Friday, June 5, 2015

NSSF kutoa mikopo kwa wanachama wake kupitia kwa waajiri



 
Dr Ramadhani Dau Mkurugenzi Mkuu wa NSSF

Christian Gaya Majira Jumamosi Juni 06, 2015
Kuanza mwaka ujao wa fedha shirika la taifa la hifadhi ya jamii litaanza kutoa mikopo kwa wanachama wake kupitia kwa waajiri wake. haya yalisemwa na mkurugenzi wa uwekezaji na miradi ndugu Yacoub Kidula wakati akiwasilisha mada yake juu ya hifadhi ya jamii na ujasiriamali katika mkutano mkuu wa wadau uliofanyika  Ukumbi wa Simba Hall AICC-Arusha  ambapo Mgeni rasmi alikuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Mizengo Kayanza Peter Pinda. Kidula alisema mpaka sasa NSSF imetoa mikopo ya riba nafuu kwa wanachama wake ambao wengi wao ni wajasiriamali ipatayo thamani ya shiilingi bilioni 55.6 za kitanzania kwa wanachama wapatao 6,920 kwa kupitia SACCOS 159, AMCOS 11na MFIs 2

Haya yalifafanuliwa zaidi na mkurugenzi mkuu wa NSSF Dakt Ramadhani Dau wakati alipokuwa akitoa risala yake kwa wanachama  na wadau mbalimbali  waliohudhuria wapatao zaidi ya 1000 katika mkutano huo mkuu wa 2015 ya kwamba mikopo inayotolewa NSSF kwa ajili ya ujasiamali ni ya masharti nafuu sana, muda mrefu wa marejesho na riba za chini kabisa ukilinganisha na hali ya soko.
“Muda wa marejesho ya mikopo hii ni kati ya miaka miwili na mitano wakati riba ni kati ya asilimia 9.32 na 10.68 kwa mwaka ukilinganisha na viwango vya riba sokoni vya kati ya asilimia 15 had 30” alisema Dakt Dau

“ Kwa sasa tumeamua kutoa mikopo ya riba nafuu kwa wanachama wetu kupitia waajiri wao ili kuwafikia wengi zaidi kuliko kupitishia kwenye SACCOS ambapo wengi wa wanachama sio wanachama wa SACCOS na hivyo kuwarahisishia wa kupata mikopo kwa muda mfupi zaidi, kujenga mshikamano zaidi sehemu za kazi, na kuwasaidia waajiri kuongeza uzalishaji wenye tija zaidi, kuwapunguzia ukali wa maisha wanachama na hivyo kupunguza umasikini kama sio kuondoa kabisa, ili mradi mwajiri akubali kutoa dhamana kwa kila mwanachama atakayehitaji kupata mkopo kutoka NSSF”alisema Kidula.

Kuhusu masharti ya mwanachama kupata mkopo Yacoub alisema mwajiri anatakiwa kuwa mchangiaji hai wa muda wa miaka mitatu (3) na kwa upande wa mwanachama atatakiwa awe mchangiaji hai wa mfuko wa NSSF kwa muda wa miezi sita ( 6)

Alisema kuanzia mwaka ujao wa fedha watatumia mawakala mbalimbali watakaotumika kuwaandikisha wanachama kutoka katika sekta isiyo rasmi na walioko ughaibuni yaani diaspora

Naye Bibi Delifina Masika ambaye ni meneja mkuu wa mkoa wa Arusha alisema wakati alipokuwa akisoma taarifa juu ya NSSF mfuko bora kwa hifadhi ya jamii Tanzania ya kuwa ukubwa na idadi wa wanachama wa NSSF katika soko la sekta ya hifadhi ya jamii kulingana na utafiti uliofanywa hivi karibuni inaonesha ya kuwa mpaka sasa NSSF inachukua asilimia 53 wakati mifuko mingine inagawana asilimia 47 zilizobaki
“Kima cha chini cha pensheni kwa wastaafu wa NSSF ni shilingi 80,000/- kwa mwezi wakati kima cha juu cha pensheni kwa wastaafu wa NSSF ni shilingi milioni 10,685,000/- hivyo shirika lina uwezo wa kujiendesha na kulipa mafao kwa wanachama wake kwa miaka saba (7) bila kukusanya michango hivyo basi NSSF ni Shirika IMARA kwani mpaka kuishia Juni 2014 mfuko ulikuwa na thamani ya shilingi trilioni 2.6 na kufikia mpaka Juni 2015 mfuko unakadiriwa kuwa na thamani ya shilingi trilioni 3” Masika alifafanua.
Mwisho

No comments :

Post a Comment