Na Mussa Juma, Mwananchi
Kwa ufupi
- Abainisha namna ya kuinusuru shilingi, asema ni suala la kitaalamu zaidi, akemea siasa kuingilia suala hili.
Arusha. Gavana wa Kwanza wa
Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Edwin Mtei ametoa somo kwa benki hiyo
kuinusuru shilingi isiendelee kuporomoka kwa kutumia akiba ya fedha za
kigeni ilizonazo.
Katika siku za karibuni, thamani ya shilingi dhidi
ya fedha za kigeni, hasa dola, imeporomoka hadi kufikia Sh2010 kwa dola
moja ya Marekani.
Akizungumza jana, Mtei alisema hakuna chombo kingine kinachoweza kusaidia tatizo hili zaidi ya Benki Kuu, kwa sasa.
“Hili ni suala la kitaalamu siyo la kisiasa, Benki
Kuu lazima itumie wataalamu wake sasa, kuhakikisha wanailinda shilingi
na hatuwezi kulalamikia mataifa ya nje katika hili,” alisema.
Mtei ambaye alijiuzulu kutokana na mgogoro kama
huu alisema, BoT ni lazima isaidie Serikali kudhibiti manunuzi nje ya
nchi na itoe sehemu ya akiba yake ya fedha za kigeni.
“Mimi nilijiuzulu katika masuala haya ya thamani ya fedha yetu, tulitofautiana na Mwalimu Julius Nyerere,” alisema.
Alisema anakumbuka wakati wa uongozi wao,
waliwahi kushusha dola hadi kufikia Sh12 na hakuna chombo cha nje
kilichowahi kulalamika kwani hili ni suala la ndani ya nchi.
Mshauri Mwandamizi wa Masuala ya Uchumi na Mipango
mkoani Arusha, Saimon Mapolu akizungumzia kushuka kwa thamani ya
shilingi alisema, inatokana na upungufu katika sera ya fedha na sheria
zilizopo.
Mapolu, hata hivyo, alisema kwa hali ya sasa, BoT inaweza kudhibiti hali isiwe mbaya zaidi.
Alisema hakuna maana kuwa na akiba nyingi ya fedha za kigeni wakati shilingi ikiwa sio imara
No comments :
Post a Comment