SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema itaendelea kuhakikisha mipango yote ya kimaendeleo inayochagizwa na malengo endelevu ya kimataifa inatekelezwa kwa vitendo ili wananchi waweze kunufaika.

Imesema katika malengo ya milennia ya 2015 serikali ilifanikiwa katika baadhi ya sekta zikiwemo sekta za elimu, afya na miundo mbinu hatua zinazotakiwa kuendelea kupewa kipaumbele na wadau wa maendeleo.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Zanzibar, Juma Reli katika Mkutano wa wadau wa sekta za maendeleo nchini wanaojadili utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s) visiwani humo. Mkutano huo ulifanyika katika Hoteli ya Zanzibar Ocean View.

Alisema licha ya kuwepo na changamoto mbali mbali za kiutendaji katika utekelezaji wa mipango hiyo ikiwemo suala la wananchi kutokuwa na uelewa mzuri wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya dunia bado mamlaka husika zinaendelea kutoa elimu hiyo.

Dkt. Tausi Kida
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Kijamii (ESRF), Dkt. Tausi Kida akitoa neno la ukaribisho katika Mkutano wa wadau wa sekta za maendeleo nchini wanaojadili utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s) visiwani Zanzibar ambao umeandaliwa na ESRF kwa kushirikiana na Tume ya Mipango Zanzibar chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini.

Reli alieleza kwamba malengo na mipango mbalimbali ya maendeleo ni kuwasaidia wananchi wa Zanzibar waweze kuondokana na tatizo sugu la umaskini, magonjwa na changamoto za kiusalama.

“Katika MDG tumeweza kufanikiwa kwa baadhi ya malengo ikiwemo suala la elimu na afya lakini kuna mengine bado hatukuweza kufanikiwa kuyafikia na kwa sasa tunaendelea na malengo mapya ya SDG’s ambayo tunatakiwa kuyafanyia kazi ili yaende sambamba na mipango ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.” alisema Reli.

Aidha alisema bado wanajadiliana ni kwa namna gani mipango ya kimataifa tutaiingiza katika sera na mipango yetu ya kimaendeleo ili wananchi waweze kunufaika na fursa hizo za kimaendeleo na kiuchumi kwa ufanisi zaidi.

Alisema utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu SDG’s ambayo ni 17 yanatakiwa kupewa kipaumbele kwani yanagusa nyanja mbalimbali za kijamii yakiwemo maisha halisi ya wananchi wanaostahiki kunufaika na fursa na mahitaji muhimu ya kibinadamu.

Anna Senga, Head of UN Sub Office, Zanzibar
Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa (UN) Ofisi ya Zanzibar, Anna Senga akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini, Bw. Alvaro Rodriguez katika mkutano wa wadau wa sekta za maendeleo nchini kujadili utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s) visiwani Zanzibar.

Kwa Upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafti, Uchumi na Kijamii nchini ( ESRF), Dkt.Tausi Kida akitoa neno la ukaribisho alisema, ili kufikia malengo yaliyokusudiwa katika SDG’s ni vyema sera na mipango endelevu ya nchi husika iweke vipaumbele vya kukuza uchumi kuanzia ngazi za chini

Kida alieleza kwamba katika utekelezaji wa SDG’s lazima kuwepo na mpango endelevu wa ufuatiliaji kuanzia ngazi za chini hadi taifa kwa lengo la kuhakikisha malengo hayo yanatekelezwa kwa mujibu wa matakwa ya malengo ya kimataifa.

Naye Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa (UN), Ofisi ya Zanzibar, Anna Senga alisema endapo malengo ya dunia yataweza kutekelezwa ipasavyo Zanzibar itaweza kupunguza changamoto mbali mbali zinazokabili sekta za kijamii na kiuchumi.

Alisema UN itaendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika utekelezaji wa SDG’s kama ilivyokuwa katika utekelezaji wa malengo ya dunia MDG’s yaliyopita ili serikali iweze kufikia ngazi za chini kwa kuinua kipato cha wananchi kiendane na ukuaji wa uchumi wa nchi.

Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Zanzibar, Juma Reli
Mgeni rasmi Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Zanzibar, Juma Reli akitoa nasha wakati akifungua mkutano wa siku moja wa wadau wa sekta za maendeleo nchini wa kujadili utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s) visiwani Zanzibar ambao umefanyika katika Hoteli ya Zanzibar Ocean View.