Mkurugenzi
Mkuu wa mfuko waTaifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Prof. Godius Kahyarara
Na Christian
Gaya
Katika kutekeleza lengo la
kuendeleza na kukuza uchumi imara na ajira nchini, Shirika la Taifa la Hifadhi
ya Jamii (NSSF) limejizatiti kuwekeza katika sekta ya viwanda kwa lengo la
kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa ajili ya manufaa ya wanachama na
Taifa kwa ujumla.
Kufuatana na mkurugenzi mkuu
wa NSSF Prof. Godius Kahyarara anasema kwamba Shirika hili limejizatiti
kuwekeza katika sekta ya viwanda nchini sambamba na kuinua viwango vya ajira
nchini na kuboresha maisha ya wanachama wa mfuko huu wa NSSF na wananchi kwa
ujumla.
Prof. anasema kuwa NSSF
imeamua kufanya mageuzi makubwa katika swala zima la uwekezaji kwa kulenga
uwekezaji ambao utawagusa moja kwa moja wananchi na kuyabadili maisha yao kuwa
bora, na katika hilo shirika limeamua kuelekeza nguvu zake za uwekezaji katika
viwanda kwa kuviwezesha kujiendesha kwa ufanisi na kuleta tija kwa lengo la
kuinua uchumi wa nchi na wananchi wake
kwa kuongeza ajira na kuongeza wanachama wake.
“Uamuzi huu unaenda sambamba
na kuitikia wito wa Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania mheshimiwa Dkt.
John Pombe Magufuli wa kujenga Tanzania kuwa nchi ya viwanda kama suluhisho la
kuwakwamua watanznia kwa kuongeza ajira”, anasema Prof. Kahyarara.
Anasema imefika wakati sasa
tuanze kuwa na viwanda vya ndani vitakavyoweza kuzalisha bidhaa kwa ajili ya
matumizi ya ndani pamoja na kuuza katika soko la nje ili kuweza kujipatia fedha
za kigeni. Hivyo jukumu la kuanza kukuza uchumi wa viwanda ni la kila mmoja
wetu na lazima tushiriki kikamilifu ili tuweze kubadilisha uchumi wetu uwe bora
zaidi.
Tanzania katika miaka ya
mwanzo baada ya uhuru mwaka 1961, ilipiga hatua kubwa ya ujenzi wa uchumi wa
viwanda chini ya mpango wa maendeleo wa mwaka 1969 hadi 1974, katika hiyo miaka
ya 70 ilijitosheleza kwa kila kitu kuanzia vifaa vya shule kama madaftari,
kalamu, karatasi na vifaa vya ujenzi, nguo na bidhaa nyinginezo.
“Mfano michache ya viwanda
ni kama urafiki, urafiki, Sungura, Kiltex, Ubungo Spinning, Mutex, VOIL, Tabora
Textile, Southern Paper Mills (Mgololo) na vingine vingi vilivyokuwa
vinaendeshwa na watanzania na kuwapa watanzania ajira. Kwa bahati mbaya viwanda
hivyo havipo tena” mkurugenzi mkuu anasema.
NSSF pia imeviwezesha
viwanda mbalimbali kwa kutoa mikopo ili viwanda hivyo viweze kujiendesha,
kuongeza ajira na pato la Taifa ikiwa ni sehemu
ya lengo kuu la uwekezaji wa shirika katika miradi inayowagusa wananchi
walio wengi.
“Hivi karibuni NSSF imetoa
mkopo wa sh. 3.1 bilioni kwa ajili ya kukuza uzalishaji wa viwatilifu katika
kiwanda kilichopo Kibaha kwa lengo la kuongeza uzalishaji. Mkopo huu ulitolewa
kupitia shirika la maendeleo la Taifa NDC ambapo mkopo huo utasimamiwa na Benki
ya Azania ili kuhakikisha unarejeshwa kwa wakati na kwa faida iliyokusudiwa.
