Sunday, September 4, 2016

BENKI YA DIAMOND TRUST YASAIDIA WATOTO


Meneja wa kitengo cha Masoko wa Benki ya Diamond Trust (DTB), Sylvester Bahati (kulia), akikabidhi magodoro 50 kwa Mkuu wa kituo cha watoto wenye mahitaji aalumu kilichopo Chamazi, Bi. Winfrida Rubanza.  Pichani chini ni Bi. Winfrida Rubanza akihojiwa na mwandishi wa habari. Tukio hili liliratibiwa na Benki ya Diamond Trust ikishirikiana na Bi Lorna Dadi ambaye ni mwandishi wa kitabu cha Vipande Vya Maisha.


NA IMMACULATE MAKILIKA MAELEZO
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe  amesema kuwa serikali imeimarisha sekta ya Mahakama nchini ambapo imeanzisha kamati ya maadili ya mahakama katika kila wilaya nchi nzima ili kusimamia upotofu wa maadili katika mahakama hizo.
Dkt. Mwakyembe  amesema  hayo  leo wakati wa kipindi cha TUNATEKELEZA kinachoandaliwa na Idara ya Habari-MAELEZO kwa kushirikiana na  TBC 1 ambapo alisema Serikali imeamua kuanzisha kamati hizo ili zipokee upotofu wa maadili  unaofanywa na baadhi ya watumishi wa mahakama ambao sio waaminifu hali ambayo inaharibu sifa ya chombo hicho cha kutoa haki.
“Tumeanzisha kamati hizi katika kila wilaya ili zipokea  upotofu wa maadili kwa upande wa mahakama, sasa wananchi wanaweza kwenda kutoa malalamiko yao kwenye kamati hizo ili yaweze kufanyiwa kazi na hatua  zitachukuliwa kwa wale watakaokutwa na makosa”.
“Kamati hizo zinazoongozwa na wakuu wa wilaya zinaundwa na wajumbe mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini ili kuwapa wananchi fursa nzuri  ya kuweza kutoa malalamiko yao”. Alisema Dkt. Mwakyembe.
Aidha, Dkt. Mwakyembe alisema kuwa kwa sasa Serikali imeendelea kuwa na mikakati kadhaa ya kuimarisha sekta ya Mahakama nchini, ambapo inaendelea kukamilisha maandalizi ya mfumo wa divisheni ya mahakama ya rushwa na ufisadi ili itakapoanza  iweze kufanyakazi bila matatizo.
“Tunaendelea kujiandaa na idara zote zinazohusika  katika  mahakama hiyo, ili ziweze kufanya kazi vizuri, tumeweka vigezo vya kesi zitakazosikilizwa huko na hakutakua na kesi za mwaka juzi au muda mrefu kwa kuwa zitasikilizwa kwa wakati”.  Alisisitiza Dkt. Mwakyembe.
Akizungumzia wananchi wanaoshindwa kumudu gharama za huduma za kisheria  zinazotozwa na mawakili au wanasheria mbalimbali, Dkt. Mwakyembe alisema kuwa Serikali imeandaa mswaada ambao utapelekwa Bungeni ili kutunga Sheria  itakayosaidia kutatua changamoto hiyo.
Dkt. Mwakyembe  aliongeza kuwa  serikali imeendelea kushirikiana na vikundi vya harakati na asasi za kirai zaidi ya 290 vyenye wataalamu wa sheria 2500 nchi nzima ili kupanua wigo wa masuala ya sheria, pamoja na kuandaa mfumo wenye tija kwa taifa utakaosaidia kuwafikia na kuwasaidia wananchi wengi  hasa waliopo maeneo ya vijijini ili kupata msaada wa kisheria kuhusu masuala mbalimbali hasa mirathi ya ndoa na ardhi.
Serikali ya Awamu ya Tano imeendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Mahakama kwa wingi kwa ngazi mbalimbali pamoja na kuwaandaa vijana wengi kutoka vyuo vikuu kila mwaka ambao watafanyakazi katika mahakama mbalimbali nchini.




Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka (kushoto) akionesha aina tofauti za maboksi yatakayotumika kufungashia chaki nyeupe na za rangi ambazo zinatarajiwa kuanza kuzalishwa na Vijana wa Wilaya ya Maswa, Mkoani humo wakati alipohitimisha Mafunzo ya Teknolojia ya Utengenezaji wa Chaki kwa vijana hao, (katikati) Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Mhe. Seif Shekalaghe (kulia) Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Maswa, Mhe. Peter Bunyongoli.
Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Mhe. Seif Shekalaghe akizungumza na vijana na wadau wengine wakati wa kuhitimisha mafunzo Teknolojia ya utengenezaji chaki yaliyotolewa na Shirika la Viwanda Vidogo vidogo SIDO kwa Vijana wajasiriamali wa Wilaya ya Maswa, katika ukumbi mdogo wa Halmashauri ya Wilaya hiyo.
Meneja wa Shirika la Viwanda Vidogo vidogo (SIDO) Mkoa wa Shinyanga, Athanas Moshi (aliyesimama) akizungumza na vijana na wadau wengine wakati wa kuhitimisha mafunzo ya Teknolojia ya utengenezaji chaki yaliyotolewa na Shirika hilo  kwa Vijana wajasiriamali wa Wilaya ya Maswa.
Baadhi ya Vijana wajasiriamali wa Wilaya ya Maswa wakiangalia sampuli za maboksi yaliyopendekezwa kutumika kufungashia chaki pindi uzalishaji utakapoanza wakati Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka (hayupo pichani) akihitimisha mafunzo ya Teknolojia ya utengenezaji chaki yaliyotolewa na SIDO kwa vijana hao, wilayani humo
Vijana wajasiriamali wa Wilaya ya Maswa wakiweka chaki walizotengeneza wakati wa mafunzo ya Teknolojia ya utengenezaji chaki yaliyotolewa na SIDO katika maboksi mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu (hayupo pichani) kabla ya Mkuu huyo wa mkoa  kuhitimisha mafunzo hayo.   
 
