Thursday, December 20, 2012

Mifuko ya hifadhi ya Jamii yatahadharishwa


Na Dege Masoli: 16th December 2012
Mifuko  ya  hifadhi ya jamii  itakayoshindwa  kuwadhibiti  waajiri wanaokwepa  kuwasilisha  michango ya wafanyakazi wake italazimika kuwajibika kwa kubeba gharama za kulipa mafao yote ya kustaafu ya mwanachama huyo.

Hayo yalielezwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa  Hifadhi ya Jamii (SSRA), Irene Issaka  katika mahojiano na NIPASHE  baada ya kuzindua semina ya Jukwaa la Wahariri Tanzania iliyohusu majukumu ya SSRA katika kusimamia  Mifuko ya Hifadhi ya Jamii iliyofanyika jana hoteli ya Tanga Beach Resort jijini hapa.

Issaka alieleza kuwa moja ya majukumu ya  Mamlaka hiyo ni kuisimamia mifuko  hiyo ili iweze kuendesha shughuli zao kwa ufanisi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha haki ya mwanachama haipotei wala kucheleweshwa baada ya kustaafu kwake.

Alibainisha kuwa endapo mfuko wa hifadhi ya Jamii utashindwa kuwadhibiti waajiri wanaokwepa kulipa ama kuwasilisha michango ya mtumishi wake kama inavyompasa kufanya hadi anastaafu mfuko husika utawajibika  kwa kulipa mafao yake.

“Maana yetu ni nini, tunataka mifuko iwajibike kukusanya michango ya wanachama wao, pamoja na kuhakikisha michango ya pande zote za miajiri na mtumishi  inawasilishwa…habari ya tumepokea ya mwanachama bado ua mwajiri sasa haipo, ikitokea mfuko utabeba jukumu hilo,” alisema Issaka.

Hata hivyo Mkurugenzi huyo alihimiza suala la mifuko hiyo kuendesha taratibu za uwekezaji kwa mujibu wa miongozo ikiwa ni pamoja na kuwa na sera, mikakati na mpango wa kazi na kwamba Mamlaka hiyo chini ya kifungu cha tano cha sheria ya mwaka 20012 imepewa uwezo wa kuchukua hatua kwa mifuko na mwajiri atakaekwenda kinyume.

Akizungumzia  majukumu ya Mamlaka hiyo, Issaka alisema kuwa ni pamoja na kufanya tathimini ya mifuko, kuchukua hatua za kinidhamu pale inapobidi, kufanya kaguzi mbalimbali na kuelekeza wajibu mwingine wowote utakaohakikisha sekta ya hifadhi ya jamii inafanyakazi kwa ufanisi na uongozi bora.

No comments :

Post a Comment