Tuesday, July 26, 2016

Jenerali Taban Deng Gai asema amechukua nafasi ya Riek Machar

media

Jenerali Taban Deng Gai
Kundi moja la waasi wa zamani nchini Sudan Kusini limetangaza kuchukua nafasi ya Riek Machar kama Makamu wa rais wa kwanza, baada ya kiongozi huyo kuondoka jijini Juba baada ya kuzuka tena kwa mapigano mapya wiki mbili zilizopita.
Hata hivyo, Machar ambaye haifahamiki yuko wapi, ametupilia mbali taarifa kuwa nafasi yake imechukuliwa na Jenerali Taban Deng Gai aliyeongoza waasi katika mazungumzo ya amani mwaka uliopita nchini Ethiopia.
Jenerali Gai amesema, anashikilia wadhifa huo kwa muda tu na ikiwa Machar atarejea atamwachia.
“Nashikilia nafasi hii kwa muda tu kwa sababu ya amani, na ikiwa Riek Machar atarejea, nitamwachia nafasi hii,” amesema.
Riek Machar Makamu wa kwanza wa rais nchini Sudan Kusini
Mshirika wa karibu wa Machar ameliambia Gazeti la kila siku nchini Kenya Daily Nation kuwa uamuzi wa Jenerali Gai ambaye zamani alikuwa Gavana wa jimbo la Unity halikuridhiwa na viongozi wakuu wa chama cha upinzani cha SPLM-OI na huenda amehongwa na rais Kiir.
Wiki iliyopita, Waziri wa Habari na msemaji wa serikali Michael Makue Lueth alinukuliwa na Gazeti na Sudan Tribune akisema kuwa nafasi ya Machar inaweza kuchukuliwa na mtu mwingine kutoka upande wa upinzani ikiwa Machar kwa mujibu wa mkataba wa amani wa Addis Ababa uliokubaliwa mwaka uliopita.
Riek Machar na rais Salva Kiir baada ya kutia saini mkataba wa amani jijini Addis Ababa mwaka jana
Wakati hayo yakijiri, rais Salva Kiir alizuru jijini Kampala mwishoni mwa juma lililopita kushauriana na rais Yoweri Museveni kuhusu hali inavyoendelea katika nchi yake.
Ripoti zinasema kuwa Kiir, amemwomba msaada wa kijeshi rais Museveni huku kiongozi huyo wa Uganda akimtaka Kiir kukubali kutumwa kwa vikosi vya Kimataifa vya kulinda amani. RFI

No comments :

Post a Comment