Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akizungumza na wakazi wa kijiji cha
Kisorya Wilayani Bunda, mkoani Mara wakati alipotembelea na kukagua
kivuko cha MV Ujenzi kinachotoa huduma kati ya Rugenzi Ukerewe na
Kisorya wilayani hapo.
Mbunge wa Mwibara Mhe. Kange
Rugora (wa pili kushoto), akiongea na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (wa pili kulia), katika ziara yake
mkoani Mara wakati alipotembelea na kukagua kivuko cha MV Ujenzi
kinachotoa huduma kati ya Rugenzi Ukerewe na Kisorya kilichopo Wilaya ya
Bunda.
Meneja wa Wakala wa Ufundi na
Umeme Nchini (TEMESA), Eng. Fredinand Mishamo akitoa maelezo kwa Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa wakati
alipotembelea na kukagua kivuko cha MV Ujenzi kinachotoa huduma kati ya
Rugenzi Ukerewe na Kisorya wilayani hapo.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, akishuka kutoka katika kivuko cha MV
Ujenzi kinachotoa huduma kati ya Rugenzi Ukerewe na Kisorya wilayani
Bunda, wakati alipotembelea na kukagua kivuko hicho.
Muonekano wa kivuko cha MV Ujenzi kinachotoa huduma kati ya Kijiji cha Rugenzi Ukerewe na Kisorya wilayani Bunda.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, akikagua kivuko cha MV Mara
kinachotoa huduma kati ya Kijiji cha Mugara na Kuruge wilayani Bunda,
wakati alipotembelea na kukagua kivuko hicho. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya
Bunda, Mwl. Lydia Bupilipili.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, akisikiliza kero kutoka kwa mmoja wa
wananchi wa Kijiji cha Iramba, Wilaya ya Bunda, mara baada ya kukagua
kivuko cha MV Mara na kuongea na wananchi hao.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, akiangalia athari za miundombinu ya
barabara kwenye Daraja la Burendabufwe lilibomoka kutokana na mvua
zilizonyesha hivi karibuni katika barabara ya Kibara-Iramba wilayani
Bunda.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, akicheza nyimbo za asili za kabila
la wakerewe, wilaya ya Bunda kabla ya kuongea na wakazi wa kijiji cha
Iramba, mkoani Mara.
Mbunge wa jimbo la Mwibara, Mhe.
Kange Lugora (kushoto) akiteta jambo na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (kulia), wakati wa mkutano wa hadhara
uliofanyika katika kijiji cha Mwibara.
………………….
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amewaagiza Wakuu wa Wilaya na
Wakurugenzi wa Halmashauri kote nchini
kuhakikisha wanafuatilia na kusimamia kwa ukaribu utekelezaji
wa miradi mbalimbali inayotekelezwa kwa kutumia Mfuko wa Barabara katika maeneo yao.
Akizungumza Wilayani Bunda, mkoani
Mara baada ya kupokea taarifa ya hali ya miundombinu Wilayani hapo,
Waziri Prof. Mbarawa amesema kuwa hatua hiyo pia itasaidia kudhibiti
upotevu wa fedha za wananchi pamoja na kuongeza kasi ya utekelezaji wa
miradi hiyo.
“Nawaagiza Wakuu wa Wilaya wote na
Watendaji wa Halmashauri kuhakikisha wanasimamia ipasavyo miradi
inayotekelezwa kwa kutumia fedha za Mfuko wa Barabara ambazo ni fedha za
wananchi”, ameagiza Prof. Mbarawa.
Aidha, amemhakikishia Mkuu wa
Wilaya ya Bunda kuwa Serikali itaendea kufanya kila linalowezekana
kuimarisha miundombinu kwa maendeleo ya watanzania.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya
hiyo Mwl.Lydia Bupilipili, amesema kuwa wilaya hiyo imejiwekea
utaratibu wa kufuatilia miradi hiyo lakini pia inawaelimisha watendaji
kata na vijiji kuhusiana na sheria ya barabara.
Katika hatua nyingine, Waziri
Mbarawa ametembelea Kivuko cha Mv Mara na Mv Ujenzi na kuahidi kuboresha
utoaji wa huduma katika vivuko hivyo ikiwemo ujenzi wa jengo la abiria
katika kijiji cha Iramba na Kisorya.
Amewasisitiza kudhibiti mapato yatokanayo na vivuko hivyo ili kuweza kuongeza ufanisi na utendaji wa vivuko hivyo.
Naye, Meneja wa Wakala wa Ufundi
na Umeme (TEMESA), Mkoani Mara amemhakikishia Waziri huyo kufunga mifumo
ya kielektroniki ili kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato.
Aidha, Waziri Prof. Mbarawa
ametembelea barabara ya Busambala – Kisorya (KM 120), na kutoridhishwa
na hatua ya ujenzi wake, hivyo kutoa miezi sita kwa Mkandarasi wa
Kampuni ya ujenzi ya Nyanza Roads Works anayejenga barabara hiyo
kukamilisha ujenzi wake.
Prof. Mbarawa ameanza ziara yake
ya siku mbili mkoani Mara ambapo anatarajia kukagua miradi mbalimbali
inayotekelezwa na Wizara yake.
Imetolewa na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, kitengo cha Mawasiliano Serikalini
No comments :
Post a Comment