Christian Gaya
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi, Meneja Mkuu wa Malipo wa Shirika la
Umeme Tanzania (TANESCO), Francis Mcharage cheti cha kuthamini michango
ya wafanyakazi wa shirika hilo kwa NSSF kila mwenzi wakati alipofungua
Mkutano wa Sita wa Wadau wa NSSF kwenye Kituo cha Kimataifa cha
Mikutano cha Arusha (AICC) Oktoba 20, 2016. Watatu kushoto ni Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama na wapili kushoto ni
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Anthony Mavunde. Kulia ni Mwenyekiti
wa Bodi ya Wadhamini ya NSSF, Profesa Samuel Wangwe.
Hifadhi ya jamii ni chombo
muhimu sana katika kuchochea ukuaji wa uchumi na hivyo basi kusaidia kupunguza
umaskini nchini kwa kutumia michango inayokusanywa na kuwekezwa katika miradi
mbalimbali ya maendeleo na hivyo kuongeza ajira na kuchochea kukua kwa uchumi
wa nchi.
Maneno haya yalitamkwa na
mheshimiwa Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kwenye ufunguzi wa mkutano mkuu wa sita (6) wa wadau wa NSSF, kituo cha kimataifa
cha mikutano cha Arusha, Oktoba 20, 2016.
Kauli Kuu ya mkutano huu wa
mwaka ya wananachama na wadau wa NSSF ilikuwa ni “Hifadhi ya Jamii na Maendeleo ya Viwanda; Mweleko
katika Kukuza Uchumi na Ajira Tanzania”
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa alisema amefurahishwa sana na
kauli mbiu hii kwani inaendana na matarajio na mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya
Tano wa kujenga Tanzania mpya yenye uchumi wa viwanda.
“Nyote mnamfahamu kuwa wakati wa kampeni za uchanguzi
mkuu mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli aliwaahidi watanzania kuwa
serikali yake itahakikisha inajenga taifa lenye uchumi wa kati unaoendeshwa kwa
viwanda na sasa utekelezaji wa ahadi hiyo umeanza kwa kasi kubwa” Waziri Mkuu alisema
Alisema Serikali ya Awamu ya
Tano imejipanga kuona nchi yetu inapata maendeleo ya haraka kwa manufaa ya
Watanzania wote. Aidha, katika kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa 2015
pamoja na Ilani ya Uchaguzi wa Chama Tawala Serikali imelenga kuiwezesha nchi
yetu kuwa ya uchumi wa kati wenye kujengwa na viwanda ili kuchochea mageuzi ya
kiuchumi na maendeleo ya watu na kupunguza umasikini.
“Nimefarijika sana kuona
kwamba NSSF imedhamiria kwenda na mweleko huo kwa kupanua wigo wa uwekezaji
wake na kuelekea katika viwanda jambo ambalo litaongeza, ajira, uzalishaji na
kukuza uchumi wa nchi kwa ujumla. Maamuzi haya yataiwezesha NSSF na mifuko
mingine kupata wanachama wapya na kukusanya michango zaidi na kuiwekeza ili
kuweza kutimiza lengo lake la msingi la hifadhi ya jamii.
Mtakumbuka kuwa
mheshimiwa Rais Magufuli aliwahi kutoa maelekezo hayo mwezi Mei, 2016 alipokuwa
akifungua majengo ya vitega uchumi vya Mfuko wa Pensheni wa (PPF) na Mfuko wa
Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) yaliyopo hapa jijini Arusha. Mheshimiwa Rais
aliagiza mifuko yote ya hifadhi ya jamii kuwekeza katika miradi inayozalisha
ajira nyingi, faida ya haraka na kuchangia kiasi kikubwa katika pato la taifa
hususani viwanda” Waziri Mkuu
alikumbusha.
