Na. Lilian Lundo-MAELEZO,Dar es Salaam
Serikali kupitia Wizara ya Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na Tume ya Taifa ya UNESCO
wamekusudia kuandaa matamasha na matembezi mbalimbali ili kutoa elimu
kwa jamii kuhusu udhibiti wa matumizi ya dawa na mbinu za kuongeza nguvu
michezoni.
Hayo yamebainishwa leo Jijini Dar es
Salaam na Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume hiyo, Dkt. Moshi Kimizi namna
ambavyo Serikali imekusudia kuanzisha kampeni hizo ili kuionyesha jamii
athari mbalimbali za kisaikolojia na kiafya kwa wachezaji na hasa
vijana.
Aliongeza kuwa mwezi Juni mwaka huu, Bunge
la Tanzania liliridhia mkataba wa kimataifa wa udhibiti wa matumizi ya
dawa na mbinu za kuongeza nguvu katika michezo, hatua iliyolenga kulinda
na kuimarisha afya za wanamichezo nchini.
“Kwa kuridhia mkataba huu na kuutekeleza
itainufaisha nchi kuweza kuhudhuria mafunzo, mikutano na vikao vya
kimataifa na kushiriki katika makongamano yenye maamuzi mbalimbali
yanayohusu suala hili” alisema Dkt. Kimizi.
Kwa mujibu wa Kimizi alisema kupitia
mkataba huo, wanamichezo, walimu wa michezo na wadau wa michezo wataweza
kuelimishwa kuhusu athali za matumizi ya dawa au mbinu za kuongeza
nguvu michezoni pamoja na aina ya vyakula au vinywaji ambavyo vina asili
ya kuongeza nguvu mwilini.
Kwa upande wake Afisa Michezo, Wizara ya
Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Rashidi Mijuza alisema kuwa,
wanamichezo wengi hujikuta wakiwekewa dawa za kuongeza nguvu na walimu
wao katika chakula au vinywaji bila kujua ili tu waweze kushinda.
Kwa mujibu wa Mijuza alisema Serikali
imekusudia kutoa elimu kwa wanamichezo na walimu ili kuondokana na
visingizio vya kutojua au udanganyifu ambao umekuwa ukifanyika kwa
wanamichezo pindi wanapokuwa katika mashindano mbalimbali.
“Kwa Tanzania kuridhia mkataba huo, nchi
itanufaika na mambo mbalimbali katika sekta ya michezo ikiwa ni pamoja
na Tanzania kushiriki na kuandaa mashindano mbalimbali ya kimataifa,
kupata misaada ya wataalamu, fedha na mafunzo kwa ajili ya utekelezaji
wa makubaliano” alisema Mijuza
No comments :
Post a Comment