Katibu
Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Prof. Justin Ntalikwa akiongea na
baadhi waandishi wa habari mara baada mkutano ya wafanyabiashara wa
sekta ya mafuta nchini jijini Dar es salaam. Ameelezwa kuwa Tanzania ina vigezo mbalimbali ambavyo vinaifanya nchi ijiamini kwa asilimia 98 kuwa mradi wa bomba la kusafirishia mafuta kutoka Ziwa Albert nchini Uganda utapitia Kaskazini mwa Tanzania hadi Bandari ya Tanga badala ya nchini Kenya.
Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu
wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa wakati wa kikao
chake na wafanyabiashara wa mafuta nchini ambacho kililenga kujadiliana
nao kuhusu fursa za uwekezaji zitakazotokana na mradi huo endapo utapita
nchini.
Profesa Ntalikwa alivitaja
vigezo hivyo kuwa ni uzoefu wa Tanzania katika ujenzi wa mabomba ya
kusafirisha nishati mbalimbali ikiwemo Bomba la
Mafuta la kutoka Tanzania hadi Zambia (TAZAMA), Bomba la kusafirisha
gesi kutoka SongoSongo hadi Dar es Salaam, Bomba la kusafirisha gesi
kutoka eneo la Mnazi Bay hadi Mtwara, pamoja na Bomba kuu la gesi kutoka
mkoani Mtwara hadi Dar es Salaam lenye kipenyo cha inchi 36 hivyo
uzoefu huo utasaidia katika kupunguza muda wa ujenzi wa bomba la mafuta
ambalo kipenyo chake ni inchi 24.
“Tumewaeleza
wenzetu kuwa Serikali ya Tanzania pia ilishajenga uwezo mkubwa katika
masuala ya kutwaa, kumiliki na kulipa madai ya wananchi wanaopisha
miradi ya mabomba na shughuli hizi zimekuwa zikifanywa kwa wepesi na
umakini mkubwa ikiwemo umakini katika kufuata kanuni na sheria za
mazingira, hivyo haitatuwia ngumu katika kutekeleza mradi huu,” alisema
Profesa Ntalikwa.
Alitaja
kigezo kingine kuwa ni ubora wa bandari ya Tanga ambayo imeonekana kuwa
ni bora zaidi ukilinganisha na Bandari nyingine Afrika Mashariki kwa
kuwa ina kingo za asili (naturally sheltered) na kina kirefu
hivyo kupunguza muda na gharama za ujenzi kwa kuwa uchimbaji wa kuongeza
kina hauhitajiki na itakuwa na uwezo wa kupakia mafuta katika kipindi
cha mwaka mwaka mzima.
Profesa
Ntalikwa aliongeza kuwa njia ya kupitia Tanzania hadi Bandari ya Tanga
ni bora zaidi kwa upande wa ujenzi wa bomba hilo kwa kuwa haipiti sehemu
yenye makazi ya watu wengi, sehemu za hifadhi na haina miinuko mikali
hivyo kupunguza muda wa ujenzi na gharama za ujenzi.\
“ Hivyo ndugu
zangu tumewaita wafanyabiashara hawa wa mafuta nchini ili waweze
kutumia fursa mbalimbali zitakazotokana na mradi huo na kuzichangamkia
na wao wamepokea vizuri suala hili na wameahidi kushirikiana na Serikali
katika kuhakikisha kwamba Tanzania inapata mradi huu muhimu,” alisema
Profesa Ntalikwa.
Awali
akizungumza kuhusu mradi huo, Mkurugenzi wa Mkondo wa Chini kutoka
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Dkt. Wellington Hudson
alieleza kuwa Uwekezaji wa mradi bomba hilo unakadiriwa kugharimu Dola
za Marekani bilioni 4 na kwamba Bomba lote litakuwa na urefu wa
kilomita 1403 na kipenyo cha inchi 24.
Alisema kuwa
hatua zilizofikiwa hadi sasa ni kuwa Serikali za Tanzania na Uganda
zilishatiliana sahihi Mkataba wa Maelewano (MOU) tarehe 12 Oktoba 2015
ambao kwa sasa ndiyo mwongozo wa kukamilisha majadiliano ya mikataba
mbalimbali ambayo inayohitajika kisheria.
“Kwa sasa
lengo ni kukamilisha mazungumzo mapema na kusainiwa kwa Mikataba husika,
ili kuruhusu shughuli za upatikanaji wa mkuza na ujenzi kuanza
maramoja. Ujenzi unatarajiwa kukamilika ndani ya miaka mitatu baada ya
Mikataba yote muhimu kusainiwa,” alisema Dkt. Wellington.
Alitaja
baadhi ya faida zitakazopatikana kutokana na mradi huo kujengwa Tanzania
kuwa ni kuchochea shughuli za utafutaji mafuta nchini hususani katika
maeneo linapopita bomba la mafuta, Kuimarisha matumizi ya Bandari ya
Tanga na hivyo kuongeza mapato ya Serikali kutoka katika bandari hiyo
pamoja na kupatikana mkuza utakaoweza kutumika siku za baadaye kwa
shughuli nyingine za maendeleo ikiwemo kusafirisha gesi na mafuta katika
mikoa ya Kaskazini, Kanda ya Ziwa na nchi za jirani.
Faida
nyingine zitakazotokana na mradi huo ni Ujenzi wa barabara mpya takriba
kilometa 200 na uboreshaji wa barabara zilizopo takriban kilometa 150 na
madaraja katika maeneo linapopita bomba,
Pia
kuongezeka kwa fursa ya Shirika la Reli Tanzania kufanya biashara ya
kusafirisha kiwango cha mabomba yanayokadiriwa kufikia 123,000 kupitia
miundombinu ya reli iliyopo, Fursa za ajira kwa takribani watu 15,000
wakati wa ujenzi na watu wapatao 1,000 wakati wa kuendesha mradi.
Dkt.
Wellington pia aliwaasa Watanzania kuchangamkia fursa zitakazojitokeza
endapo bomba hilo litapita nchini na kuzitaja baadhi ya fursa hizo kuwa
ni kazi za kuunganisha mabomba (welding), huduma za afya, huduma
za mabenki, huduma za usafi na kudhibiti taka, Kandarasi za kujenga na
za umeme, huduma za Bima, Huduma za mawasiliano na mtandao, kandarasi za
ujenzi wa Mabarabara na Huduma za uuzaji mafuta.
Alitaja fursa
nyingine zitakazopatikana kuwa ni Karakana za ukarabati wa mashine
mbali mbali na magari, Huduma za sheria, Huduma za Mawasiliano na
Kandarasi za kusamba vifaa vya ujenzi.
Kwa upande
wake Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Biashara, Dkt. Gideon Kaunda
akiongea kwa niaba ya wafanyabiasahara hao aliishuukuru Serikali kwa
kuamua kuwashirikisha katika suala hilo muhimu kwa manufaa ya nchi na
kuahidi kushirikiana nayo ili kuhakikisha kuwa lengo la Serikali la
kuhakikisha bomba hilo la Mafuta linapita Tanzania linafanikiwa.
No comments :
Post a Comment