Alisema mkurugenzi mkuu wa
NSSF Prof. Godius Kahyarara amekumbusha ya kuwa nchi yetu katika miaka ya
mwanzo baada ya uhuru mwaka 1961 ilikuwa na uchumi wa viwanda na kwamba mpaka
hadi kufikia miaka ya 70 nchi yetu ilijitosheleza kwa kila kitu kuanzia vifaa
vya shule kama madaftari, kalamu, karatasi, na vifaa vya ujenzi na
tumekumbushana baadhi ya viwanda vilivyokuwepo kama vile urafiki, Sungura,
Kiltex, Ubungo Spinning, Mutex, VOIL, Tabora Textile, Southern Paper Mills
(Mgololo) na vingine vingi vilivyokuwa vinaendeshwa na watanzania na kuwapa
watanzania ajira. Kwa sababu mbalimbali ikiwemo uwajibikaji mbovu na
ubadhirifu, viwanda hivi havipo tena.
“Jambo hili la kuwa na
viwanda halafu baadaye vifungwe kwa sababu rahisi tu halitakuwa na nafasi tena
kwa Serikali ya Awamu hii ya Tano na natumaini hata awamu zijazo. Serikali
haitasita kuchukua hatua kali dhidi ya watendaji wabadhirifu na wasio kuwa na
uchungu na nchi yao. Utaratibu huu ni endelevu kwa kila sekta bila kujali
wadhifa wa mtu kwani wadhifa huo ulitolewa kwa lengo la kuwahudumia watanzania
hivyo mtu akishindwa kutekeleza wajibu huo ni vema atupishe” Waziri Mkuu
Majaliwa Kassim Majaliwa alisisitiza.
“Nawapongeza NSSF sana kwa
juhudi zenu ambazo zinaunga mkono dhamira ya serikali ya kujenga uchumi imara
kupitia uwekezaji katika viwanda. Jambo muhimu kwenu ni kusimamia kikamilifu
dhamira hii” Waziri Mkuu aliwapongeza kwa dhati.
Alisema kazi ya kujenga
uchumi wa viwanda inaweza kufanywa kwa namna mbili, kwanza ni kwa kuvifufua
vilivyokuwepo na pili ni kwa kuvianzisha viwanda vipya.
“Wenzetu wa NSSF wameanza
kutekeleza yote mawili. Hilo la sukari ambalo linafanywa kwa ushirika wa PPF
lakini pia NSSF wameanza kazi ya uwezeshaji kwa kutoa mikopo kwa viwanda nchini
kwa dhamira hiyo hiyo ya kuijenga Tanzania yenye uchumi wa viwanda. Tumeambiwa
hapa ya kuwa shirika limetoa mkopo wa shilingi bilioni 3.1kwa ajili ya kukuza
uzalishaji wa viwatilifu yaani biolovecides katika kiwanda kilichopo Kibaha kwa
lengo la kuongeza uzalishaji wa biashara ya nafaka mchanganyiko kupia bodi yake
(CPB)” Waziri Mkuu alisema.
Juu ya mwelekeo huu wa
Serikali ya Awamu ya Tano wa kujenga Tanzania mpya yenye uchumi wa viwanda Waziri
Mkuu alimalizia kwa kutamka kama yafuatayo
“Natoa Rai kwa Taasisi
ambazo zimenufaika au zitanufaika na mikopo hii, kutumia kwa malengo
yaliyokusudiwa na pia kurejesha kwa wakati kwa mujibu wa mikataba ili wengine
nao wanufaike. Aidha, natoa wito kwa Taasisi na Makampuni mbalimbali kuiga
mfano wa NSSF na PPF kuunganisha nguvu zao katika kutekeleza agizo la
Mheshimiwa Rais la kuwekeza kwenye ujenzi wa viwanda”.
Christian Gaya ni mwanzilishi wa
Kituo cha HakiPensheni Tanzania na mshauri wa masuala ya pensheni. Kwa maelezo zaidi
gayagmc@yahoo.com Au kwa habari zaidi za
kila siku juu ya HakiPensheni unaweza kutembelea tovuti www.hakipensheni.co,tz au
hakipensheni.blogspot.com Simu namba +255 655 13 13 41
No comments :
Post a Comment