindi cha muda mfupi, muda wa kati na
muda mrefu. Uchambuzi unaonesha kuwa viashiria vyote vitaendelea kuwa
chini ya ukomo wa kimataifa hivyo deni la Taifa ni himilivu.
- Changamoto
Pamoja na mafanikio hayo, changamoto kadhaa zilijitokeza zikiwemo:-
- Baadhi ya wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla kutokuwa na mwamko wa matumizi ya mashine za kielektroniki;
- Ukusanyaji usioridhisha wa maduhuli ya Serikali;
- Kushindwa au kuchelewa kupatikana kwa mikopo yenye masharti nafuu na ya kibiashara kutoka nje;
- Maombi ya misamaha ya kodi; na
- Mahitaji makubwa (yasiyowiana na hali halisi ya upatikanaji wa mapato) ya kuboresha miundombinu hususan ya maji, reli, bandari, viwanja vya ndege na barabara;
- MAENEO YANAYOLALAMIKIWA NA BAADHI YA MAGAZETI NA KWENYE MITANDAO
4.1 Kupungua kwa Ukwasi Kufuatia Uamuzi wa Serikali Kuzitaka Taasisi za Umma Kufungua Akaunti za Mapato Benki Kuu
Uamuzi wa Serikali kuzitaka
taasisi za umma kufungua akaunti ya mapato Benki Kuu utaendelea kubaki
kama ulivyo. Kwa kifupi, fedha hizi za umma zilikuwa zinatumika vibaya
na Bodi za mashirika lakini pia zilitumika kuikopesha Serikali fedha
zake yenyewe kwa riba kubwa kupitia biashara ya dhamana na hati fungani
za Serikali. Kasoro hiyo iliondoa motisha kwa mabenki ya biashara
kupeleka huduma za kifedha vijijini na hata kukopesha sekta binafsi
(crowding out credit to the private sector).
Aidha, ni vyema jamii ya
Watanzania ikafahamu kwamba akaunti ambazo fedha za mashirika
zimehamishiwa Benki Kuu ni akaunti za kukusanya mapato tu. Akaunti za
matumizi bado ziko katika benki za biashara ili kuyawezesha mashirika
kufanya malipo kupitia akaunti hizo. Hivyo, bado benki za biashara ni
kiungo muhimu kati ya mashirika ya umma na watoa huduma kwa mashirika
hayo. Hatua iliyochukuliwa na Serikali inalenga kuzisukumu benki za
biashara kuchukua hatua za ziada kupanua huduma za kifedha hadi vijijini
badala ya kujikita mijini zaidi kuhudumia makampuni makubwa (corporate
sector) na kufanya biashara katika soko la dhamana na hati fungani za
Serikali.
4.2 Mkikimkiki wa Ukusanyaji Kodi umekimbiza Wapangaji wa Majengo Marefu na Kusababisha Biashara Nyingi Kufungwa
Taarifa kutoka Mfuko wa Pensheni
wa PPF zinaonesha kuwa kati ya majengo 15 inayomiliki sehemu mbalimbali
nchini, mtiririko wa wastani wa wapangaji uko kama ifuatavyo:
- Majengo saba (7) yana wapangaji kwa asilimia 100 hadi kufikia Desemba 14, 2016;
- Jengo moja (DICC – PPF Tower) kwa sasa halipangishwi bali linaendeshwa na PPF wenyewe kama ukumbi wa mikutano;
- Jengo moja (PPF Plaza – Arusha) ni jipya na idadi ya wapangaji imeshaanza kuongezeka kutoka asilimia 34 mwezi Machi 2016 lilipofunguliwa hadi asilimia 39.1 Desemba 2016;
- PPF Kijitonyama ina nyumba nne (4) na kati ya hizo, mbili tu zenye wapangaji. Hatua za kutafuta wapangaji zinaendelea;
- PPF Kaloleni Arusha ina nyumba 20 na mwenendo wa wapangaji ulikuwa ukipanda na kushuka na katika kipindi kilichoishia Desemba 2016 umeongezeka kufikia asilimia 75 kutoka asilimia 65 mwezi Juni 2016;
- Majengo manne yaliyobaki (PPF Tower and Parking Arcade, PPF Plaza Mwanza, PPF House na PPF Olerien Estate) idadi ya wapangaji ilipungua na kufikia wastani wa asilimia 78.5 kwa yote katika kipindi kilichoishia Desemba 2016 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 84.8 Juni 2016.
