Tuesday, December 6, 2016

ASKOFU MKUU JIMBO LA ZANZIBAR AWATAKA WAZAZI KUWEKEZA KATIKA ELIMU YA WATOTO


askof
Na Masanja Mabula –Pemba ..
ASKOFU wa Kanisa Katoliki Zanzibar Augostino Shayo amewataka wazazi kuwekeza katika sekta ya elimu kwa kuwasomesha watoto wao katika skuli ambazo zinatoa elimu bora ili waweze kumudu ushindani wa soko la ajira.
Amesema urithi pekee kwa mtoto ni elimu hivyo ni jukumu la kila mzazi kuhakikisha mtoto wake anapata elimu bora ambayo itamwezesha kukabiliana na changamoto za utandawazi zinazojitokeza siku hadi siku.
Askofu  Shayo ameyasema hayo kwenye Ibada ya kumpandisha daraja la ushemasi Fratel Abeil Ignus Ndomba iliyo fanyika katika kanisa kuu Parokia ya Wete  Pemba na kuhudhuriwa na waumini wa kanisa hilo Kisiwani hapa.
Amesema kutokana na kutambua umuhimu wa elimu katika maendeleo ya nchi na wananchi wake ,  kanisa litaendelea kuiimarisha skuli yake iliyoko Tomondo Unguja ili iweze kutoa elimu bora kuanzia ngazi ya msingi hadi sekondari .
Amesema skuli hiyo imekuwa ikitoa wanafunzi bora kwani ina Vifaa vya kutosha , mazingira bora ya kufundishia , walimu bora na wanaoingia kazini kwa wakati .
“Ni lazima kila mzazi kupima ubora wa elimu wanayopewa watoto wao  na kuacha kuridhika na elimu inayotolewa bure kwani inakabiliwa na changamoto mbali mbali ”alisema .
Aidha amezidi kueleza kuwa skuli inayomilikiwa na kanisa hilo ya Tomondo imejipatia umaarufu kwani imezingatia viwango na idadi ya wanafunzi katika darasa moja , tofauti na skuli zinazotoa elimu bure ambazo zinakuwa na msongamano mkubwa  wa wanafunzi katika darasa moja.
Naye mkurugenzi wa wito kanisa katoliki jimbo la Zanzibar padri John  Pita Mfoi aliwataka wazazi kusimamia pamoja na kufuatilia maendeleo ya watoto wao skuli ili kujua mwenendo wao na kusaidia kutatua changamoto  za kielimu zinazowakabili.
Amesema elimu ndiyo njia pekee inayoweza kumkomboa mwananchi kutoka katika wimbi la umaskini wa kipato , hivyo ni jukumu lao kuhakikisha wanajenga utamaduni wa kuwa karibu na walimu , kamati ya skuli na wadau wengine wa elimu .
“Ni vyema wazazi na walezi kujenga utamaduni wa kufuatilia maendeleo ya watoto wao skuli kwani elimu ndiyo ambayo inaweza kumkomboa mwananchi kutoka katika wimbi la umaskini ”alieleza.
Katika nasaha zake , paroko wa Parokia ya Wete , Padri Beatusi Babu amemtaka Shemasi Abeil kufanya kazi kwa uhuru na kuyakemea matendo maovu bila ya woga ili aweze kuitumikia vyema jamii .

No comments :

Post a Comment