Tuesday, July 26, 2016

Umuhimu wa kinga ya afya ya ujauzito kwa wanawake




 Mama akifurahia mtoto baada ya kujifungua salama

Christian Gaya, Majira Jumanne 19 Julai 2016
Mmojawapo wa wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii (mama mjamzito) akipatiwa huduma kwenye hospitali ambazo zimeingia mkataba na mfuko ikiwa kama maandalizi binafsi ya  kujifungua, utayari wake kwa matatizo yanayoweza kutokea katika  ujauzito, kujifungua na baada ya kujifungua.

Kutokana na kanuni na haki za uzazi na utaratibu wa shirika la kazi duniani (ILO) lengo la kubwa la kuwa na fao la uzazi ni kuhakikisha kuwa kazi za wanamke hawaingiliwi na hali hatarishi ya afya ya wanamke pamoja na mtoto wake na kwamba shughuli za kujifungua hazikwamishi shughuli zao za kiuchumi za kila siku pamoja na usalama wa kazi zao iwe ya kujiajiri au kuajiriwa. 

Kwa mara ya kwanza katika karne, nguvu zaidi zimekuwa zikielekezwa  kwenye lengo la millennia ya maendeleo namba 5 yaani MDG 5, ambapo vifo vya wanawake wenye mimba na watoto vimeweza kupungua mpaka kufikia asilimia 35.

Utafiti wa Shirika la Afya Duniani, WHO, unaonesha ya kuwa wajawazito 303,000 kati ya milioni 130 wanaojifungua kila mwaka hufariki dunia kote ulimwenguni, watoto milioni 2.6 wakifariki dunia kabla ya kuzaliwa, na milioni 2.7 wakifariki dunia katika siku 28 baada na kuzaliwa.

Lakini kati ya nchi zenye mapato ya chini kama Tanzania vyenye idadi kubwa ya vifo vya wajawazito na watoto vimekuwa vikitofautiana sana na ni nchi 23 tu ambazo ziko kwenye kundi la kufikisha asilimia 75 katika kupunguza vifo vya wajawazito na watoto mpaka ilipofikia mwaka 2015. 

Elementi kuu za kinga za uzazi ni kama kupata likizo ya uzazi, kupata mafao taslimu ya kuhakikisha kuwa mama anaweza kujikimu yeye pamoja na mtoto wake wakati akiwa wa likizo ya uzazi, kuhakikisha kuwa anapatiwa matibabu kwa ajili ya kinga ya afya ya ujauzito.
Mama mjamzito au anayeyonyesha ana haki kupewa kinga ya kutofukuzwa na kubaguliwa na kupewa kinga ya kwenda kunyonyesha mara tu baada ya kurudi kazini baada ya kurudi likizo yake ya uzazi. 

Kwa hiyo kinga ya uzazi kwa akina mama lazima ichangie afya na ustawi wa wamama pamoja na watoto wao na hivyo kutimiza malengo ya namba 4 na 5 ya maendeleo ya millennia ya Tanzania kama mwanachama wa umoja wa mataifa, yanayotaka kupunguza vifo vya watoto na kuboresha afya za wamama. 

Wanawake wengi wanakosa fursa ya kupatiwa malipo ya uzazi kabla ya kujifungua na hata baada ya kujifungua. Na wanawake wengi zaidi wanatishiwa kufukuzwa kazi na hata kubaguliwa eti kwa sababu ni mjamzito au atakuja apate mimba. 

Kulea watoto bila ya kuwaharibia wanawake fursa zao za haki za kushirikishwa kwenye kazi za maendeleo ya kiuchumi inabaki kuwa ni changa moto kubwa wakati ubora na uwezo nafuu wa mipangilio ya uangalizi wa mtoto haupo kwa mpana mkubwa kabisa. 

Na inasekama karibu asilimia tisini na tisa ya wamama duniani wanaopoteza maisha yao wakati wa kujifungua hutokea
Afrika na Tanzania ikiwa mojawapo.

Ingawa vifo vya watoto wanaozaliwa kwa mwaka 1990 vilipungua kutoka 320 mpaka kufikia 250 kwa kila watoto 100,000 waliozaliwa wakiwa wazima kwa mwaka 2008, lakini angalau wanawake wapatao 343,000 wanaendelea kufa wakati wa ujauzito na wakati wa kujifungua watoto kila mwaka. Kwa kila mwanamke anayekufa angalau kama 20 wanateseka na kusumbuka na maumivu makali au kupatwa na ulemavu.

