Tuesday, December 6, 2016

Hongera JPM kwa miaka 55 ya Uhuru wetu


jpm1
Kuelekea Miaka 55 ya Uhuru wa Tanzania Bara, Serikali imepongezwa kwa Mafanikio yaliyofikiwa katika kipindi chote tangu awamu ya kwanza hadi awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli.

Watanzania walio wengi wanakupongeza Mhe. Rais kwa kazi nzuri unayofanya, mengi tumeyashuhudia katika kipindi kifupi cha uongozi wako na tunakuombea Mwenyezi akulinde ili Watanzania wanufaike na yale mema uliyopanga kuwafanyia.
Tumeshudia shirika la ndege Tanzania (ATCL)  likiwa na ndege mpya,mikakati ya ujenzi  wa reli yenye viwango vya Kimataifa  (Standard gauge) na mabadiliko makubwa katika kuwaletea wananchi maendeleo.
Hakika  tuna kila sababu ya kujivunia na kumshukuru Mungu kwa zawadi hii aliyotupatia ambayo ni Rais Dkt. John Pombe Magufuli,hakika umevaa viatu vya Baba wa Taifa Mwalimu  Julius Kambarage Nyerere kwa falsafa yako ya “HAPA KAZI TU” inayoakisi falsafa ya Baba wa Taifa ya “UHURU NA KAZI”.
Kufanya kazi kwa bidii ni kielelezo cha uhuru wetu na msingi wa Kujenga uchumi wa Viwanda utakaosaidia kukuza uchumi kwa kasi zaidi katika kipindi hiki ambapo maendeleo yanahitaji watu kufanya kazi kwa bidii na weledi.
Uhuru wetu umekuwa kielelezo cha Mafanikio tuliyoyapata katika nyanja mbalimbali ikiwemo elimu,afya,maji,miundombinu,ujenzi na nyingine nyingi.
Tarehe 9 desemba kila mwaka ni siku yakutafakari hatua tuliyofikia na kuongeza juhudi kwa kufanya kazi bila kuchoka ili kuijenga Tanzania mpya ambayo tayari misingi imejengwa na Kazi kubwa inafanywa na Rais wetu katika kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa nchi ya asali na maziwa.
Kuimarika kwa huduma za Afya katika Hospitali ya taifa Muhimbili ni kielelezo kuwa tumeweza kuitekeleza ile dhana ya Uhuru ni Kujitegemea na kwa hali hiyo tunamuenzi Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye nyakati zote alisisitiza umuhimu wa kujenga uwezo wa kujitegemea kwa Taifa letu.
 Serikali katika awamu zote tangu awamu ya kwanza hadi sasa zimekuwa zikiweka kipaumbele katika Sekta  zote zinazochangia ustawi wa maisha ya wananchi hali iliyochangia kuongezeka kwa shule za msingi ,Sekondari na Vyuo Vikuu ambapo wakati wa uhuru hakukuwa na chuo Kikuu hata kimoja,  sasa tunavyo vyuo Vikuu  48.
Je hayo si mafanikio makubwa katika Kipindi cha miaka 55?ni wazi kuwa nchi yetu imefakiwa katika sekta ya elimu na sekta nyingine pia ambazo kwa kiasi kikubwa zimechochea ukuaji wa uchumi wa Taifa Letu.
  Elimu bure ni miongoni mwa  dhamira ya Serikali  ya Awamu ya tano  ya kuwaletea wananchi wake maendeleo na kuzidi kuendeleza azma ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ya kupambana na maadui watatu ambao ni ujinga,maradhi na umasikini.
Miundo mbinu ya barabara imeimarishwa ikiwemo barabara za Lami na madaraja ambayo yamerahisisha mawasiliano kati ya Mkoa na Mkoa,Wilaya na Wilaya,Kata na Kata hadi ngazi ya vijiji wananchi wanafurahia matunda ya Uhuru wao na rasilimali za Taifa.
 Sekta ya maji pia imeimarika ukilinganisha na wakati wa uhuru ambapo moja ya miradi mikubwa iliyotekelezwa na Serikali ni mradi wa maji wa ziwa Victoria hadi shinyanga na mwingine ni ule wa upanuzi wa mitambo ya Ruvu juu na Ruvu Chini ambayo imeanza kumaliza tatizo la maji katika Jiji la Dar es salaam.
 Wananchi wote bila kujali itikadi zetu tunalo jukumu la kushiriki kikamilifu katika ulinzi wa rasilimali za Taifa na miundo mbinu iliyopo kwa maslahi ya taifa kwa kuwafichua wale wote wanaokwaamisha au kuhujumu nia njema ya Serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo.
Sherehe za Uhuru huadhimishwa kila mwaka inapofika tarehe 9 mwezi Desemba ambapo mwaka huu Kitaifa zitafanyika Jijini Dar es salaam na Kuongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa mara ya kwanza  tangu achaguliwe mwaka mmpja uliopita.
Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni “Tuunge Mkono Jitihada za Kupinga Rushwa,Ufisadi na Kuimarisha Uchumi wa Viwanda kwa Maendeleo yetu.”
Kauli mbiu hii inasadifu yale ambayo kiongozi wetu mkuu anayasimamia hivyo ni wajibu wetu Watanzania kuunga mkono juhudi hizi zakuwakwamua Watanzania na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wetu.

No comments :

Post a Comment