.
PICHANI: Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Uhamasishaji wa SSRA Sarah Kibonde Msika akiongea na waandishi wa habari kuhusu Miongozo ya Sekta ya Hifadhi ya Jamii iliyotolewa na SSRA. Kushoto kwake ni Mkurugenzi wa Sheria wa SSRA Ngabo Ibrahim
Na Christian Gaya majira 26 Novemba 2013
PICHANI:
Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Uhamasishaji wa SSRA Sarah Kibonde Msika
akiongea na waandishi wa habari kuhusu Miongozo ya Sekta ya Hifadhi ya Jamii
iliyotolewa na SSRA. Kulia kwake ni Mkurugenzi wa Sheria wa SSRA Ngabo Ibrahim.
Muundo
wa kisheria wa mifuko ya hifadhi jamii nchini ni moja changamoto zinazoikabili
Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii nchini (SSRA). Mpaka sasa mifuko
inaendelea na mtindo wa kuwaruhusu wanachama wake kutoa mchango ya pensheni
wakati wowote anapopatwa na majanga kama vile kuacha kazi au kuachishwa kazi,
magojwa, ulemavu, kuolewa na wanapofikia umri wa miaka 55 ya hiyari au 60 ya
lazima. Na mwanachama anapotoa michango hiyo ya pensheni uhusiano kati ya
mwanachama na mfuko unakoma hapo hapo.
Udhaifu mwingine ni
kwamba mafao yanatolewa na baadhi ya mifuko mengine hayatambuliwi na shirika la
kazi (ILO) kifungu cha 102 cha mwaka 1952 na hata hivyo mifuko mengi
hairekebishi pensheni au mafao yanayotolewa kulingana na mfumuko wa bei ya
wakati huo au mwongozeko wa kima cha chini cha mshahara .
Riba wanayopata
mwanachama kutokana na michango yake kuwekezwa kwenye miradi mbalimbali na
mfuko inaendelea kuporomoka kila mwaka
mfano mwaka 1996-1997 mfuko mmoja ulitoa riba kwa wanachama wake kwa asilimia
12 ½ ambayo mpaka sasa imefika riba ya asilimia 0.0034 kwa mwaka kulingana na
maelezo ya taarifa ya hesabu za michango ya wanachama
Na kwa vile mwanachama wanachukua
michango yote ya pensheni kwa mkupuo hivyo muda mfupi mtu huyo anabaki kuwa
maskini zaidi, na kupatwa mawazo na magonjwa hatimaye kufa haraka na hivyo
idadi ya watu maskini inazidi kuongezeka nchini. Mifuko haishughuliki au
kuhusika kabisa na majanga hivyo yote yanatupiwa kwa mwanachama
aliyejitoa.
Pamoja na hayo mifuko
hii yote ina wigo mdogo sana wa wanachama na wale ambao ni wanachama wa hifadhi
ya jamii ni asilimia 6 ya nguvukazi ya idadi ya watu watu nchini. Mpaka kufikia mwaka 2012 kulikuwa na jumla ya
wastaafu wapatao 70,522. Na mbinu zinazotumika za uendeshaji wa mifuko
zimepitwa na wakati. Nchi kwa muda mrefu haina sera kwa ajili ya kusimamia
utawala bora wa hifadhi ya jamii na kwa maendeleo ya hifadihi nchini.
