Katibu Mkuu Wizara ya Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati)
akiongea wakati wa ufunguzi wa warsha kuhusu urithi wa Utamaduni
Usioshikika inayoratibiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu,
Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kwa wadau wa utamaduni leo Jijini Dar es
Salaam. Wakwanza kushoto ni Mtaalam wa Utamaduni wa UNESCO Bi. Rehema
Sudi anayefuatia ni Mtaalam wa Mipango kutoka UNESCO Bw. Mathias Luhanya
na wakwanza kulia ni Mkufunzi wa Mafunzo hayo Bibi. Deirdre
Solani.Picha na Lorietha Laurence.
Mtaalam wa Mipango kutoka UNESCO
Bw. Mathias Luhanya (katikati) akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha
kuhusu urithi wa Utamaduni Usioshikika kwa wadau wa utamaduni
iliyoratibiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na
Utamaduni(UNESCO) leo Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Katibu Mkuu Wizara
ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel na
kushoto ni Mtaalam wa Utamaduni wa UNESCO Bi. Rehema Sudi.
Wadau wa Utamaduni wakifuatilia
hotuba ya mgeni rasmi(hayupo katika picha) wakati wa ufunguzi wa warsha
kuhusu urithi wa Utamaduni usioshikika leo Jijini Dar es Salaam.
Wadau wa Utamaduni wakifuatilia
hotuba ya mgeni rasmi(hayupo katika picha) wakati wa ufunguzi wa warsha
kuhusu urithi wa Utamaduni usioshikika leo Jijini Dar es Salaam.
………………………………………………………..
Na: Genofeva Matemu
Serikali imeahidi kuhifadhi
kumbukumbu na takwimu sahihi za urithi wa Utamaduni usioshikika kwa
lengo la kuuendeleza na kuiwezesha jamii kuulinda kwa ajili ya vizazi
vijavyo.
Rai hiyo imetolewa na Katibu Mkuu
Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole
Gabriel alipokua akifungua warsha ya siku kumi iliyoandaliwa na Shirika
la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kuhusu
urithi wa Utamaduni Usioshikika leo Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa warsha hiyo
Prof. Gabriel amewataka washiriki kujifunza vizuri ili baadaye waweze
kusaidia katika kuwekeza, kuibua, kutambua na kutunza urithi wa
utamaduni ushioshikika kwani hiyo ndio njia mojawapo itakayowavutia
watalii wengi kuja nchini kujifunza tamaduni zetu zisizoshikika.
“Utamaduni ni nta inayowaweka
watu pamoja, ni vyema mafunzo haya na utaalamu mtakayoipata izingatie
kuibua fursa na kutambua tamaduni ambazo hazishikiki kwani serikali ina
malengo na matumaini makubwa sana kutoka kwenu” alisema Prof. Gabriel.
Kwa upande wake Mkurugenzi
Msaidizi Utamaduni kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
Bibi. Lily Beleko amesema kuwa Tanzania iliweka saini na kuridhia
mkataba wa kulinda urithi wa utamaduni usioshikika ambao ulipitishwa na
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzanzaia mnamo mwaka 2011.
Anaongeza kuwa baadaye UNESCO
kwa kushirikiana na Wizara inayohusika na mambo ya Utamaduni wamekua
wakishirikiana katika kutoa mafunzo kwa wadau wa utamaduni na watu
binafsi kuhusu namna ya kuhifadhi urithi wa utamaduni usishikika
ambapo mafunzo hayo yanafanyika kwa mara ya nne sasa huku lengo
likiwa ni kutekeleza mkataba huo.
Aidha Bibi. Beleko amesema kuwa
watanzania wengi wamekua wakidhani kuwa utamaduni ushioshikika
unahusiana na mambo ya kichawi hivyo kutotilia maanani umuhimu wake
kitu ambacho si kweli kabisa kwa kuwa maana halisi ya utamaduni
usioshikika unahusisha vitu vinavyohusiana na mazingira, maendeleo ya
watu pamoja na mila na desturi zao yakiwemo maongezi, nyimbo, maigizo,
midundo ndani ya ngoma ambayo yanaambatana na ala.
Naye Mwakilishi kutoka Shirika la
Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Bw. Mathias
Luhanya amesema kuwa dhumuni la warsha ni pamoja na kuwajengea uwezo
wadau wa utamaduni namna ya kuhifadhi urithi wa utamaduni usioshikika
ili baadaye waweze kuorodhesha urithi huo kwani Tanzania ina bahati ya
kuwa na jamii zaidi ya 120 hivyo ni matarajio kuwa urithi wa utamaduni
usioshikika umesheheni ndani ya kila jamii.
No comments :
Post a Comment