Waziri
wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) akizungumza na
Wajumbe wa Bodi ya Shirika la Bima la Taifa (NIC) pamoja na waandishi wa
Habari (hawapo pichani), kabla ya uzinduzi rasmi wa Bodi ya NIC Jijini
Dr es Salaam.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Shirika la Bima la Taifa (NIC), Bw. Sam Kamanga, akielezea
mikakati mipya ya Shirika hilo katika kuboresha utoaji wa huduma za Bima
za aina mbalimbali kwa wateja wao, wakati wa uzinduzi wa Bodi ya
Shirika hilo, tukio lililofanyika katika ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano
wa Mwalimu Julius Nyerere, Jijini Dar es salaam.
Waziri
wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango (kulia), akimkabidhi
Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Bima la Taifa (NIC) Bw. Laston Msongole
(Kushoto), vitendea kazi ikiwemo sheria za masuala ya Bima na miongozo
mingine ya sekta hiyo ikiwa ni ishara ya uzinduzi rasmi wa Bodi ya
Shirika hilo uliofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa
Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Waziri
wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (wa tatu kulia) akiwa
katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Bodi ya Shirika la Bima la Taifa
(NIC) pamoja na viongozi wengine wa Serikali na Maafisa wa Shirika hilo
baada ya kuzinduliwa rasmi kwa Bodi ya Shirika hilo katika Ukumbi wa
Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.
……………
Na Benny Mwaipaja, WFM, Dar es salaam
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt.
Philip Mpango, ameahidi kushirikiana na Taasisi zote zilizo chini ya
Wizara yake kwa kuhakikisha zinajiendesha kwa faida ili Serikali
ifaidike na mapato yatokanayo na biashara za Taasisi na Mashirika yote
kwa lengo la kukuza uchumi wa nchi pamoja na kupunguza umaskini.
Dkt. Mpango aliyasema hayo katika
uzinduzi wa Bodi ya Wajumbe wa Shirika la Bima la Taifa (NIC),
uliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere, jijini Dar es
Salaam.
Katika uzinduzi huo Waziri Mpango
ameishauri NIC kutoa elimu ya kutosha kwa Wananchi walioko vijijini na
mijini ili watambue umuhimu wa Bima mbalimbali zinazotolewa na Shirika
hilo.
Aliongeza kuwa Shirika hilo
linatakiwa kubuni mikakati mizuri ya kuongeza huduma za bima nchini hasa
katika Sekta ya Kilimo, Ufugaji na Uvuvi kwa kuwa sekta hizo zimeajiri
idadi kubwa ya wananchi ililiweze kupata faida na kutoa gawiwo kwa
serikali.
“Naishauri Bodi iwe bunifu na
kuhakikisha kuwa huduma za bima zinaelekezwa kwa wananchi waliowengi
vijijini ambao wanakosa huduma hizo kwa kipindi kirefu ili waweze
kunufaika na huduma hizo badala ya kung’ang’ania mijini kama
zinavyofanya Benki” alisisitiza Dkt. Mpango
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa
Shirika la Bima la Taifa (NIC), Bw. Sam Kamanga, amesema kuwa
Menejimenti itashirikiana bega kwa bega na Bodi iliyozinduliwa ili
kurudisha hadhi ya Shirika hilo, lakini pia itafanya kazi kwa uaminifu
na umakini mkubwa ili kuongeza idadi ya wateja ambao watachangia mapato
ya Serikali.
Amesema kuwa Shirika hilo
limejiekeza kupanua wigo wa utoaji wa huduma zake kwa kuanzisha Bima
kwaajili ya wakulima, wafugaji na wavuvi kwa kuwa eneo hilo halijaweza
kufikiwa na huduma hizo.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Bodi
ya Shirika hilo, Bw. Laston Msongole, amesema kuwa Bodi hiyo
itahakikisha kuwa shirika hilo linakuwa la kisasa na lenye tija kwa
taifa.
Amesema katika kipindi kifupi cha
kulifufua shirika hilo limeweza kupata faida ya zaidi ya shilingi
Bilioni 6.8 hatua iliyoliwezesha kuwalipa wateja wao madai yao ya bima.
“Katika Kipindi cha mwaka mmoja wa
Serikali ya awamu ya Tano, NIC imewalipa wateja wake madai yao
yanayofikia kiasi cha shilingi Bilioni 1.26 sawa na asilimia 9.8 ya
makusanyo yote ya biashara ya Bima katika kipindi cha Oktoba 2015/2016.
Ameiomba serikali iridhie maombi
ya Shirika hilo ya kuiruhusdu iuze baadhi ya rasilimali zake yakiwemo
majengo na viwanja ili lipate mtaji wa kutosha na kuliwezesha kulipa
madai ya wateja wao ambao wameanza kulitumia tena shirika hilo kwa kasi
baada ya kuboreshwa.
Shirika la Bima la Taifa (NIC)
linashughulika na biashara ya Bima za Maisha na zisizo za maisha,
ikiwemo kuuza bima za mali na ajali ambazo ni Bima za moto, magari,
meli, ndege, wizi na ujenzi hali kadhalika kushughulikia biashara ya
soko la pamoja la mashariki na kusini mwa Afrika (COMESA) na taasisi
nyingine za kikanda.
No comments :
Post a Comment