Baadhi ya wadau wa
mfuko wa sekta ya hifadhi ya jamii waliohudhulia mkutano wa nne wa Shirika la
Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwenye Ukumbi wa Simba Hall AICC-Arusha mwaka
jana 2014, ambapo mgeni rasmi alikuwa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete. Madhumuni ya mkutano huu wa
TANO wa wadau kwa mwaka 2015 utakuwa kwa ajili ya kutathmini na kujadili
maendeleo na maboresho ya sekta nzima ya hifadhi ya jamii, mchango wake katika
kuongeza ajira, kuchochea ujasiriamali na kuboresha michezo nchini. Mgeni rasmi
atakuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Mizengo
Kayanza Peter Pinda
Wajibu wa mifuko ya pensheni
ya hifadhi ya jamii ni kuhakikisha ya kuwa inawashirikisha wadau wake wote
wakuu hasa wanachama, waajiri na serikali, ambapo makundi hayo matatu yanaunda
kitu kinachoitwa utatu. Wawekezaji wa mifuko hii ni wafanyakazi na waajiri pale
wanapojiandikisha na kuwa wanachama wachangiaji kwa kukatwa asilimia fulani
kutoka katika mishahara yao na mwajiri na yeye kuchangia kiasi hicho hicho kila
mwezi au zaidi kwa ajili ya mfanyakazi wake kwa makubaliano ya kupata huduma
mbalimbali za mafao za muda mfupi na za muda mrefu kutoka katika mifuko ya
pensheni ya hifadhi ya jamii.
Hivyo uwakilishi wao lazima
uwemo ndani ya utawala wa mifuko hii ya pensheni ya hifadhi ya jamii mara kwa
mara tena kwa vitendo. Vile vile inatambulika kuwa hata serikali ina kazi kubwa
juu ya mifuko hii ya hifadhi ya jamii hasa zaidi kwa kuangalia na kusimamia
kiwango cha kinga juu ya majanga wanayokumbana nayo jamii hapa nchini pamoja na
kuangalia mchango wa mifuko hii kwa upande wa uchumi wa nchi yetu na serikali
kama mdhamini mkuu wa mifuko hii ya pensheni ya hifadhi ya jamii chini ya
msimamizi na mdhibiti wa sekta hii ya hifadhi ya jamii.
Njia mojawapo ya wadau wa
mifuko ya hifadhi ya jamii ni kufuatilia na kujua utendaji wa mifuko hii
inayosimamiwa na bodi za wadhamini kwa njia ya mikutano mikuu inayofanyika kila
mwaka. Ambapo wadau kama vile wanachama ambao ndio wachangiaji na waaajiri
ambao mara nyingi ndio waliodhaminiwa au wakala wa kuhakikisha ya kuwa
wanashirikiana na mifuko hii kama vile kusimamia ukataji na kupeleka michango
kwenye mifuko ya hifadhi na kuhakikisha ya kuwa wanatunza kumbukumbu za
wafanyakazi wao, pamoja na wawakilishi kutoka katika vyama mbalimbali vya
wafanyakazi nchini na baadhi ya taasisi za serikali na zisizo za kiserikali.
Kwa kawaida hii inakuwa
nafasi ya kipekee na muhimu sana kwa wadau kama wanachama wa mifuko hii ya
hifadhi ya jamii kuhudhuria kwa ajili ya kuzungumzia mambo muhimu yanayogusa
afya na ustawi wa mifuko zinazohusiana na taarifa za hesabu, taarifa za ukaguzi
wa mahesabu, zinazohusiana na taarifa za bodi ya wadhamini wa mifuko na kujua
nafasi na uwezo wa mfuko kifedha na za kiutekelezaji. Lakini pamoja na hayo
wadau wanakuwa na haki ya kujua maamuzi muhimu yaliyoamuliwa kwa mfano na
mkutano wa mwaka jana ambayo yalipewa kipa umbele pamoja na yatokanayo ambapo
tumeona mara nyingi wadau kama mwanachama inakuwa nafasi nadra sana kwao kama
wachangiaji kuitumia vizuri.
Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii
wa NSSF unategemea kuwa na mkutano wa TANO wa wanachama wa mfuko na wadau
mbalimbali wa sekta ya hifadhi ya jamii katika Kituo cha Kimataifa cha Arusha
(AICC) ukumbi wa Simba Hall utakaoanza tarehe 02 mpaka 04 Juni, 2015. Wanachama
na wadau wote wa sekta ya hifadhi jamii wakiwemo wenyeviti na wajumbe wa bodi,
maofisa watendaji wakuu, maofisa wanaoshughulika na raslimali watu na utawala,
sheria, uhasibu, fedha, teknolojia na mawasiliano na bima, kutoka serikali kuu
na taasisi za serikali, mashirika ya umma, makampuni binafsi, mashirika yasiyo
ya kiserikali pamoja na wawakilishi wa vyama vya wafanyakazi kutoka sehemu za
kazi, vyama vya waajiri na watu wengine wowote watakaopenda kushiriki kwa lengo
la kutaka kujua na kupata elimu ya masuala ya hifadhi ya jamii.
Madhumuni
ya mkutano huo utakuwa kwa ajili ya kutathmini na kujadili maendeleo na
maboresho ya sekta nzima ya hifadhi ya jamii, mchango wake katika kuongeza
ajira, kuchochea ujasiriamali na kuboresha michezo nchini. Mgeni rasmi atakuwa
Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Mizengo Kayanza
Peter Pinda
Kwa
maana hiyo wanatakiwa kuandaliwa mapema kwa muda muafaka na kupewa habari bora
na za hali ya juu na isipofanyika hivyo
basi uwezo wa nguvu wa kisheria waliopewa unakuwa hauna nguvu yeyote kwa
wanachama, waajiri na hata kwa wadau wengine. Ni wajibu wa bodi ya wadhamini ya
NSSF kuhakikisha ya kuwa taarifa za kuwapasha wadau zinawafikia wadau wa mfuko
huu juu ya kufanyika mkutano mkuu wa mwaka kwa muda muafaka. Maswali ya
kujiuliza ni kama vile taarifa au habari hizo zinazotolewa na NSSF zina ubora
gani na je, zimewafikia wadau wanaohusika kwa muda unaotakiwa?
Na kwa upande mwingine mtu
anaweza kujiuliza ya kwamba chukulia ya kuwa mwanachama amepelekewa habari na
kupata taarifa mapema juu ya kuhudhuria mkutano mkuu wa tano (5) wa wanachama
na wadau wa NSSF. Je baada ya hapo inafuatiliwa ili kuhakikisha ya kuwa hawa
wanachama na wadau watakaochaguliwa kuwawakilisha wenzao kwenye mkutano huo
watawajibika kama inavyotakiwa.
Hivyo kwa upande mwingine
unaweza kusema ya kuwa wadau kupatiwa taarifa kwa muda muafaka hiyo haitoshi
kabisa kinachotakiwa hapa ni kwa hali na
mali mdau kuwa tayari kujua au kuelewa kilichoandaliwa kwenye makabrasha ambalo
ni jambo linaloonekana kuwa ni tatizo kubwa kwa wanachama na wadau wengi wa
mifuko ya hifadhi ya jamii hapa nchini.
Chukulia madhalani mtu
mwingine kuwa na mashaka na kilichopo ndani ya makabrasha kama siyo pambo tu la
kuvutia mfuko kwa idadi kubwa ya wanachama. Kwa upande mwingine wanachama mara
nyingi wameonekana kuwa ni kundi ambalo halina nguvu kabisa kwa kusimamia
utendaji na uendeshaji wa mifuko ya hifadhi ya jamii ikiwemo kufuatilia tabia
na utaratibu wa utendaji wa wadhamini au bodi hizi za hifadhi ya jamii na hata inaonekana wanatofautiana katika mitazamo
kwa upande mwingine
Tunategemea NSSF kutumia
vyombo vya habari kwa ajili ya kuwahabarisha idadi kubwa ya wadau wengine ambao
hawatapata nafasi kuhudhuria kuhamasishwa kwa njia ya programu za redio,
runinga, blog, facebook, twitter, you tube, google, linkedln, magazeti n,k.
Christian Gaya ni
mwanzilishi wa Kituo cha HakiPensheni Tanzania, mshauri na mtaalamu wa masuala
ya pensheni. Kwa maelezo zaidi wasiliana kwa barua pepe: gayagmc@yahoo.com Au kwa habari zaidi za
kila siku juu ya HakiPensheni unaweza kutembelea tovuti www.hakipensheni.blogspot.com
Simu namba +255 655 13 13 41
No comments :
Post a Comment