                                   Na Stella Kalinga, Simiyu
Serikali Mkoani Simiyu imetangaza azma yake ya  kuanza kutengeneza Chaki ambazo zitauzwa katika Wilaya za Mkoa huo na nchi nzima kabla ya Oktoba 14 mwaka huu.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Anthony John Mtaka wakati alipohitimisha mafunzo ya Teknolojia ya utengenezaji wa Chaki kwa vikundi vya vijana Wajasiriamali wilayani Maswa, yaliyotolewa na Shirika la Viwanda Vidogo vidogo (SIDO) Mkoa wa Shinyanga.

Mtaka amesema shule zote za Msingi na Sekondari za Serikali Mkoani humo  zinatumia jumla ya katoni 1200 za chaki ambazo zinagharimu shilingi 25,000,000 kwa kila mwezi, hivyo kama Vijana wa Wilaya ya Maswa wakizalisha Chaki na kusambaza katika mkoa mzima watajipatia kipato na kuondokana na umaskini.

Mkuu huyo wa Mkoa amesema katika kutekeleza azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuwa na  Tanzania ya Viwanda, Mkoa huo umejipanga kuimarisha uwekezaji katika viwanda vidogo vidogo ambavyo vitazalisha mahitaji ya kila siku ya wananchi, hivyo wamedhamiria kuwa na uzalishaji wa bidhaa moja kwa kila wilaya ( one district  one product), ambapo Wilaya ya Maswa itakuwa ikizalisha chaki.

“ Wilaya ya Maswa imepokea shilingi 38,000,000  Meatu 31,000,000 kwa ajili ya vijana kutoka Wizara yenye dhamana na Vijana, sasa hivi  tumepeleka maombi ya wilaya zilizobaki. Tumedhamiria kuutambulisha Mkoa kwa kuzalisha bidhaa zetu wenyewe, tumeanza na Chaki wilaya ya Maswa, Wilaya ya Meatu wao watazalisha maziwa,  tutaendelea kutengeza utambulisho(brand) wa wilaya nyingine kwa kuzalisha bidhaa zinazoendana na malighafi zilizopo” alisema Mtaka.

Akizungumza katika hitimisho la Mafunzo hayo kwa Vijana, Meneja wa Shirika la Viwanda vidogo (SIDO) Mkoa wa Shinyanga, Athanas Moshi ametoa wito kwa vikundi vya vijana kuwa na mipango itakayowasaidia kutangaza bidhaa zao na kupata soko la bidhaa hizo ndani na nje ya Mkoa ili kujiongezea kipato.

“Mtakapoanza kuzalisha chaki, kulingana na tathmini iliyofanyika kama mtauza kwa Mkoa wa Simiyu tu mtakuwa na uwezo wa kutengeneza faida ya shilingi 8,000,000 kila mwezi, hiyo si fedha ndogo mkiwa na mipango thabiti mkazalisha chaki bora mtaweza kuuza chaki zenu nchi nzima na hata nje ya nchi” alisema Moshi. 

Naye mmoja wa vijana waliopata mafunzo ya utengenezaji wa chaki, Kelvin Steven ametoa wito kwa Wananchi wa  Simiyu na Watanzania kwa ujumla,  kuunga mkono juhudi za Vijana Wajasiriamali na kuthamini bidhaa zinazozalishwa hapa nchini ili kuinua uchumi wa Vijana hao na Taifa kwa jumla.

Aidha, Bi. Specioza Fundikira ambaye pia amepata mafunzo hayo amesema matarajio ya Vijana waliopata mafunzo ni kuwa uzalishaji wa chaki utakapoanza kutakuwa na soko la uhakika kwa Shule zote za Msingi na Sekondari za Serikali mkoani humo na mikoa ya jirani, vijana watapata ajira na kuachana na shughuli zisizo halali kama wizi na ulevi.

Kwa Mujibu wa Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Mhe. Seif Shekalaghe vijana kutoka vikundi 8 vya Wajasiriamali ambao wameunda kikundi kimoja cha ‘Maswa Youth Enteprises’ wamepatiwa mafunzo ya Teknolojia ya utengenezaji wa chaki na Shirika la Viwanda Vidogo vidogo (SIDO) Mkoa wa Shinyanga kuanzia tarehe 29/08/2016 hadi tarehe 03/09/2016.

No comments :

Post a Comment