Makamu wa Rais wa Shirika la
Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA), Bi. Noriko Suzuki (kulia),
akisikiliza kwa makini maelezo yaliyokuwa yanatolewa na Waziri wa Fedha
na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) (hayupo Pichani),
alipomtembelea na kufanya mazungumzo naye Ofisini kwake Jijini Dar es
salaam. Katikati ni Mwakilishi Mkuu Mkazi wa JICA nchini Tanzania, Bw.
Toshio Nagase na kulia ni Afisa wa Shirika hilo anayeshughulikia masuala
ya usafiri na usafirishaji Bi. Lilian Masalu.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe.
Dkt. Philip Mpango (Mb) (wa pili kulia), akisisitiza jambo wakati
alipokuwa akizungumzia umuhimu wa Nishati ya umeme katika kuchochea
maendeleo ya viwanda nchini, wakati alipokutana na Makamu wa Rais wa
Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) Bi. Noriko Suzuki,
Makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini dar es salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe.
Dkt. Philip Mpango (Mb) (kulia), akizungumzia namna Serikali ya Tanzania
ilivyojipanga kutekeleza miradi mbalimbali ya kipaumbele ikiwemo ujenzi
wa viwanda mbele ya Makamu wa Rais wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo
la Japan (JICA) Bi. Noriko Suzuki (hayupo pichani), alipomtembelea na
kufanya naye mazungumzo ofisini kwake Jijini Dar es salaam. Kushoto ni
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Sheria Bw. Elias Kalist, na kulia kwake
ni Mchumi Mkuu, Yosephe Tamamu, wote kutoka Wizara ya Fedha na Mipango.
Mchumi Mkuu wa Wizara ya Fedha na
Mipango Bi. Yosephe Tamamu (kushoto), akifafanua jambo katika kikao kati
ya Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) na Makamu
wa Rais wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) Bi. Noriko
Suzuki. Aliyekaa kulia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Sheria wa
Wizara hiyo Bw. Elias Kalist.
Makamu wa Rais wa Shirika la
Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) Bi. Noriko Suzuki, akizungumza
katika kikao na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb)
(hayupo pichani), kuhusu ushirikiano wa kimaendeleo kati ya Tanzania na
Japan, Makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe.
Dkt. Philip Mpango (Mb), akimsindikiza mgeni wake, Makamu wa Rais wa
Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) Bi. Noriko Suzuki,
baada ya kufanya mazungumzo namna pande hizo mbili zitakavyoimarisha
ushirikiano uliodumu muda mrefu katika Nyanja mbalimbali za kiuchumi na
kijamii.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe.
Dkt. Philip Mpango (Mb), (kulia) akifurahia jambo na mgeni wake, Makamu
wa Rais wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) Bi. Noriko
Suzuki, kabla ya kuondoka baada ya kufanya mazungumzo namna pande hizo
mbili zitakavyoimarisha ushirikiano uliodumu muda mrefu katika Nyanja
mbalimbali za kiuchumi na kijamii. Kulia ni Mwakilishi Mkuu mkazi wa
JICA hapa nchini, Toshio Nagase.
(Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano-WFM)
…………………
Benny Mwaipaja, WFM, Dar es salaam
Makamu wa Rais wa Shirika la
Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA), Bi. Noriko Suzuki, amesema kuwa
nchi yake itaendelea kuisaidia Tanzania katika Nyanja mbalimbali za
kiuchumi na kijamii ili iweze kufikia malengo yake ya kuondokana na
umasikini.
Suzuki ametoa ahadi hiyo baada ya
kukutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt.
Philip Mpango, ofisini Kwake Jijini Dar salaam.
Makamu huyo wa Rais wa JICA,
amesema kuwa nchi yake inatumia zaidi ya dola za Marekani Milioni mia
moja kila mwaka kusaidia shughuli mbalimbali za maendeleo hapa nchini
katika sekta za miundombinu ya barabara, maji, nishati, afya na kilimo.
Miongoni mwa miradi mikubwa
inayofadhiliwa na serikali hiyo ya Japan ni barabara ya juu ya mzunguko
inayojengwa katika makutano ya barabara katika eneo la Tazara, Jijini
Dar es salaam.
“Tuko tayari kushirikiana na
Tanzania katika kutekeleza Mpango wake wa Pili wa Taifa wa Maendeleo kwa
kuwekeza fedha katika miradi mbalimbali ya maendeleo mliyoipa
kipaumbele kuiwezesha nchi kufikia malengo yake ya kuwa nchi ya viwanda
ifikapo mwaka 2025” alisisitiza Makamu huyo wa Rais wa JICA.
Ameahidi kuwa Shirika lake pia
linaagalia uwezekano wa kuishirikisha sekta binafsi nchini Japan kujenga
barabara katika eneo la Gerezani ili kupunguza msongamano mkubwa wa
magari hasa yanayotoka Bandari ya Dar es salaam na Katikati ya Jiji la
Dar es salaam.
Kwa upande wake Waziri wa Fedha na
Mipango Dkt. Philip Mpango, ameeleza kuwa uhusiano kati ya Japan na
Tanzania ni wa muda mrefu na kwamba nchi hiyo imekuwa mdau wake mkubwa
wa maendeleo.
Amesema katika mazungumzo kati
yake na Makamu huyo wa Rais wa JICA, wamekubaliana kuongeza kasi ya
utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara
eneo la Bendera tatu na Gerezani ili kupunguza msongamano wa magari
kutoka katikati ya Jiji la Dar es salaam
“Mradi Mwingine ni ujenzi wa
barabara kutoka eneo la Moroco hadi Mwenge, Jijini Dar es salaam, ambayo
Japan waliahidi kuijenga muda mrefu uliopita” Aliongeza Dkt. Mpango
Amesema kuwa wamekubaliana pia
kwamba Shirika hilo lisaidie kufungua ukanda wa Kati kwa kujenga
barabara ya Kigoma-Nyakanazi na Kigoma-Mto Malagarasi, ambazo
hazijapata mfadhili mpaka sasa.
“Halikadhalika nimemwomba
atusaidie kuhamasisha sekta binafsi nchini Japan kuja Tanzania kuwekeza
katika sekta ya viwanda vya kutengeneza dawa na vifaa tiba ili kuokoa
kiasi kikubwa cha fedha ambacho serikali inatumia kuagiza dawa nje ya
nchi na pia itakuwa chanzo cha ajira kwa vijana” alisisitiza Dkt. Mpango
Waziri huyo wa Fedha na Mipango,
Dkt. Philip Mpango, ametaja eneo lingine kuwa ni kuiomba Japan iongeze
fursa ya mafunzo kwa vijana wa kitanzania katika nyanja za tiba na ujuzi
maalumu ambao haufundishwi hapa nchini.
Amesema kuwa ameiomba pia nchi
hiyo ya Japan iendelee kusaidia sekta ya kilimo inayotegemewa na idadi
kubwa ya watanzania kwa kusaidia kuongeza uzalishaji na kusindika mazao
ya wakulima ili kuyaongezea thamani.
Katika majadiliano hayo, Makamu wa
Rais wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan Noriko Suzuki,
aliiomba Serikali ya Tanzania itoe msamaha wa kodi kwa miradi miwili
mikubwa inayotekelezwa na wakandarasi mbalimbali kupitia shirika hilo
ikiwemo ujenzi wa barabara ya Bagamoyo na mradi wa maji mkoani Tabora,
maombi ambayo amesema Serikali itayafanyiakazi.
No comments :
Post a Comment