Ni kweli ya kuwa idadi kubwa ya akina mama hawako katika mpango wa hifadhi ya jamii hivyo wengi wamejiajiri wenyewe. Lakini hata idadi ndogo ya wanawake walioajiriwa na kuwa wanachama wa mifuko hii ya pensheni hawajaweza hata kutumia fursa ya fao la uzazi kabla ya kujifungua na baada ya kujifungua. 

Kwa kweli elimu ya juu ya fao hili la uzazi inahitajika sana, kwa sababu hata kama wanawake wengi wamejiajiri wenyewe lakini wanaruhusiwa kujiunga, kwa mfano na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii NSSF kwa mpango wa hiyari kwa kulipia kadri ya uwezo wao kuanzia shilingi 20,000/= kwa kila mwezi ya mshahara wa kima cha chini wa serikali na kufanya hivyo atakuwa na uwezo wa kupata mafao yote yatolewayo na NSSF. 

Na kwa upande wa fao hili la uzazi mara nyingi wazazi wengi hawapata taarifa ya kuwa anastahili kupata kabla ya kujifungua au baada ya kujifungua na kupita muda wa ziada ambao ni miezi mitabu (3) au ndani ya siku tisini (90). 

Dorca Gikaro aliyekuwa wahi kuwa mwanachama wa mfuko NSSF Dar es Salaam, alipohojiwa na Kituo cha HakiPensheni anasema alipata mafao ya uzazi karibu asilimia 100 ya wastani ya mapato ya siku ambayo ni sawa na mafao ya muda wa wiki 12. 

Anasema tangia aanze na mimba ya mtoto wake kwanza aitwae neema alipata kwa awamu mbili tofauti kwanza alipata mafao ya fedha taslimu wiki 4 kabla ya kujifungua na awamu ya mwisho alipata baada ya wiki 8 baada ya kujifungua. Lakini ikumbukwe ya kuwa mwanachama akitaka anaweza kuamua kulipwa kwa wiki zote 12 baada ya kujifungua.

Dorca mama mwenye watoto watatu kwa sasa anasema kuwa fedha ya awamu ya kwanza ilimsaidia sana kwa ajili ya kujenga afya yake na ya kichanga tumboni. 

Na mafao ya awamu ya pili yaani baada ya kujifungua anasema ilimsaidia sana kujipatia supu na mahitaji mengine ya muhimu kama mama mnyonyeshaji, kwani mtoto wake alipata maziwa ya kutosha na yenye virutubisho vilivyo bora zaidi kwa mtoto wake mchanga na kuimarisha zaidi afya ya mama. 

Anasema kuna wakati fulani mara tu alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa uliokuwa umeambatana na ujauzito wake, kama mwanachama, NSSF ilimtibu bure kwa gharama zao.
Bibi Eunice Chiume ambaye ndiye Meneja mkuu wa uhusiano na masoko wa NSSF alipohojiwa juu ya utaratibu wa utoaji wa huduma hii, anasema matibabu huanza kutolewa baada ya wiki ya 24 ya ujauzito na huishia masaa 48 baada ya kujifungua au siku 7 ikiwa nikujifungua kwa upasuaji. 

Kutokana na Eunice NSSF inatoa huduma yenye lengo maalumu na inayotolewa kwa wajawazito  ikisisitiza juu ya afya wanawake kwa ujumla, maandalizi binafsi ya  kujifungua, utayari wake kwa matatizo yanayoweza kutokea katika  ujauzito, kujifungua na baada ya kujifungua.

NSSF inatoa huduma bure kwa mama mwanachama aliyejiunga na mfuko kwa mfumo wa hiyari au lazima ili kuwawezesha  kuwa na afya ya kutosha katika muda wote wa ujauzito, kujifungua, na baada ya kujifungua. 

“Matibabu haya hufanywa na hospitali ambazo zimeingia mkataba na Shirika wa kutibu wanachama wa NSSF na unaruhusiwa kubadilisha hospitali nyingine pale unapoona huduma zao haziridhishi au iko mbali na eneo la makazi yako” Eunice anakumbusha.

Christian Gaya ni mwanzilishi wa Kituo cha HakiPensheni Tanzania, mshauri na mtaalamu wa masuala ya pensheni. Kwa maelezo zaidi gayagmc@yahoo.com Au kwa habari zaidi za kila siku juu ya HakiPensheni unaweza kutembelea tovuti www.hakipensheni.co,tz au hakipensheni.blogspot.com Simu namba +255 655 13 13 41

No comments :

Post a Comment