Na Ismail Ngayonga-Dar es Salaam.
BUNGE la 11 la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kesho (leo) linatarajia kuanza mkutano wake wa
tano, ambapo macho na masikio ya wadau na wananchi mbalimbali
yataelekezwa katika mjadala wa miswada mbalimbali ikiwemo ule wa huduma
za habari wa mwaka 2016.
Tangu muswada huo uliposomwa kwa
mara ya kwanza Bungeni tarehe 16 Septemba mwaka huu, wadau mbalimbali wa
habari na wasomi, vyama vya kitaaluma ya habari wamekuwa na mitazamo na
misimamo tofuati kuhusu muswada huo.
Miongoni mwa hoja zilizotawala
katika mijadala ya wadau ni pamoja na kuongezwa muda wa kujadili muswada
huo kwa kina zaidi ili kutoa fursa kwa wadau kuelewa kwa usahihi
vipengele vilivyopo katika muswada huo.
Itakumbukwa mwaka 2006, Serikali
iliwasilisha kwa wadau miswada miwili ya Haki ya Kupata Habari na
Huduma za Habari ili kuwawezesha kupitia kwa kina vipengele hivyo ili
kuboresha uendeshaji na usimamizi wa vyombo vya habari nchini.
Maoni na mapendekezo ya wadau wa
habari juu ya muswada wa haki ya kupata habari wa mwaka 2006
yalikamilika na kuwasilishwa Serikalini mwaka 2007 na mapendekezo ya
muswada wa huduma za habari uliwasilishwa mwaka 2008.
Kwa kuzingatia uhitaji wa muda
mrefu wa sheria hizo, mwezi septemba mwaka huu Serikali iliwasilisha
Bungeni muswada wa sheria ya haki ya kupata taarifa, ambayo ilisomwa,
kujadiliwa na kupitishwa na Bunge.
Pamoja na dhamira ya dhati ya
Serikali ya kuharakisha mchakato wa kutungwa kwa sheria hizo,
inasikitisha kuona wadau wa habari wakiwemo baadhi ya wamiliki,
wahariri, vyombo vya habari na waandishi wa habari wakibishana katika
majukwaa na mitandao ya kijamii.
Inashangaza kuona miongoni mwa
wadau wanaobishana kuhusu muswada huo ni miongoni mwa taasisi za
kisheria ambazo ziliusoma muswada huo, kuujadili na kuwasilisha maoni
yao mbele ya Kamati ya Bunge kabla muswada huo kusomwa kwa mara ya
kwanza Bungeni mwezi septemba mwaka huu.
Muswada umeweka wazi wajibu, haki
na maslahi ya wamiliki, wahariri, vyombo vya habari na waandishi wa
habari ambayo kwa kipindi kirefu yameshindwa kutambuliwa kutokana na
kukosekana kwa mfumo wa kisheria.
Sura ya nne ya muswada imeainisha
uanzishaji wa Baraza huru la Habari, ambalo wadau wa habari wamekuwa
wakilihitaji kwa ajili ya kuanzisha chombo huru cha wanahabari
kinachosimamia haki, wajibu usalama na maslahi ya waandishi wa habari.
Kipengele hicho cha muswada
kimekusudia kuongeza na kuimarisha wajibu wa vyombo vya habari katika
jamii, na kuifanya tasnia ya habari kuaminika na kudhaminiwa na jamii.
Katika katika nchi zinazoendelea
ikiwemo Tanzania, vyombo vya habari vimekuwa chachu ya ujenzi wa maadili
ya jamii, nguzo ya amani, mshikamano na utulivu, sambamba na kitovu cha
mabadiliko ya kifikra na mawazo ndani ya jamii.
Ili kutekeleza wajibu huo wa
msingi ni vyema vyombo vya habari wajibu kuzingatia miiko, maadili na
usalama wa nchi kama ilivyobainishwa katika sheria mbalimbali za nchi
ikiwemo sheria ya magazeti ya mwaka 1976.
Ibara ya 18 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeanisha haki na uhuru mawazo: “Bila
ya kuathiri sheria za nchi, kila mtu yuko huru kuwa na maoni yoyote na
kutoa nje mawazo yake, na kutafuta, kupokea na kutoa habari na dhana
zozote kupitia chombo chochote bila ya kujali mipaka ya nchi”.
Waandishi wa habari wanakumbushwa
pia kusoma Ibara ya 31 ya Katiba inayosisitiza kuhusu madaraka ya
pekee ya mamlaka ya nchi kuhusu ukiukaji wa haki na uhuru.
Tanzania kama zilivyo nchi
nyingine duniani zina zimeanisha taratibu za ukomo wa kuzuia utangazaji
na uchapishaji wa habari zinazohatarisha usalama wa taifa ikiwemo vita,
uasi, mapigano na kadhalika.
Sheria na mikataba ya mbalimbali
za kimataifa ikiwemo ibara ya 19 ya mkataba wa kimataifa wa haki za
kiraia na kisiasa, umeainisha ukomo wa vyombo vya habari katika masuala
ya usalama wa taifa, kashfa na maadili ya taifa.
Wakati tukielekea katika utungaji
wa sheria hiyo, ni wajibu wa wadau wa habari kuwa katika mlengo mmoja,
kwa kuwa sheria kiasi kikubwa imekusudia kumkomboa mwandishi wa habari
wa Tanzania kuondokana na maslahi duni yaliyopo katika vyombo mbalimbali
vya habari.
Aidha kutungwa kwa sheria hizo
mbili haki ya kupata habari na sheria ya huduma ya habari ni moja ya
dhamira za mipango ya kuendesha shughuli za Serikali kwa uwazi, ikiwa ni
utekelezaji wa ahadi iliyotolewa Rais mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho
Kikwete Jijini London Uingereza wakati wa mkutano wa OGP mwaka 2013 na
2014.
No comments :
Post a Comment