Kiwanda hiki kinazalisha dawa za kuangamiza mazalio ya mbu kwa hiyo shirika
limeona ni vyema liwe mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa malaria inatoweka
na afya za wananchi zinakuwa imara kwa kuongeza uzalishaji” Prof. anaeleza.
Anasema Shirika pia limetoa
mkopo wa sh. bilioni 3.67 kwa ajili ya kuwawezesha ukuzaji wa biashara ya
nafaka mchanganyiko kupita bodi yake ya CPB. Haya ni maboresha ya iliyokuwa Shirika
la Usagaji Tanzania (NMC) ambapo jukumu lake kubwa ni kujishughulisha na
biashara ya nafaka na mazao machanganyiko ili kuwapatia wakulima fursa ya
kupata bei ya ushindani na soko la uhakika.
“Haya yote yanatokana na
dhamira ya dhati ya Shirika kutowekeza katika miradi ambayo haina tija na ndio
maana sasa shirika limebadili uelekeo wake ili kupata tija zaidi katika miradi
yake” Mkurugenzi Mkuu anafafanua.
Kuhusu daraja la Nyerere
lililofunguliwa Aprili mwaka huu kahyarara
anasema NSSF imeweka mfumo mzuri wa uthibiti wa ukusanyaji wa mapato
ambapo mapato ya daraja kwa sasa yamefikia wastani wa Sh.milioni 600 kwa mwezi
Anasema pia NSSF pia
imejikita katika ujenzi wa nyumba mia 300 mjini Dodoma kwa lengo la kuziuza
ukizingatia kuwa kuna uhitaji mkubwa za makazi kufuatia maamuzi ya serikali
kuhamia Dodoma.
Pia Shirika lina mpango wa
kujenga hospitali ya kisasa “NSSF Hospital” jijini Dar es Salaam kwa lengo la
kupanua na kuwarahisishia wananchi huduma za afya na kupunguza gharama hasa kwa
matibabu yaliyokuwa yanafanyika nje kwa gharama kubwa ili yapatikana hapa hapa
nchini kwa gharama nafuu.
“NSSF pia imekuwa mstari wa
mbele kuchangia huduma za jamii kama fadhila kwa wanachama na wananchi kwa
ujumla kutokana na mchango wao kwa Mfuko” Prof. Kahyarara anasema.
Hata Waziri Mkuu Majaliwa
Kassim Majaliwa wakati akitoa hutuba yake ya ufunguzi wa mkutano wa 6 wa wadau
wa NSSF, Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC) tarehe 20 Oktoba,
2016 aliipongeza NSSF kwa kuendelea kuunga mkono Serikali ya awamu ya tano
katika mikakati ya kuboresha sekta zote ikiwemo afya na elimu.
“Mathalani NSSF imeshiriki
kikamilifu katika kusaidia Serikali katika sekta ya elimu ambapo ilitoa shilingi milioni mia nne (400,000,000.00) za
kutengeneza madawati na shilingi milioni
hamsini (50,000,000.00) kwa ajili ya ukarabati wa shule ya Lindi iliyoungua
moto, ili kusaidia kuirejesha katika hali ya kawaida. Leo tumesikia
watakabidhiwa tani 45 za saruji sawa na mifuko 900 kwa ajili ya waathirika wa
tetemeko la ardhi mkoani Kagera. Hayo ni baadhi ya mambo mengi mnayoyafanya,
nawapongeza sana na natoa wito kwa Taasisi
nyingine kuendelea kuunga mkono jitihada za serikali.” Waziri Mkuu aliwapongeza
NSSF.
Christian Gaya ni mwanzilishi wa
Kituo cha HakiPensheni Tanzania na mshauri wa masuala ya pensheni. Kwa maelezo
zaidi gayagmc@yahoo.com Au kwa habari
zaidi za kila siku juu ya HakiPensheni unaweza kutembelea tovuti www.hakipensheni.co,tz,
hakipensheni.blogspot.com Simu namba +255 655 13 13 41
No comments :
Post a Comment