Monday, December 19, 2016

TUME ya nguvu za Atomiki (TAEC) yazitaka taasisi mbalimbali zinazotumia mionzi kutekeleza maelekezo

bd
TUME ya nguvu za Atomiki (TAEC) imezitaka taasisi mbalimbali za umma na binafsi  ambazo zinatumia  mionzi kwenye shughuli zao kuhakikisha vituo vyote  vinatekeleza maelekezo yaliyotolewa na wakaguzi  ikiwemo kuwa na leseni kabla ya Julai ya kila mwaka ndipo viruhusiwe kutoa huduma.
Agizo hilo limetolewa Desemba 16 na Kaimu mkurugenzi mkuu wa Tume ya Atomiki, (TAEC) Brigedia Jeneral Fulgence Simon Msafiri, aliokuwa akifunga mafunzo ya wiki moja  kuhusu matumizi salama ya vyanzo vya mionzi, kwa watumishi wa hospital , usafirishaji salama wa vyanzo vya mionzi  yaliyofanyika kwa watu wa viwandani na migodini.
Amesema mafunzo hayo yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Tume hiyo iliyopo Njiro jijini Arusha,  ili kituo kiweze kutoa huduma inayotegemea nguvu ya mionzi lazima  kiwe kimekaguliwa na kutekeleza maelekezo ya wakaguzo ikiwemo pia kuwa na mashine zenye ubora ,vyumba bora  na madhubuti ili kuzuia mionzi isipenye na kusababisha madhara  pamoja na kuwa na wataalamu waliofunzwa sawa sawa.
Brigedia Jenerali,Msafiri,amesema mafunzo hayo yamewawezesha kujifunza  mambo mapya  katika maeneo yao ya kazi  kwa ajili ya kuboresha usalama  kwa wagonjwa wanaopata huduma ya matibabu kupitia mionzi .
Pia mafunzo hayo yanaimarisha utendajimigodini na viwandani ambako mionzi inatumika.
Hivyo akawataka washiriki hao wa mafunzo hayo kuwa mabalozi kwa kusimamia usalama wa vyanzo vya mionzi vilivyopo nchini ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza kutoka kwenye mionzi na hivyo kuathiri wananchi na mazingira.
Awali mkurugenzi wa usimamizi wa mionzi ,Dakta Wilbroad Mhongora, amesema kuwa  mafunzo hayo yametolewa kwa wafanyakazi wa Hospital wanaotumia mionzi, wachimbaji wa migodi ya madini na viwandani  ili kuwawezesha kuimarisha usalama sehhemu zao za kazi.
Amesema mkazo uliopo sasa ni kuwahimiza kusimamia mpango wa kinga  dhidi ya mionzi sehemu za kazi ili mionzi hiyo isije ikawaathiri wao wenyewe na watu wengine pamoja na mazingira.
Dakta Mhongora,amesema mkakati uliopo sasa ni kuendelea kufanya ukaguzi kwenye maeneo yote yanayotumia mionzi ikiwemo hospitalini, migodini na viwandani ili kuhakikisha yanakuwa ni salama.
Amesema tume ya mionzi inajipanga kuangalia uwezekano wa kuwasilisha hoja serikali ili kuwezesha taasisi zote zinazotumia mionzi kuhakikisha zinashiriki mafunzo hayo vinginevyo kama vituo hivyo havitashiriki vinyimwe leseni .
Dakta Mhongora, amesema pamoja na kuwepo upungufu wa watumishi, Tume ya nguza za Atomiki inaendelea  na  hatua kufanya ukaguzi kqwenye vituo vyote vinavyotumia mionzi nchini ili kuzuia madhara.
Ameongeza kuwa tume ipo katika hatua ya kufungua ofisi katika maeneo mbalimbali ya nchi  ili kuzibiti bidhaa na vitu vingine vinavyoingia nchini kupitia mipakani vinavyotum,ia mionzi ili kudhibiti visilete madhara.
Tayari wameshafungua ofisi  katika kandaya mashariki jijini Dar es Salaam ,Zanzibar na sasa wapo mbioni kufungua ofisi mikoa ya Ruvuma kwa ajili ya kanda ya kusini.
Kwa upande wao washiriki hao wameelezea kuridhishwa na kufurahishwa na mafunzo hayo na kusema kuwa yamewajengea uwezo na mbinu mpya za kusimamia mionzi.
Wamesema kuwa huu ni wakati wa teknolojia hivyo mafunzo hayo yamekuwa ni muhimu na yamewapanua wigo hivyo watafanya kazi kwa ufanisi zaidi kwa kuhakikisha wanaimarisha usimamizi wa mionzi ili isilete madhara kwa jamii.

No comments :

Post a Comment