Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba NHC Bw. Nehemia Mchechu akizungumza
na waandishi wa habari katika makao makuu ya shirika hilo Upanga jijini
Dar es salaam kuhusu wadaiwa sugu wa pango katika shirika hilo moja ya
wadaiwa waliotajwa ni Jengo la Club Billicanas ambali linadaiwa Bilioni
moja, Kulia ni Meneja Mauzo wa NHC Bw. Itandula Gambalagi na katikati ni
Muungano Saguya Meneja katika ofisi ya Mkurugenzi.
Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba NHC Bw. Nehemia Mchechu akisisitiza
jambo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya
shirika hilo Upanga kushoto ni Hamad Abdalla Mkurugenzi wa Miliki NHC
na katikati ni Suzan Omari Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano NHC .
..............................................................................................
Serikali imeamua kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala
inayoelekeza Serikali kuhamishia shughuli zake Mji Mkuu wa nchi yetu
Mjini Dodoma. Shirika la Nyumba la Taifa linaunga mkono uamuzi huu wa
kizalendo wa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mheshimiwa Rais Dkt.
John Pombe Joseph Magufuli wenye lengo la kuharakisha maendeleo ya nchi
yetu. Sisi katika Shirika la Nyumba tunaunga mkono uamuzi huu kwa sababu
umetupatia fursa zifuatazo:-
- Kuendelea kutekeleza jukumu letu la msingi la ujenzi wa nyumba katika mji wa Dodoma kwa ajili ya watumishi wa Serikali wanaohamia Dodoma
- Kuliongezea Shirika soko la nyumba inazojenga kwa ajili ya kuwauzia wananchi
- Kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi kupitia sekta ya ujenzi wa nyumba
- Kuongeza ajira kutokana na shughuli za ujenzi wa nyumba zitakazofanyika Dodoma
B: NAMNA SHIRIKA LILIVYOJIANDAA KATIKA KUSAIDIA UAMUZI HUU WA SERIKALI:
Shirika la Nyumba la Taifa kama chombo cha Serikali limejiandaa
kuwezesha upatikanaji wa nyumba za watumishi wa Serikali kwa kufanya
yafuatayo:-
- Tumejenga nyumba za makazi 153 eneo la Medeli, Mjini Dodoma kwa ajili ya kuuza. Kwa sasa bado nyumba 97 zinaendelea kuuzwa kwa wananchi. Nyumba hizi kwa sasa zimepangishwa na kipaumbele kitapewa kwa wapangaji waliopo ndani, na wakishindwa basi zitauzwa kwa Watanzania wengine wenye uhitaji wa kumiliki nyumba. Katika mkataba wa upangishaji nyumba hizo, kulikuwa na kipengele kinacholiruhusu Shirika la Nyumba kuuza nyumba kama watahitaji kufanya hivyo.
- Tumejenga nyumba 44 za gharama nafuu katika Wilaya ya Kongwa nje kidogo ya Mji Mkuu wa Dodoma ambazo tunaziuza kwa wananchi.
- Tumenunua ekari 236 ya benki ya ardhi katika eneo la Iyumbu, pembezoni mwa Makao Makuu ya Chuo Kikuu cha Dodoma. Tutatengeza Master Plan ndogo ya “Satelite Center” ndani ya Main master Plan ya Dodoma inayoandaliwa na CDA. Tunatarajia kufanya ujenzi wetu katika eneo hili na pia kuwakaribisha wawekezaji wengine watakaotaka kuwekeza au kuendeleza ujenzi katika eneo hili.
- Tumenunua ekari 7 eneo la Chamwino ambazo tutazitumia kujenga nyumba
- Tumenunua ekari 4 eneo la Bahi, kwa ajili ya ujenzi wa nyumba
- Tumenunua ardhi ekari 4 eneo la Chemba, kwa ajili ya kujenga nyumba
Kupitia akiba ya ardhi tuliyo nayo Shirika linajiandaa kuanza ujenzi
wa nyumba 300 hadi 500 ndani ya miezi 12 kwa ajili ya kusaidia makazi
ya watumishi wa Serikali. Kipaumbele kitakuwa kuuza na baadhi tutaziacha
kwa ajili ya kupangishwa.
C: NAMNA YA KUPATA FEDHA ZA UJENZI HUU
Ili kutekeleza kwa haraka ujenzi wa nyumba za watumishi Mjini Dodoma,
NHC inatarajia kuwa na shilingi bilioni 60 zitakazopatikana kutoka
katika vyanzo mbalimbali vya fedha vifuatavyo:-
- Kuuza nyumba 97 za makazi eneo la Medeli ambazo kwa sasa tunazipangisha ili kupata kiasi cha shilingi bilioni 15 za kujenga nyumba mpya.
- Kuendelea na uuzaji wa baadhi ya maeneo na viwanja vya Shirika vilivyo wazi Jijini Dar es Salaam na maeneo mengine ili kupata kiasi cha shilingi bilioni 30 zitakazotumika kujenga nyumba mpya Mjini Dodoma. Uuzaji wa viwanja hivi ni muendelezo wa kuwezesha ukuaji wa miji haraka kama tulivyoanza na uuzaji wa maeneo yetu katika eneo la uwekezaji la Safari City Arusha.
