Sunday, December 18, 2016

BARABARA YA LOLIONDO-MTO WA MBU KUJENGWA KWA KIWANGO CHA LAMI

 lewa
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akizungumza na Watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro kuhusu utekelezaji wa miradi ya miundombinu alipowatembelea ofisini kwao.
lewa-1
Muonekano wa barabara ya Changarawe ya Loliondo – Mto wa Mbu KM 218 inayotarajiwa kujengwa kwa kiwango cha lami, mkoani Manyara
lewa-2
Mkazi wa Kijiji cha Sale, Bw. Michael Nagwianye mkoani Manyara akitoa maoni kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa mara baada ya kukagua barabara ya Loliondo – Mto wa Mbu KM 218 inayotarajiwa kujengwa kwa kiwango cha lami.
……………….


Serikali imesema ipo katika hatua za mwisho za kuanza ujenzi wa Barabara ya Loliondo- Mto wa Mbu yenye urefu wa KM 218 itakayojegwa kwa kiwango cha lami ili kurahishisha usafiri na usafirishaji wa mizigo kwa wananchi wa  mikoa ya Mara, Manyara, Arusha na Mwanza.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa katika kijiji cha Sale, wilayani Ngorongoro mara baada ya kukagua barabara hiyo ambayo ni kiungo kati ya mikoa hiyo minne na nchi jirani ya Kenya.
“Tumeshatangaza Zabuni kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii, mapema mwakani zitafunguliwa ili kumpata mkandarasi ambae atajenga barabara hii kwa kiwango kilichobora”, amesema Waziri Prof. Mbarawa.
Aidha,Waziri huyo amefafanua kuwa ujenzi wa barabara hiyo utatekelezwa kwa awamu mbalimbali ambapo awamu ya kwanza itahusisha ujenzi wa barabara ya kutoka katika kijiji cha Waso –  Sale  yenye urefu wa KM 49.
Ameongeza kuwa barabara hiyo ikikamilika itaungana na ile ya Makutano-Nata yenye urefu wa KM 50 iliyopo Wilaya ya Butiama, mkoani Mara na itasaidia kupunguza kero ya usafiri na kufungua mikoa hiyo  kibiashara kwa wakazi wa maeneo hayo.
Amewataka wananchi wa maeneo hayo kutoa ushirikiano kwa mkandarasi atakayepata zabuni hiyo ili kumrahisishia kumaliza mradi huo kwa wakati na viwango vinavyokubalika.
Kwa upande wao wakazi wa Kijiji cha Sale wamemuelezea Waziri Changamoto wanazozipata katika barabara hiyo na kuiomba Serikali kuharakisha mradi huo kwani utasaidia kuongeza pato katika Sekta ya Utalii na kurahisisha huduma za kijamii.
“Barabara hii ni ya muhimu sana kwani tumeteseka kwa muda mrefu, huduma za kijamii kama kumsafirisha kutoka nyumbani mpaka kwenye kituo cha afya ilikuwa ikituchukua muda mrefu kutokna na ubovu wa miundombinu”, amesema Bw. Elias Badiani.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

No comments :

Post a Comment