Meneja
Mkaazi wa Kampuni ya Jumia Travel Tanzania, Fatema Dharsee (kushoto),
akielezea shughuli mbalimbali zinazofanywa na kampuni hiyo.
Hafla ikiendelea.
Wadau wakiwa kwenye hafla hiyo.
Meneja Mkaazi wa Kampuni ya Jumia Travel Tanzania, Fatema Dharsee (kulia), akimkabidhi tuzo Flora Rwehumbiza katika hafla hiyo.
Meneja Mkaazi wa Kampuni ya Jumia Travel Tanzania, Fatema Dharsee akimkabidhi tuzo ya Ushirikiano
Mkubwa mwaka 2016 kwa Meneja wa Huduma za Hoteli ya Amaan Bungalows,
Daudi Fundi (kushoto). Hafla ya sherehe hizo zilifanyika jana katika
ukumbi wa Mayfair jijini Dar es Salaam.
Meneja
Mkaazi wa Kampuni ya Jumia Travel Tanzania, Fatema Dharsee (kulia)
akikabidhi tuzo ya Mshirika Bora Katika Biashara mwaka 2016 kwa Mtendaji
wa Mauzo wa Hoteli ya Serena ya jijini Dar es Salaam, Emma Sizya.
Meneja Mkaazi wa Kampuni ya Jumia Travel Tanzania, Fatema Dharsee (kushoto), akizungumza na wanahabari.
………………………………………………………
Na Dotto Mwaibale
MTANDAO
unaoongoza kwa huduma za hoteli kwa njia ya mtandao barani Afrika wa
Jumia Travel umetoa tuzo kwa hoteli na washirika wake wakati wa hafla
fupi iliyofanyika siku ya Alhamisi katika ukumbi wa hoteli ya Mayfair
jijini Dar es Salaam.
Akizungumza
wakati wa sherehe za utoaji wa tuzo hizo zilizofanyika Dar es Salaa
jana, Meneja Mkaazi wa Jumia Travel Tanzania Fatema Dharsee alibainisha
kuwa tuzo hizo zimelenga kuleta chachu katika matumizi ya huduma za
hoteli mtandaoni nchini na kupanua wigo wa huduma kwa wateja.
“Leo
hii tumejumuika hapa kuzitambua na kuzitunuku hoteli zinazotoa huduma
nzuri pamoja na kupendwa na wateja wa ndani na nje ya nchi. Mbali na
sababu hizo lakini kikubwa zaidi ni kwa hoteli hizi kuendana na
mabadiliko ya teknolojia kupitia mtandao wa intaneti ambao unawezesha
huduma zao kufikiwa na mtu yeyote duniani,” alisema Dharsee.
“Hoteli
zote zilizojiunga au kujumuishwa kwenye mtandao wetu wa ‘Extranet’
zinazo fursa kubwa za kuongeza ufanisi na thamani ya biashara yao kwani
hazitegemei tena wateja wanaokwenda moja kwa moja kutafuta huduma kwenye
meza zao za maulizo. Kupitia mtandao wetu ambao unapatikana kwenye
kompyuta, tabiti na simu, unamwezesha meneja wa hoteli au mapokezi
mahali popote walipo mbali na vituo vyao vya kazi kupokea maombi ya
wateja kisha kuthibitisha au kubatilisha upatikanaji wa huduma husika,”
aliongezea Dharsee
Aliendelea mbele kwa kufafanua zaidi kuwa vipengele vya tuzo za Jumia Travel Tanzania vilivyokuwa vikiwaniwa ni pamoja na:
Chaguo
la Wasafiri – hii ilitolewa kutokana na maoni ya wateja au wageni wengi
walioitembelea; Hoteli Iliyoonesha Ushirikiano Mkubwa – hii ilitolewa
kwa kigezo cha kuthamini mchango na ushirikiano wake; Hoteli Bora
Inayochipukia – hii ilitolewa kutokana na juhudi na jitihada
zilizooneshwa katika sekta nzima kwa ujumla; Hoteli Iliyopokea Maombi
Zaidi Kutoka Kwa Wateja – hii ilitolewa kwa mujibu wa kuwa na maombi
mengi kutoka kwa wateja; na Mshirika Bora Katika Biashara – hii
ilitolewa kwa kutuunga mkono na mchango mkubwa katika biashara.
“Ningependa
kutoa shukrani za dhati kwa hoteli zote zilizokubali wito na kuhudhuria
hafla hii. Uwepo wenu hapa jioni ya leo unaonyesha kutuamini na kuunga
mkono jitihada za kuinua sekta ya utalii na ukarimu nchini hususani
kuhamasisha kuendana na mabadiliko ya teknolojia duniani,” alihitimisha
Meneja Mkaazi huyo wa Jumia Travel nchini Tanzania.
Katika
hafla hiyo hoteli zilizojinyakulia tuzo hizo ni pamoja na Serena ambayo
ilitunukiwa tuzo ya Mshirika Bora Katika Biashara; Tanzanite Executive
Suites ilitunukiwa tuzo ya Chaguo Bora la Wasafiri; Amaan Bungalows
ilitunukiwa tuzo ya Hoteli Iliyoonesha Ushirikiano Mkubwa; Harbour View
Suites ilitunukiwa tuzo ya Hoteli Iliyopokea Maombi Zaidi Kutoka Kwa
Wateja; na Slipway ambayo yenyewe ilitunukiwa tuzo ya Hoteli Bora
Inayochipukia.
Akizungumza
baada ya kupokea tuzo Mtendaji wa Mauzo kutoka Hoteli ya Serena ya
jijini Dar es Salaam Emma Sizya amesema kuwa amefarijika kupokea tuzo
hiyo na kuipongeza kampuni ya Jumia Travel Tanzania kwa kuja na kitu
hiki cha kipekee.
“Kwanza
ningependa kuipongeza Jumia Travel Tanzania kwa kuja ni hizi tuzo
ambazo ninaamini kuwa zitaleta mchango mkubwa katika kuhamasisha sekta
ya hoteli nchini. Tumekuwa tukiona sekta mbalimbali zikiwa na tuzo zao
lakini yetu ikiwa imelala kidogo, huu ni mwanzo mzuri na ninaamini
waandaaji hawataishia hapa,” alisema na kumalizia Sizya kwamba, “Serena
siku zote tunajivunia kuwa mbele katika kuunga mkono jitihada za wadau
mbalimbali wanaofanya kazi na sisi. Lengo letu kubwa ni kuona kuwa kwa
pamoja tunashirikiana katika kuwashawishi wateja kuendana na kasi ya
mabadiliko ya teknolojia ambapo sasa hivi kupitia kampuni kama hii
unaweza kupata huduma zetu mtandaoni.”
Hafla
hiyo imeambatana na kuadhimisha miaka mitatu tangu Jumia Travel
kuanzishwa pamoja na kampeni maarufu ya mauzo inayoendelea kwa jina la
‘Black Friday’ ambayo imeanza Novemba 14 mpaka Novemba 25, 2016.
Matarajio ya kampuni kwa wiki hizi mbili za mbili ni makubwa ambapo
imelenga kuwapatia wateja fursa ya kufanya manunuzi ya bidhaa na huduma
za awali kwa ajili ya msimu wa sikukuu kwa gharama nafuu.
No comments :
Post a Comment