Friday, November 18, 2016

NSSF kuinua uchumi, kuongeza ajira, idadi ya wanachama



HakiPensheni

NSSF YACHANGIA UJENZI WA KITUO CHA POLISI KILUVYA

Mkurugenzi Mkuu wa NSSF Prof. Godius Kahyarara 

Na Christian Gaya
Katika kutekeleza lengo la kuendeleza na kukuza uchumi imara na ajira nchini, Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) limejizatiti kuwekeza katika sekta ya viwanda kwa lengo la kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa ajili ya manufaa ya wanachama na Taifa kwa ujumla.

Kufuatana na mkurugenzi mkuu wa NSSF Prof. Godius Kahyarara anasema kwamba Shirika hili limejizatiti kuwekeza katika sekta ya viwanda nchini sambamba na kuinua viwango vya ajira nchini na kuboresha maisha ya wanachama wa mfuko huu wa NSSF na wananchi kwa ujumla.
Prof. anasema kuwa NSSF imeamua kufanya mageuzi makubwa katika swala zima la uwekezaji kwa kulenga uwekezaji ambao utawagusa moja kwa moja wananchi na kuyabadili maisha yao kuwa bora, na katika hilo shirika limeamua kuelekeza nguvu zake za uwekezaji katika viwanda kwa kuviwezesha kujiendesha kwa ufanisi na kuleta tija kwa lengo la kuinua uchumi wa nchi na wananchi  wake kwa kuongeza ajira na kuongeza wanachama wake.
“Uamuzi huu unaenda sambamba na kuitikia wito wa Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli wa kujenga Tanzania kuwa nchi ya viwanda kama suluhisho la kuwakwamua watanznia kwa kuongeza ajira”, anasema Prof. Kahyarara.
Anasema imefika wakati sasa tuanze kuwa na viwanda vya ndani vitakavyoweza kuzalisha bidhaa kwa ajili ya matumizi ya ndani pamoja na kuuza katika soko la nje ili kuweza kujipatia fedha za kigeni. Hivyo jukumu la kuanza kukuza uchumi wa viwanda ni la kila mmoja wetu na lazima tushiriki kikamilifu ili tuweze kubadilisha uchumi wetu uwe bora zaidi.
Tanzania katika miaka ya mwanzo baada ya uhuru mwaka 1961, ilipiga hatua kubwa ya ujenzi wa uchumi wa viwanda chini ya mpango wa maendeleo wa mwaka 1969 hadi 1974, katika hiyo miaka ya 70 ilijitosheleza kwa kila kitu kuanzia vifaa vya shule kama madaftari, kalamu, karatasi na vifaa vya ujenzi, nguo na bidhaa nyinginezo.
“Mfano michache ya viwanda ni kama urafiki, urafiki, Sungura, Kiltex, Ubungo Spinning, Mutex, VOIL, Tabora Textile, Southern Paper Mills (Mgololo) na vingine vingi vilivyokuwa vinaendeshwa na watanzania na kuwapa watanzania ajira. Kwa bahati mbaya viwanda hivyo havipo tena” mkurugenzi mkuu anasema.
NSSF pia imeviwezesha viwanda mbalimbali kwa kutoa mikopo ili viwanda hivyo viweze kujiendesha, kuongeza ajira na pato la Taifa ikiwa ni sehemu  ya lengo kuu la uwekezaji wa shirika katika miradi inayowagusa wananchi walio wengi.
“Hivi karibuni NSSF imetoa mkopo wa sh. 3.1 bilioni kwa ajili ya kukuza uzalishaji wa viwatilifu katika kiwanda kilichopo Kibaha kwa lengo la kuongeza uzalishaji. Mkopo huu ulitolewa kupitia shirika la maendeleo la Taifa NDC ambapo mkopo huo utasimamiwa na Benki ya Azania ili kuhakikisha unarejeshwa kwa wakati na kwa faida iliyokusudiwa. Kiwanda hiki kinazalisha dawa za kuangamiza mazalio ya mbu kwa hiyo shirika limeona ni vyema liwe mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa malaria inatoweka na afya za wananchi zinakuwa imara kwa kuongeza uzalishaji” Prof. anaeleza.