- Kufuatilia madeni sugu ya kodi ya nyumba kwa wale wote wanaodaiwa, madeni yanayofikia shilingi bilioni 15,052,877,606. Fedha hizi zitatumika kujenga nyumba mpya Mjini Dodoma. Tunawasihi wadaiwa wote ikiwemo taasisi za Serikali kulipa madeni yao ndani ya mwezi mmoja kuanzia tarehe 25 Agosti, 2016 ili kuepuka adha ya kuondolewa katika nyumba wanazopanga. Lakini kwa wale waliopewa notisi za kulipa kodi, tunawataka wahakikishe wanalipa kodi zao ndani ya muda wa notisi walizopewa na kinyume na hapo tutawatoa kwenye nyumba na kuendelea na hatua nyingine za kisheria ikiwemo kukamata mali zao.
D: NAFASI YA SEKTA YA NYUMBA KATIKA JIJI LA DAR ES SALAAM
Uamuzi wa Serikali wa kuhamishia Makao Makuu yake Mjini Dodoma,
unalenga kulifanya Jiji la Dar es Salaam kuwa kitovu kikuu cha shughuli
za kibiashara. Mpango kabambe wa Dar es Salaam mpya unaandaliwa na
Serikali na utakuwa tayari mwezi Oktoba mwaka huu. Kwa vyovyote vile
Mpango huu unalenga kuifanya Dar es Salaam iweze kubeba shughuli nyingi
za kiuchumi na kibiashara. Tunapenda kuwafahamisha wateja wetu kuwa
tumejiandaa kuendelea na ujenzi wa nyumba bora za kuuza na majengo
makubwa kwa ajili ya kupangisha wafanyabiashara Dar Es Salaam, kwa kuwa
jiji hili litaendelea kuwa kitovu cha Biashara.
Aidha, asilimia takribani 70 ya rasilimali za Shirika la Nyumba la
Taifa ziko katika Jiji la Dar es Salaam hivyo kulipa Shirika nafasi
nzuri ya kushirikiana na Serikali katika kulipanga upya Jiji la Dar es
Salaam. Niwatoe hofu wananchi na wateja wetu kuwa wasiogope kununua
nyumba zetu kwa hofu ya kukosa biashara, badala yake watarajie kuliona
jiji la Dar Es salaam litakalokuwa bora zaidi kwa ajili ya shughuli za
kibiashara. Tunatarajia yafuatayo katika jiji letu
- Tunatarajia kuwa Dar es Salaam mpya itakuwa na ufanisi mkubwa kwa kuwa sasa usafiri wa kutoka eneo moja kwenda jingine utakuwa mwepesi kuliko hivi sasa.
- Hali ya Jiji hili inabadilika kupitia mpango kabambe unaokuja na kuwa kitovu kikuu cha biashara.
- Pia hii itakuwa fursa nzuri kwa Uongozi wa Jiji pamoja na wakazi wake, kujipanga vizuri ili kuwa na jiji la kibiashara litakaloshindana na majiji ya kibiashara ya nchi zingine.
Sekta ya Ujenzi itanufaika zaidi katika maamuzi haya na matokeo yake yatainufaisha nchi katika maeneo yafuatayo:-
- Kuongeza ajira kubwa kupitia sekta ya nyumba ambayo inagusa wakandarasi, mafundi ujenzi, wafanyakazi kwenye mabenki, wafanyabiashara wa vifaa vya ujenzi na samani, mama lishe na watoa huduma wengine.
- Ujenzi mkubwa utasaidia kuchochea uwekezaji na ukuaji wa viwanda vinavyohusiana na mambo ya ujenzi kwa kuwa mahitaji na soko lake vitakuwa na uhakika.
- Fursa hii itaongeza wigo wa kodi na mapato mbalimbali ya serikali, kutokana na faida kubwa ya washirika mbalimbali wa sekta ya ujenzi.
- Kuongeza upatikanaji wa nyumba bora nchini. Nchi yetu ina upungufu mkubwa wa nyumba unaofikia takribani nyumba milioni tatu na nusu na mahitaji ya nyumba kwa mwaka yanaongezeka kwa nyumba laki mbili. Hivyo, kila kunapokuwa na fursa ya kuchochea ujenzi wa nyumba, kama ilivyo fursa hii ya serikali kuhamishia shughuli zake za kiutawala Mjini Dodoma, daima inakuwa ni nafasi murua na sahihi kuitumia kupunguza pengo hilo la nyumba ambalo linazidi kuongezeka kila mwaka.
- Ujenzi huu mkubwa utasaidia kukuza uchumi wa nchi yetu. Kwa sasa sekta ya ujenzi inachangia katika ongezeko la kukua kwa uchumi kwa asilimia 24 kwa mwaka. Fursa ya ujenzi mkubwa inayotokana na uamuzi wa serikali wa kuhamia Dodoma kwa vyovyote vile utapaisha mchango wa sekta ya ujenzi na nyumba kwa takriban asilimia 30 kwa mwaka.
Kwa hiyo, tunatarajia kuuona mji wa Dodoma ukibeba shughuli za
kiutawala za Serikali wakati Dar Es Salaam ikibaki kuwa Jiji la
Kibiashara na hivyo kufanya mgawanyo huo kuwa na manufaa na maslahi
mapana kwa Taifa letu.
IMETOLEWA NA:
NEHEMIA KYANDO MCHECHU
No comments :
Post a Comment