Siyo hivyo mifuko ya hifadhi
ya jamii mpaka sasa haina utaratibu wa kuhamisha michango ya mwanachama kutoka
mfuko mmoja wa hifadhi ya jamii kwenda mwingine endapo mwanachama atapata
mwajiri mwingine anayechangia labda PPF badala ya NSSF na hata akihamishwa kwenda
nchi jirani kama vile Kenya au Uganda kama wanachama chini ya jumuuiya ya
afrika mashariki hivyo anaishia kutoa na kuitumia anavyojua yeye mwanachama
Mpaka sasa mdhibiti
na msimamizi wa mifuko ya hifadhi ya jamii (SSRA) ameanza kuleta marekebisho ya
baadhi ya vifungu vya sheria kwa awamu
kwa mfano waajiri wote katika utumishi wa umma na sekta binafsi
wanapaswa kuzingatia matakwa ya sheria hii kwa kuwapa fursa watumishi wapya
kujiunga na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya lazima wanayoitaka. Bado ni
changamoto kubwa sana kwa SSRA kuleta na kufanya marekebisho haya yote. kwani mpaka sasa haya mashirika ya hifadhi ya jamii
kila moja ina wizara yake inayoisimamia na kuwa utaratibu na kanuni tofauti za
uendeshaji wa mifuko hii. Matokeo yake ni kwamba kiwango cha michango, mfumo wa
mafao, na sifa za kupata mafao na hata mipako na vipa umbele vinatofautiana
kabisa kwa kila mfuko. Kumekuwepo na fofauti
kubwa kwenye ukokotoaji wa mafao na hata tofauti kubwa ya mafao kati ya mifuko
Mpaka sasa
hakuna utaratibu ulioanzishwa wa kuruhusu haki za mafao ya mwanachama kuhamishwa
kutoka mfuko mmoja hadi mwingine. Matokeo yake wafanyakazi wamekuwa wakipoteza
baadhi ya haki zao za mafao wakati wakihama kutoka sehemu moja ya mwajiri hadi
mwajiri mwingine. Pia hii imechangia sana kuongezeka kwa tabia ya kuondoa
michango ya pensheni kabla haijakomaa.
Kumekuwa hakuna
soko huru la hifadhi ya jamii ambalo linaweza kumruhusu hata taasisi za watu
binafsi au sekta za watu binafsi kuendesha mifuko ya hifadhi ya jamii kwa muda
mrefu ingawa kwa sasa wameruhusu lakini muundo rasmi haujatoka bado kutoka kwa
mdhibiti na msimamizi wa hifadhi ya jamii (SSRA) ;
kumekuwepo na ukosefu wa takwimu sahihi; gharama kubwa za uendeshaji wa mifuko,
uelewa mdogo wa hifadhi ya jamii kwa watunga sera, waajiri na waajiriwa na umma
kwa ujumla. kila
mfuko una sera yake ya uwekezaji, wigo finyu wa hifadhi ya jamii kwa Watanzania
yote kwa pamoja ikiwa imesajili asilimia mbili tu ya Watanzania wote.
Miongozo ya
uwekezezaji wa rasilimali za mifuko hii ya hifadhi ya jamii ingawa imetolewa
tayari lakini haijaanza kutumika na baadhi ya mifuko. Mapungufu yaliyomo kwenye mfumo huu wa hifadhi ya jamii ambayo
yanahitajika kutatuliwa na sera hii ya hifadhi ya jamii. Watu waliomo
katika mifuko hii ya hifadhi ya jamii ni wale tu ambao wameajiriwa kwenye sekta
iliyo rasmi
Mamlaka
ya usimamizi na udhibiti wa sekta ya hifadhi ya jamii (SSRA) iliundwa kwa
sheria Na 8 ya hifadhi ya jamii ya mwaka 2008 kwa lengo la kusimamia na
kudhibiti sekta ya hifadhi ya jamii kwa manufaa ya wanachama na kwa taifa kwa
ujumla. Hivyo basi Mamlaka ilianza kazi rasmi mwaka 2010 ingawa baadaye
ilifanyiwa marekebisho chini ya kifungu cha sheria namba 5 cha mwaka 2012
Na jukumu kubwa la
mamlaka ni kusimamia shughuli zote za hifadhi ya jamii nchini ikiwa ni pamoja
na mifuko yote ya hifadhi ya jamii iliyo anzishwa kwa sheria ya bunge ambayo ni
mifuko ya pensheni, mifuko ya akiba ,mifuko ya bima ya afya na mifuko ya hiari
na kuhakikisha kwamba mifuko inakuwa endelevu ,inaendeshwa kwa kufuata kanuni
na taratibu za kisheria, wanachama wanapata taarifa za mifuko yao ,mafao
yanaboreshwa na serikari inapunguziwa mzigo .Dhana kubwa ya hifadhi ya jamii ni
kwa ajili ya kuhusisha taratibu za ulinzi dhidi ya majanga ya kiuchumi na ya
kijamii yanayosababishwa na kukoma au kupungua kipato kutokana na maradhi,
uzazi, kuumia kazini, ukosefu wa ajira, ulemavu, uzee, kifo na kuongezeka kwa
gharama za matibabu.