Aidha, taarifa kutoka PSPF
zinaonesha kuwa katika majengo manne (4) inayomiliki imeweza kukodisha
jumla ya futi za mraba 58,119.33 katika kipindi kilichoishia Juni 2016
ikilinganishwa na futi za mraba 57,883.5 zilizokodishwa hadi Juni 2015,
sawa na ongezeko la asilimia 0.4. Katika kipindi hicho kilichoishia Juni
2016, eneo lililokodishwa katika majengo ya Jubilee na PSPF Plaza
lilipungua kwa asilimia 4.7 na 2.7 kwa mtiririko huo wakati ambapo
katika majengo ya HIP na Ubungo Plaza kulikuwa na ongezeko la eneo
lililopangishwa kwa asilimia 20.9 na 1.3 mtawalia.
Ni dhahiri kuwa, kwa ujumla,
kumekuwa na ongezeko la ushindani katika sekta ya nyumba na majengo
kufuatia kuongezeka kwa ujenzi unaofanywa na mashirika na taasisi
mbalimbali za umma na binafsi. Hali hii ilipelekea baadhi ya wamiliki wa
majengo hayo kubuni mbinu mbalimbali za kibiashara ikiwa ni pamoja na
kubadili matumizi ya majengo hayo na pia kuweka viwango vya kodi ya
pango vinavyoendana na hali halisi ya soko. Kwa kuzingatia takwimu za
hapo juu ni wazi kuwa madai kwamba mkikimkiki wa ukusanyaji kodi ndiyo
umekimbiza wapangaji hayana mashiko.
Madai ya biashara nyingi
kufungwa: Kwa upande wa madai ya biashara nyingi kufungwa katika siku za
karibuni, tumefuatilia na kwa kiasi fulani kuna ukweli. Imebainika
kwamba kasi ya wafanyabiashara kufunga biashara zao imeongezeka kati ya
mwezi Agosti na Oktoba 2016. Mfano Ilala 1,076, Kinondoni 443, Temeke
222 na Arusha 131. Aina ya biashara nyingi zilizofungwa ni katika sekta
ya ujenzi na biashara ya jumla na rejareja, na chache katika huduma za
usafiri.
Hata hivyo, sababu hasa
zilizopelekea biashara hizo kufungwa hazijabainika kutokana na ugumu wa
kupata taarifa kutoka kwa wenye biashara zilizofungwa. Sababu za mtu
kufunga biashara yake zinaweza kuwa nyingi, ikiwemo, kushindwa kuingiza
bidhaa nchini bila kulipa kodi stahiki, kushindwa kulipa au kulipwa
madeni, kubadilisha aina ya biashara, kushindwa kusimamia biashara,
gharama kubwa za uendeshaji, wabia katika biashara kutoelewana au
kutapeliana, kuibuka kwa washindani wa kibiashara wenye nguvu au huduma
bora zaidi n.k.
4.3 VAT Imekimbiza Watalii
Takwimu rasmi kuhusu wageni
walioingia nchini katika mwaka 2016 kwa ujumla zinaonyesha kuwa idadi ya
wageni imeongezeka ikilinganishwa na mwaka 2015 (Jedwali 4). Hivyo
madai kuwa watalii wameikimbia Tanzania kwa sababu ya VAT kwenye baadhi
ya huduma za utalii hayana msingi! Na kama nia ni kutolipa kodi na
wakati huohuo Serikali inadaiwa fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu
ya utalii na huduma nyingine kwa wananchi, hilo halikubaliki! Nawaalika
wadau wa sekta ya utalii waje wajenge hoja zenye mashiko wakati wa
mapitio ya marekebisho ya kodi kwa ajili ya bajeti ya 2017/18.
