Tuesday, May 29, 2012

Wanachama waitaka NSSF ianzishe benki

11th March 2012
Chapa
Maoni
Baadhi ya Wanachama wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) wameuomba mfuko huo kuanzisha benki ambayo itatumika kuwakopesha wanachama wake fedha za kuendeshea miradi mbalimbali ili waweze kujikwamua kiuchumi kwa kutumia dhamana ya akiba zao ndani ya mfuko huo.
Ombi hilo lilitolewa jana na walimu wa Shule za sekondari zinazomilikiwa na Jumuiya ya Wazazi Tanzania zilizopo mkoani Mbeya wakati wa semina ya mafunzo iliyoandaliwa na NSSF mkoani hapa.
Wakichangia maoni yao katika semina hiyo, baadhi ya walimu hao walisema kutokana na umri wa kuishi wa watanzania pungua, wanachama wengi wa mfuko huo hawafikii hatua ya kustaafu na kulipwa mafao yao, hali ambayo inasababisha amana zao ndani ya mfuko kuliwa na watu wengine wasiostahili.
“Ikiwa kwa sasa mfuko wa NSSF una wanachama zaidi ya 500, ambao wanachangia kila mwezi, kwa nini isiwe benki badala ya shirika la umma ili benki hiyo itumike kuwakopesha wanachama wake kwa dhamana za akiba zao?” alihoji mmoja wa walimu hao ambaye hakutaja jina lake.
Mwalimu huyo alisema kwa sasa kati ya wanachama mia moja wa NSSF, wale wanaofikia umri wa kustaafu na kulipwa mafao yao hawafiki 10, akidai kuwa umri wa kuishi kwa watanzania umepungua na ndio sababu anapendekeza kuwa NSSF ingefungua benki ambayo ingewakopesha wanachama wake ili na wao waweze kufaidi fedha zao wangali hai.
Akijibu hoja hiyo Meneja wa NSSF Mkoa wa Mbeya, Hamis Fakii, alisema suala la NSSF kufungua benki haliwezekani kwa kuwa kila taasisi ina majukumu yake.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments :

Post a Comment