Tuesday, November 26, 2013

Pinda azitaka Serikali za Mitaa kugawa maeneo ya uwekezaji


Waziri Mkuu Mizengo Pinda (katikati) akiwa kwenye  Mkutano wa Ushirikiano wa Serikali za Mitaa za Tanzania na China jijini Dar es Salaam jana. Kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia na kulia ni Naibu Gavana wa Jimbo la Shandong nchini China, Xia Geng.Picha na Michael Jamson . 
Na Ibrahim Yamola, Mwananchi
Kwa ufupi
  • Pia amezishauri  serikali hizo kuonyesha fursa zilizopo katika uwekezaji  kwa lengo la kuwashawishi wawekezaji.


Asema hatua hiyo itasaidia kuvutia uwekezaji na kukuza mapato
Dar es Salaam.Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amesema, Serikali za Mitaa zikiweza kujisimamia na kutoa maeneo kwa ajili ya uwekezaji, zinaweza kupiga hatua za kiuchumi.

Pia amezishauri  serikali hizo kuonyesha fursa zilizopo katika uwekezaji  kwa lengo la kuwashawishi wawekezaji.

Pinda aliyasema hayo jana wakati akifungua mkutano wa siku mbili wa  Ushirikiano wa Serikali za Mitaa kati ya Tanzania na China.

Mkutano huo unawashirikisha wafanyabiashara kutoka China na Tanzania, magavana na mameya, makuu wa mikoa, wakurugenzi wa halmashauri za mikoa na wakuu wa wilaya. 
Akifungua  mkutano huo Waziri Pinda alisema; “Tumieni mkutano huu vizuri na wenzetu wa China kuwaeleza fursa mlizonazo katika halmashauri zenu, kama mtazielezea mtawavutia kuja kuwekeza,” alisema na kuongeza;

Jifunzeni kutoka kwao, wao wamepigaje hatua kwao ili na sisi hapa tufanye hivyo kwa lengo la kuzifanya halmashauri zetu kuweza kukusanya mapato zaidi na hata kujiongoza zenyewe.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Lindi , Dk Nasoro Hamidi, alisema kama Serikali itapanua sekta ya viwanda nchini, itasaidia kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa.
Pia alipendekeza kuboreshwa kwa mazingira ya mfumo wa sekta ya elimu ili kusaidia idadi kubwa ya vijana kujiajiri.

“Kama mtu ataelimishwa kila kitu kitakwenda sawa hivyo tunapowekeza tunahakikisha na elimu inawafikia wananchi ambao wakielimishwa hakuna jambo litakaloshindikana,” lisema Dk Hamidi.
Meya wa Manispaa ya Bukoba, Dk Anatory Amani, alisema kama  kila mkoa  utapata wawekezaji katika  sekta ya kilimo na uvuvi, wananchi watapiga hatua katika maendeleo.

“Kilimo ni  sekta muhimu katika taifa maana asilimia kubwa ya wananchi wanategemea kilimo,” alisema

No comments :

Post a Comment