Jedwali 4a: Idadi ya Wageni walioingia Nchini 2015 – 2016
Mwezi | 2015 | 2016 | Badiliko % |
Januari | 98,710 | 99,763 | 1 |
Februari | 88,939 | 91,519 | 3 |
March | 77,841 | 93,096 | 20 |
Robo ya Kwanza | 265,490 | 284,378 | 7 |
Aprili | 67,447 | 76,679 | 14 |
Mei | 81,538 | 76,155 | -7 |
Juni | 90,236 | 89,626 | -1 |
Robo ya Pili | 239,221 | 242,460 | 1 |
Julai | 91,896 | 126,755 | 38 |
Agosti | 142,885 | 121,321 | -15 |
Septemba | 100,829 | 121,279 | 20 |
Robo ya Tatu | 335,610 | 369,355 | 10 |
Octoba | 84,121 | 124,623 | 48 |
Jedwali 4b: Idadi ya Wageni waliongia nchini kupitia njia mbalimbali ;
Januari – Septemba
KITUO | 2015 | 2016 | Badiliko % |
JNIA | 238,423 | 252,524 | 5.91 |
KIA | 126,286 | 137,024 | 8.50 |
ZIA | 109,738 | 139,284 | 26.92 |
Namanga | 105,883 | 81,073 | (23.43) |
Kasumulo | 9,871 | 12,006 | 21.63 |
Sirari | 18,899 | 24,393 | 29.07 |
Zanz. Port | 31,994 | 43,242 | 35.16 |
Kabanga | 13,565 | 16,751 | 23.49 |
Manyovu | 17,761 | 18,550 | 4.44 |
- MWELEKEO NA MATARAJIO HADI JUNI 2017
Kwa kuzingatia mwenendo wa
ukuaji wa uchumi kwa kipindi cha Januari hadi September 2016, matarajio
ni kwamba kasi ya ukuaji wa uchumi kwa mwaka 2016/17 unatarajiwa kufikia
asilimia 7.2 kama ilivyokadiriwa awali.
Mfumuko wa bei unatarajiwa kuendelea kubaki kwenye tarakimu moja.
Thamani ya shilingi inategemea
kuendelea kuimarika kutokana na hatua zinazoendelea kuchukuliwa na
Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania.
Kwa upande wa mapato, Serikali inakusudia kufanya yafuatayo hususan katika kuongeza mapato ili kuweza kufikia lengo:
- Kusimamia dhana ya kulipa kodi kwa hiari kupitia udhibiti wa matumizi ya mfumo wa EFDs;
- Kuendelea kuboresha makusanyo ya mapato yasiyo ya kodi hasa yale yanayotokana na michango ya mashirika na wakala za Serikali;
- Kuendelea na majadiliano baina ya serikali na wahisani ili kuhakikisha kwamba fedha za misaada na mikopo zinapatikana kama ilivyopangwa;
- Kuendelea kufanya uthamini wa mkupuo wa majengo ili kukusanya zaidi katika kodi ya majengo;
- Kuendelea kuboresha na kuimarisha mifumo ya ukusanyaji na usimamizi wa maduhuli; na
- Kuendelea kutoa elimu juu ya umuhimu na faida za kulipa kodi kwa kutumia mitandao ya kielektroniki. Aidha, MDAs zinahimizwa kutumia mabenki katika kulipia maduhuli.
Aidha, Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kusimamia matumizi kama ifuatavyo:-
(i) Kuendelea kusisitiza
nidhamu katika utekelezaji wa bajeti kama ilivyoidhinishwa kwa
kuzingatia Sheria ya Bajeti ya mwaka 2015;
(ii) Kuendelea kuwianisha
mapato na matumizi kwa kuhakikisha kuwa mgawo wa fedha utaendana
na upatikanaji wa mapato; (iii) Kupunguza matumizi yasiyo ya lazima
kama kupunguza safari za nje zisizo na tija, matumizi katika
sherehe za kitaifa pamoja na makongamano.
- HITIMISHO
Ninapohitimisha maelezo yangu naomba kusisitiza yafuatayo:
Kwanza: napenda kuwahakikishia
wafanyabiashara kuwa Serikali ya awamu ya Tano inathamini sana mchango
wa Wafanyabiashara katika Maendeleo ya nchi yetu. Milango ya serikali
ipo wazi kwa wale wote wenye hoja zenye maslahi kwa Taifa letu. Wizara
ya Fedha na Mipango imekwisha toa tangazo kwa Watanzania na wadau wote
wa kodi kuwasilisha mapendekezo ya marekebisho ya kodi kwa ajili ya
uchambuzi na kufikiriwa kuingizwa katika mapendekezo ya mabadiliko ya
kodi katika bajeti ijayo. Ninawaomba wadau wote kuitumia vizuri fursa
hiyo ili tupate mapendekezo mazuri ya kuboresha mfumo wetu wa kodi na
kutupatia mapato zaidi ya kuendeleza nchi yetu.
