Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akitoa maelekezo kwa Mkandarasi wa
Kampuni ya Beijing Construction Engineering Group (BCEG), anayejenga
jengo la abiria katika Kiwanja cha Ndege cha Mwanza, Yuzhang Xiong,
wakati alipokagua maendeleo ya mradi wa ujenzi huo.
Meneja Mipago, Ubunifu na
Tathimini wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (TAA), Eng. Mbila Mdemu
akitoa ufafanuzi kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa
Makame Mbarawa, kuhusu mradi wa jengo la abiria katika Kiwanja cha Ndege
cha Mwanza.
Muonekano wa jengo la abiria
katika Kiwanja cha Ndege cha Mwanza kinachojengwa na Kampuni ya Beijing
Construction Engineering Group (BCEG), ambapo ujenzi wake unatarajiwa
kukamilika mwezi Agosti mwakani.
Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya
Viwanja vya Ndege nchini (TAA), Salum Msangi akieleza mikakati ya
utekelezaji wa upanuzi na uboreshaji wa viwanja vya ndege nchini.
Pembeni yake ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame
Mbarawa.
Meneja wa Wakala wa Barabara
Nchini (TANROADS), mkoa wa Mwanza, Eng. Marwa Rubirya akimuonesha Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa upanuzi wa
sehemu ya barabara ya Mwaloni-Furahisha yenye urefu wa Mita 725, wakati
alipokuwa akikagua ujenzi wa Daraja la Furahisha na upanuzi wa Barabara
ya Makongoro-Uwanja wa Ndege, mkoani Mwanza.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akiongea na wakazi wa Pasiansi wakati
alipokuwa akikagua ujenzi wa Daraja la Furahisha na upanuzi wa Barabara
ya Makongoro-Uwanja wa Ndege, mkoani Mwanza.
Muonekano wa Daraja la Furahisha
mkoani Mwanza, ambalo linatarajiwa kukamilika mwazoni mwa mwezi Januari
mwakani. Ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 80.
……………………
Serikali imeanza ujenzi na upanuzi wa viwanja 11 ikiwa ni hatua ya kuendelea kuboresha na kukuza usafiri wa anga hapa nchini.
Akizungumza mara baada ya kukagua
maendeleo ya ujenzi wa jengo jipya la abiria katika kiwanja cha ndege
cha Mwanza, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame
Mbarawa amesema kuwa kiasi cha zaidi ya shilingi Bilioni 150
zinatarajiwa kutumika kwa ajili ya upanuzi wa viwanja hivyo.
Ameongezeza kuwa miradi
itakayotekelezwa katika viwanja hivyo ni pamoja na ujenzi wa majengo ya
abiria na upanuzi wa barabara za kuruka na kutua ndege.
“Maboresho ya miundombinu ya
viwanja vya ndege yatachochea ongezeko la pato la Taifa, hivyo basi
Serikali imeonesha nia ya dhati katika kuhakikisha usafiri huu utakuwa
ni wa uhakika na nafuu kwa wananchi”, amesema Profesa Mbarawa
Aidha, Waziri Prof. Mbarawa
amevitaja baadhi ya viwanja hivyo kuwa ni kiwanja cha ndege cha
Shinyanga, Tabora, Sumbawanga, Kigoma, Mtwara, Songea na Iringa.
Kuhusu ujenzi wa Jengo la abiria
katika Kiwanja cha Ndege cha Mwanza, Profesa Mbarawa amesema kuwa
Serikali imeshatoa kiasi cha shilingi bilioni 7.6 kwa ajili ya kumlipa
mkandarasi na msimamiz wa mradi huo ambao unatarajiwa kukamilika mwezi
Agosti mwakani.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi
wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (TAA), Salum Msangi amesema
Mamlaka itaendelea na uboreshaji wa miundombinu ya viwanja vya
ndege lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa watanzania wanapata huduma zilizo
bora na kukuza pato la Taifa.
Ameahidi kuendelea kutatua
changamoto ya ndege hai wanaohatarisha uharibufu wa miundombinu za
injini za ndege katika uwanja huo ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha usalama
wa anga na watumiaji wake.
Naye, Mkandarasi wa Kampuni ya
Japan Engineering Construction Group (JECP), anayejenga jengo hilo,
Yuzhang Xiong, amemhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kukamilisha ujenzi
huo kwa wakati kwani kwa sasa jengo limefika katika hatua nzuri.
Katika hatua nyingine, Waziri
Mbarawa ametembelea Daraja la Furahisha na barabara ya makongoro hadi
uwanja wa ndege yenye urefu wa kilomita tano na kusema kuwa kukamilika
kwa miradi hiyo kutasaidia kupunguza foleni kwa watumiaji wa vyombo vya
moto na ajali kwa watembea kwa miguu.
Aidha, amefafanua mradi huo kuwa
umegawanyika katika sehemu tatu ambapo kwa sasa sehemu ya tatu ya mradi
huo iliyoanza inahusisha upanuzi wa barabara ya Mwaloni hadi Furahisha
Mita725 na ujenzi wa barabara ya Pasiansi hadi Uwanja wa Ndege (km 5)
kwa kiwango cha lami unatarajiwa kuanza hivi karibuni.
Prof. Mbarawa amewataka wananchi
kutunza na kulinda miundombinu hiyo ambapo Serikali imekuwa ikitumia
fedha nyingi kugharamia utekelezaji wa miradi hiyo.
Amewaagiza uongozi wa Wakala wa
Barabara nchini (TANROADS), mkoa wa Mwanza kumsimamia mkandarasi wa
kampuni ya Nyanza Roads anayejenga barabara hiyo kujenga kwa kiwango
kilicho bora ili kuweza kushawishi Serikali kuwapatia tenda za miradi
mengine.
Meneja wa TANROADS, mkoa wa
Mwanza, Eng. Marwa Rubirya amesema kuwa hadi sasa utekelezaji wa mradi
wa Daraja la Furahisha umefikia asilimia 80 ambapo ujenzi wa daraja na
ufungaji wa vyuma umekamilika na unatarajiwa kukamilika mwanzoni mwa
mwezi Januari.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
No comments :
Post a Comment