Pamoja na hayo SSRA
imepewa mamlaka makubwa ya kufanya tathmini ya mifuko ya hifadhi ya jamii,
kuchukua hatua za kinidhamu pale inapobidi, kufanya kaguzi mbalimbali na
kutekeleza wajibu mwingine wowote utakaohakikisha sekta ya hifadhi ya jamii
inafanya kazi kwa ufanisi na kwa uongozi bora.
Majukumu ya mamlaka (SSRA) yameainishwa bayana chini ya kifungu cha 5(1)
cha sheria ya mamlaka ya usimamizi na
udhibiti wa sekta ya hifadhi ya jamii kazi hizo ni pamoja na Kusajili mifuko,
watunzaji na meneja wa uwezaji katika sekta ya hifadhi ya jamii.
Kudhibiti/kurekebisha na kusimamia utendaji wa mifuko, watunzaji na meneja wa
uwekezaji. Kuweka mazingira yakayopanua uwigo wa hifadhi ya jamii na kuongeza
wanachama hasa kwenye sekta isiyo rasmi.
Mamlaka hii vile vile
ina jukumu la kutoa miongozo ya utendaji sahihi na yenye ubora katika sekta ya
hifadhi ya jamii. Kutetea na kulinda maslahi ya wanachama. Kuweka mazingira mazuri
na yanayofaa kukuza na sekta ya hifadhi ya jamii. kuendeleza Kumshauri waziri
juu ya sera na masuala ya utendaji kuhusiana na sekta ya hifadhi ya jamii.
Miongozo mengine ni
pamoja na kupanga na kutangaza rasmi miongozo itakayo tumika kwa mifuko, watunzaji na. Kusimamia na
kupitia upya utendaji wa sekta ya hifadhi ya jamii. Kuanzisha mafunzo, kushauri,
kuratibu na kutekeleza mabadiliko ya sheria katika hifadhi ya jamii. Kumteua
mtu atakae simamia mifuko pale inapobidi. Kurahisisha upanuzi wa wigo wa hifadhi
ya jamii kuwafikia wale ambao bado hawajafanikiwa ikiwa ni pamoja na makundi/sekta zisizo rasmi . Kuendesha
mipango ya elimu na uhamasishaji kwa umma juu ya masuala ya hifadhi ya jamii.
Vilevile Mamlaka
inajukumu la kulinda, kutetea na kuendeleza maslahi ya wanachama wa sekta
ya Hifadhi ya Jamii. Kwa kuzingatia haya, Mamlaka imetoa miongozo sita ambayo
yote inalenga katika kuhakikisha kuwa sekta ya hifadhi ya jamii inakuwa bora na
endelevu na hivyo kuboresha maisha ya wanachama na kuchangia maendeleo ya nchi
kwa ujumla.
Kwa
upande wa uandikishaji wa wanachama Miongozo hii inalenga;
Kuongoza Bodi za Mifuko ya hifadhi ya jamii
kufanya usajili wa wanachama kwa mujibu wa sheria; Kuhakikisha kwamba mwanachama mpya anapata haki yake ya kuchagua
Mfuko wa Hifadhi ya Jamii anaopenda kujiunga nao; Kuondoa migongano kati ya Mifuko wakati wa uandikishaji wanachama
wapya; Kuainisha taratibu kwa
mwanachama wa Mfuko wa hiari kuhamia Mfuko wa lazima; Kuongeza wigo wa wanachama
katika sekta ya hifadhi ya jamii.