Pili: Napenda kutoa rai kwa
Watanzania wenzangu kuhakikisha kuwa tunadai risiti za EFD kila
tunaponunua bidhaa au huduma kama Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alivyokwisha kuagiza. Yeyote
asiyetoa risiti na asiyedai risiti ajue anatenda kosa na anasaliti
jitihada zetu za kuijenga Tanzania mpya. Aidha, ningependa kusisitiza
kwa wale wote wenye mashine za EFD wazitumie ipasavyo kwa kila muamala
wanaoufanya. Kuna tabia ambayo imezuka ya kusingizia kuwa mashine
imeharibika au kutoa risiti ya EFD kwa mteja anayeidai tu. Wale wote
wenye tabia hii wanahujumu maendeleo ya nchi yetu na ninawataka waache
mara moja! Nimewaagiza TRA kufanya kaguzi za kushtukiza na
kuwashughulikia ipasavyo wale wasiotaka kutii maelekezo ya Serikali kwa
mujibu wa sheria za nchi.
Napenda nisisitize kuwa Tanzania
mpya ambayo wote tunaitamani iko mikononi mwetu! Lakini ili tufike huko
lazima tufanye kazi kwelikweli – iwe ni kazi ya kuajiriwa au kujiajiri
katika kilimo, uvuvi, ufugaji, biashara au huduma au kumiliki viwanda
(vidogo, vya kati na vikubwa)!! Aidha, lazima kila mmoja wetu alipe kodi
stahiki kwa ajili ya maendeleo ya Tanzania yetu! Tuitikie wito wa Rais
wetu kwa vitendo ambaye amedhamiria kujenga Tanzania mpya ili kuwaondoa
Watanzania kwenye lindi la umaskini haraka. Kulipa kodi ndiyo njia ya
uhakika ya kuiwezesha Serikali kutoa huduma bora zaidi (upatikanaji wa
maji, elimu, afya, umeme, barabara, ulinzi & usalama) kwa wananchi
wake. Uamuzi huu unahitaji kuachana na mazoea, kujitoa (sacrifice) na
kufanya kazi kwa bidii, nidhamu na uadilifu. Tunataka uchumi ambao
wananchi wengi wananufaika nao, uchumi ambao utajengwa kwa kufanya kazi
siyo uchumi wa ujanja ujanja (mission town), kukwepa kodi au wizi wa mali na fedha za umma.
Tatu: Wanahabari kwa ujumla
mnafanya kazi nzuri sana. Nawaomba mwendelee hivyo na hasa nikiwasihi
mtumie weledi na mjielekeze kuwajuza Watanzania kuhusu mifano mizuri ya
maendeleo hapa nchini na hata katika nchi nyingine lakini wakati huo huo
mtangulize maslahi ya Taifa letu kwanza. Hata hivyo, yapo magazeti
fulani ambayo consistently yanajielekeza kutoa taarifa za kupotosha na
kuifanya jamii ihamaki! Nawaomba: Epukeni kuwa vipaaza sauti vya nyimbo
za watu wachache wenye maslahi binafsi (wawe wanasiasa, wafanyabiashara,
au wafanyakazi) waliozoea “upigaji”! Punguzeni uandishi wa kuuza
magazeti (sensationalism) na uchambuzi wa mambo kijuujuu! Pimeni
taarifa mnazoziandika ili msiwanufaishe washindani wa nchi yetu kiuchumi
(kibiashara au kiuwekezaji) au kuchafua sura nzuri ya Tanzania!!
Nimalizie kwa kuwahakikishia
Watanzania wote kwamba madai ya baadhi ya magazeti siku za karibuni
kuwa uchumi wa Taifa una hali mbaya siyo ya kweli. Hata gazeti moja la
leo limeandika kuwa “Ripoti ya Uchumi Yashtua”!! Ukweli ni kuwa kama
Taifa tumeendelea kupiga hatua nzuri katika maeneo mengi ya uchumi japo
yapo maeneo machache ambayo yana changamoto, na Serikali inaendelea
kuyafuatilia kwa karibu ili kuyatafutia ufumbuzi. Afya ya uchumi wetu
bado ni nzuri na inatarajiwa itaendelea kuwa ya kuridhisha katika mwaka
ujao 2017.
NAWATAKIA WOTE HERI YA MWAKA MPYA 2017
UWE KWELI MWAKA WA HAPA KAZI TU!!
ASANTENI KWA KUNISIKILIZA
No comments :
Post a Comment