Sunday, March 22, 2026

Kiwanda cha Chai Mponde kimeingiza Sh.bilioni 6.3 kwenye mzunguko wa fedha


‎Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu

Picha: Mpigapicha Wetu 
Precious Metals
‎Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sang
By Mwandishi Wetu Nipashe Jumapili

Kiasi cha Shilingi bilioni 6.3 zimeingia katika mzunguko wa fedha kutokana na uwekezaji wa Kiwanda cha  Chai Mponde kilichoko Bumbuli, Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga.

 ‎Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, amewaambia wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamaii iliyotembelea kiwanda hicho kinachomilikiwa kwa ubia na Mfuko wa Hifadhi ya Jamaii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Machi 14, 2026.
 ‎
 ‎Akifafanua Sangu alisema, wakulima wa majani mabichi ya  chai kutoka wilaya za Lushoto na Korogwe tayari wamepata Shilingi bilioni 3.8 huku Shilingi milioni 431.46 zikiwanufaisha wakulima wa miti, ulipaji misharaha kwa wafanyakazi Shilingi bilioni 1.40, wasafirishaji wa chai Shilingi milioni 319.46, malipo ya kodi na tozo mbalimbali kwa Halmashauri Shilingi milioni 301.2 na huduma za kijamii (CSR) Shilingi milioni 1.62.
 ‎ ‎
 ‎“Wakulima wanaozunguka eneo hili hawana mahala popote pa kuuzia chai yao isipokuwa hapa, viwanda vyote vilivyokuwepo katika eneo hili vilifungwa na ndio maana serikali tukaona tufufue kiwanda hiki, ili kuwawezesha wanachi kupata sehemu ya kuuza chai yao, kiwanda hiki kina manufaa makubwa kwa wakulima hawa.” alisema Sangu.
 ‎ ‎
 ‎Alisema, jumla ya wakulima 3,500 wanauza majani mabichi ya chai kwenye kiwanda hicho, huku kiwanda kikitoa ajira za kudumu 79 na ajira za msimu 100-300 kutegemea na msimu wa mavuno.
 ‎
 ‎Kwa upande wao wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, wamepongeza mafanikio yaliyopatikana tangu kiwanda kilipoanza uzalishaji Oktoba 2022 hadi sasa.
 ‎
 ‎ ‎“Ukiangalia huu mnyororo wa thamani utaona kabisa manufaa yanayotokana na uwepo wa kiwanda hiki ni makubwa,” alisema mjumbe wa kamati Katani A Katakani.
 ‎
 ‎ ‎Aidha, wajumbe hao wametoa ushauri wa maboresho ya miundombinu ya barabara kuelekea kwenye kiwanda hicho ili kuwarahisishia wakulima kusafirisha chai yao kwenda kiwandani kwa urahisi.
 ‎
 ‎ ‎Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Mhe. Hawa Mchafu alisema, Kamati inatamani kuona kiwanda kinaendelea kustawi na hivyo kuleta manufaa kwa wakulima.
 ‎
 ‎“Tunatamani wakati mwingine tutakapotembelea tuone kuna maendeleo makubwa zaidi ya haya tuliyoyaona leo, tunawapongeza sana wakuu wa mifuko hii ya hifadhi ya Jamii PSSSF na WCF na sisi tuko bega kwa bega na ninyi. ” alisema Mchafu.
 ‎
 ‎ ‎Aidha amewahamasisha vijana katika eleo hilo kushiriki kwa wingi katika kilimo cha chai ili kuongeza vipato na kuboresha maisha yao.
 ‎
 ‎“Mhe,DC (Mkuu wa Wilaya) tunaomba uwahamasishe vijana washiriki katika kilimo na wasiwaachie wazee peke yao.” alisema.

No comments :

Post a Comment