Miongozo
ya uwekezaji, hii inalenga ; Kuelekeza Bodi za Mifuko kufanya maamuzi ya uwekezaji kwa mujibu
wa sheria; Kuhakikisha uwekezaji wa Mifuko unaleta maendeleo bila kuhatarisha
afya ya Mifuko, pamoja na kuhakikisha uwekezaji unafanywa kwenye maeneo yenye
tija, kukuza uchumi wa nchi na kuboresha mafao ya wanachama; Kuhakikisha kwamba
Mifuko muda wote inaweza kulipa wanachama wanaostahili mafao; Kuhakikisha kuwa
utawala bora; unazingatiwa katika shughuli zote za uwekezaji na Kuhakikisha
kuwa wanachama wananufaika na uwekezaji
unaofanywa na Mifuko.
Mamlaka
vile vile imetoa miongozo ya takwimu inayolenga; Kuainisha
kumbukumbu ambazo ni lazima zitunzwe na Mifuko; Kuelekeza mifumo ya kuandaa na kuweka taarifa za Mifuko; Kuelekeza taratibu za kutoa taarifa za
wanachama na michango yao; Kuelekeza
taratibu za kuhahikisha kwamba taarifa za Mifuko zinapatikana muda wowote
zinapohitajika.
Pamoja
na hayo mamlaka imeweza kuja na miongozo ya utawala bora wa bodi za Wadhamini
inayolenga; Kukuza utawala bora katika bodi za Mifuko; Kanuni
za Mifuko kuzingatia vigezo vya utawala bora katika uendeshaji wake; Kuwaongoza wadhamini kutimiza wajibu
wao kisheria; Kuweka sifa na
masharti ya mtu kuwa mjumbe wa Bodi ya Mfuko; Kuweka viwango vya taratibu na miundo vya kukuza utawala bora; Kukuza na kuendeleza imani ya umma kwa
Mifuko
Kwa
upande mwingine Mamlaka imeaanisha miongozo ya tathmini za Mifuko inayolenga: Kuweka
taratibu za namna ya kufanya tathmini za mifuko; Kuweka vigezo vya kuzingatia kwa makampuni na wataalum wanaotarajia
kufanya tathmini za mifuko; Kufanikisha kupata taarifa ya tathmini inayoeleweka na yenye taarifa
sahihi.
Mamlaka
imeweza kuja na taratibu za miongozo ya kujumulisha vipindi vya michango
inayolenga: Kuainisha
taratibu za kujumlisha vipindi vya michango kwa wanachama waliochangia katika
Mifuko zaidi ya mmoja; Kuainisha
masharti ya kuunganisha vipindi; na Kumsaidia
mwanachama aliyechangia Mfuko zaidi ya mmoja kupata haki yake stahiki.
Imefikia wakati sasa mifuko ya hifadhi ya jamii
inahitaji kubadilika kimtazamo na kidira imefika wakati ambapo mteja huenda
akaonekana ni mfalme. Mifuko ya jamii nchini inahitaji kujua hili ili kujipanga
upya na kuhakikisha ya kuwa inajali wateja wao hasa kwa kutoa huduma bora kwa
wanachama na wastaafu pamoja na washika dau wengine kama vile wamama, wababa na watoto tegemezi. Mashirika
ya hifadhi ya jamii yanahitaji kupokea malalamiko ya wanachama wao na kujibu
kwa muda muafaka ili kuwaridhisha kama wenye wachagiaji wa michango hiyo. Wanahitaji
kutimiza ahadi wanazotoa kwa wanachama kwa wakati muafaka na siyo vinginevyo.
Wakati umefika wa kubadilisha sheria zilizopitwa na
wakati na ukiritimba, kila mmoja anahitaji kuingia uwanjani kwa kuuza sera zake
ili kumvutia mteja. Mifuko inahitajika kubadilika juu ya suara hili la mabadiliko
ya marekebisho ya sheria na miongozo ya utendaji ya sekta ya hifadhi ya jamii
nchini
Christian
Gaya ni mwanzilishi wa kituo cha HakiPensheni Tanzania, mshauri na mtaalamu wa
masuala ya hakipensheni. Kwa maelezo zaidi wasiliana kwa barua pepe: gayagmc@yahoo.com AU kwa habari zaidi za kila siku
juu ya HakiPensheni unaweza kutembelea tovuti www.hakipensheni.blogspot.com simu namba +255 655 13 13 41
No comments :
Post a Comment