Anasema Shirika pia limetoa mkopo wa sh. bilioni 3.67 kwa ajili ya kuwawezesha ukuzaji wa biashara ya nafaka mchanganyiko kupita bodi yake ya CPB. Haya ni maboresha ya iliyokuwa Shirika la Usagaji Tanzania (NMC) ambapo jukumu lake kubwa ni kujishughulisha na biashara ya nafaka na mazao machanganyiko ili kuwapatia wakulima fursa ya kupata bei ya ushindani na soko la uhakika.
“Haya yote yanatokana na dhamira ya dhati ya Shirika kutowekeza katika miradi ambayo haina tija na ndio maana sasa shirika limebadili uelekeo wake ili kupata tija zaidi katika miradi yake” Mkurugenzi Mkuu anafafanua.
Kuhusu daraja la Nyerere lililofunguliwa Aprili mwaka huu kahyarara  anasema NSSF imeweka mfumo mzuri wa uthibiti wa ukusanyaji wa mapato ambapo mapato ya daraja kwa sasa yamefikia wastani wa Sh.milioni 600 kwa mwezi
Anasema pia NSSF pia imejikita katika ujenzi wa nyumba mia 300 mjini Dodoma kwa lengo la kuziuza ukizingatia kuwa kuna uhitaji mkubwa za makazi kufuatia maamuzi ya serikali kuhamia Dodoma.
Pia Shirika lina mpango wa kujenga hospitali ya kisasa “NSSF Hospital” jijini Dar es Salaam kwa lengo la kupanua na kuwarahisishia wananchi huduma za afya na kupunguza gharama hasa kwa matibabu yaliyokuwa yanafanyika nje kwa gharama kubwa ili yapatikana hapa hapa nchini kwa gharama nafuu.
“NSSF pia imekuwa mstari wa mbele kuchangia huduma za jamii kama fadhila kwa wanachama na wananchi kwa ujumla kutokana na mchango wao kwa Mfuko” Prof. Kahyarara anasema.
Hata Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa wakati akitoa hutuba yake ya ufunguzi wa mkutano wa 6 wa wadau wa NSSF, Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC) tarehe 20 Oktoba, 2016 aliipongeza NSSF kwa kuendelea kuunga mkono Serikali ya awamu ya tano katika mikakati ya kuboresha sekta zote ikiwemo afya na elimu.
“Mathalani NSSF imeshiriki kikamilifu katika kusaidia Serikali katika sekta ya elimu ambapo ilitoa shilingi milioni mia nne (400,000,000.00) za kutengeneza madawati na shilingi milioni hamsini (50,000,000.00) kwa ajili ya ukarabati wa shule ya Lindi iliyoungua moto, ili kusaidia kuirejesha katika hali ya kawaida. Leo tumesikia watakabidhiwa tani 45 za saruji sawa na mifuko 900 kwa ajili ya waathirika wa tetemeko la ardhi mkoani Kagera. Hayo ni baadhi ya mambo mengi mnayoyafanya, nawapongeza sana na natoa wito kwa Taasisi  nyingine kuendelea kuunga mkono jitihada za serikali.” Waziri Mkuu aliwapongeza NSSF
Christian Gaya ni mwanzilishi wa Kituo cha HakiPensheni Tanzania na mshauri wa masuala ya pensheni. Kwa maelezo zaidi gayagmc@yahoo.com Au kwa habari zaidi za kila siku juu ya HakiPensheni unaweza kutembelea tovuti www.hakipensheni.co,tz, hakipensheni.blogspot.com Simu namba +255 655 13 13 41

No comments :

Post a Comment