
By Christina Mwakangale , Nipashe Jumapili
Mlango wa Hormuz ni njia nyembamba ya bahari inayounganisha Ghuba ya Uajemi (Persian Gulf) na Ghuba ya Oman, kisha kuelekea Bahari ya Arabia/Indian Ocean.
Ni moja ya njia muhimu sana duniani kwausafirishaji wa mafuta na gesi.
Njia hii ni kuu ya mafuta na LNG duniani. Zaidi ya asilimia 20 ya mafuta na gesi asilia ya kimiminika (LNG) duniani hupita hapa. Hii inaifanya kuwa sehemu nyeti sana kwa uchumi wa dunia.
Ndiyo njia pekee ya kutoka Persian Gulf kwenda bahari ya wazi. Nchi kama Iraq, Kuwait, Qatar, UAE, na Iran hutegemea njia hii kupeleka mafuta yao nje.
Nchi nyingi za Asia hutegemea sana njia hii. Mafuta mengi yanayopita Hormuz huenda China, India, Japan na Korea Kusini, hivyo usalama wake unaathiri sana soko la nishati duniani.
Njia hii ikifungwa au kuvurugwa, bei za mafuta hupanda haraka.
Migogoro au mashambulizi kwenye eneo hili yanaweza kusababisha uhaba wa mafuta, kupanda kwa bei, na kuathiri biashara ya kimataifa.
Reuters imeripoti pia kuwa wakati wa mvutano mkubwa, meli nyingi zilisimama au kuchelewa kupita.
Ni eneo la kimkakati na nyeti kijeshi. Iko kati ya Iran (kaskazini) na Oman (kusini, hasa eneo la Musandam). Njia za meli ziko hasa kwenye maji ya Oman lakini sehemu pia hupitia karibu na Iran, na zinalindwa chini ya sheria za kimataifa za bahari.
Hormuz ni “mlango wa nishati wa dunia.” Ikiwa kuna shida hapo, dunia nzima huhisi athari hasa kwenye bei ya mafuta, usafirishaji, na uchumi wa kimataifa.
Njia hii iliyoko ukanda wa nchi za Ghuba, ni muhimu zaidi.
UMUHIMU WA UKANDA WA GHUBA DUNIANI
Mataifa ya Ghuba, humaanisha nchi zinazozunguka Ghuba ya Uajemi (Arabian/Persian Gulf), ambazo nyingi ni wanachama wa Gulf Cooperation Council (GCC).
Nchi hizo za Ghuba ni sita, Saudi Arabia, United Arab Emirates (UAE), Qatar, Kuwait, Oman na Bahrain.
Umuhimu wa mataifa hayo kwa dunia, ni hasa katika bidhaa muhimu nishati. Hapo kuna mafuta ikiwamo petrol na dizeli pamoja na gesi, ambayo matumizi yake yameshika kasi duniani.
Uchumi wa nchi wanachama wa GCC unaendelea kukua, na inakadiriwa ukuaji wa takribani asilimia 4.4 mwaka 2026, unaozidi wastani wa ukuaji wa uchumi wa dunia. Ukuaji huo unachangiwa na uzalishaji wa mafuta na ukuaji wa sekta zisizo za mafuta, kwa mujibu wa Get EnterpriseAMdaily.
UAE, inatarajiwa kukua kwa karibu asilimia tano mwaka 2026 kutokana na nguvu ya sekta zisizo za mafuta kama huduma, biashara na teknolojia, kwa mujibu wa Gulftoday.
Yamejiwekea malengo hasa kupunguza utegemezi wa mafuta, kwa kuja na mipango ya mabadiliko ya uchumi kama ‘Saudi Vision 2030’.
Pia, eneo hilo lina ujenzi wa miji yenye majengo ya kisasa, miradi mikubwa ya utalii na biashara.
ENEO LA AKIBA KUU MAFUTA
Kwa ujumla jambo la kwanza, mataifa hayo yanamiliki sehemu kubwa ya akiba ya mafuta na gesi asilia duniani. Yanapoguswa kwa muda mfupi uchumi wa dunia huathirika mara moja.
Huathiri bei ya mafuta kimataifa, hivyo kuathiri uchumi wa dunia. Vita ambayo ina takribani wiki sasa tangu Marekani pamoja na Israel, kufanya mashambulizi huko Iran, na kuua takribani viongozi wakuu wa kitaifa wanane na mamia ya raia, Mataifa ya Ghuba yameathiriwa.
Kikosi cha Msalaba Mwekundu cha Iran (Iranian Red Crescent Society), kinasema idadi ya watu waliofariki imefikia takriban 787 tangu mashambulizi hayo yalipoanza.
Pia Shirika la Haki za Binadamu linaloongozwa na Watu wa Marekani (Human Rights Activists in Iran–HRANA) linaripoti kuwa kati ya waliofariki, takriban 742 ni raia, wakiwamo 176 watoto.
Mataifa hayo kila mmoja sasa anajihami dhidi ya mashambulizi, ingawa tayari baadhi yameshaguswa, kama vile UAE, maeneo yenye hoteli, viwanja vya ndege yalishambuliwa na Iran, kwa mujibu wa vyombio vya habari kimataifa.
BIASHARA NA USAFIRISHAJI
Pili, Mataifa ya Ghuba, ni eneo ambalo liko kwenye njia muhimu ya bahari hasa ‘Hormuz Strait’.
Hormuz Strait, ni eneo la mlango wa bahari ambayo ni njia nyembamba ya maji inayounganisha Ghuba ya Uajemi (Persian Gulf) na Bahari ya Oman (Gulf of Oman), ambayo inaelekea hadi Bahari ya Hindi.
Eneo hilo liko kati ya Iran (kaskazini), Oman na United Arab Emirates (kusini). Eneo hilo ni miongoni mwa njia muhimu zaidi za usafirishaji wa mafuta duniani.
Na kwa kiwango kikubwa ya mafuta ya kimataifa hupita hapo na mzigo wa meli kila siku. Migogoro yoyote katika eneo hilo, inaweza kuathiri bei ya mafuta duniani. Hiki ndicho kinaanza kushuhudiwa sasa.
Bandari na viwanja vya ndege vya kimataifa vinaunganisha Asia, Ulaya na Afrika.
MIFUKO IMARA UWEKEZAJI
Tatu, Mataifa ya Ghuba, ni muhimu kwenye uwekezaji wa kimataifa, yakiwa na ‘Sovereign Wealth Funds (SWFs)’ kubwa zinazowekeza duniani kote hasa katika teknolojia, miundombinu, michezo, benki na kwingineko.
Sovereign Wealth Funds (SWFs), ni mifuko ya uwekezaji inayomilikiwa na serikali. Serikali huweka akiba ya fedha, mara nyingi kutokana na mafuta, gesi, au ziada ya biashara.
Pia, huziwekeza duniani ili kuzalisha faida na kulinda uchumi wa taifa kwa muda mrefu. Mataifa ya Ghuba na SWFs, baadhi yana mifuko mikubwa zaidi duniani, kama vile Abu Dhabi Investment Authority (UAE); Public Investment Fund (Saudi Arabia); Qatar Investment Authority–(Qatar); Kuwait Investment Authority (Kuwait).
Baadhi yake yana thamani ya mamia ya mabilioni hadi trilioni za dola. Mataifa ya Ghuba, huchangia maendeleo ya miradi mikubwa barani Ulaya, Asia, Afrika na Marekani, yana ushawishi wa kisiasa kupitia uwekezaji wao.
Pia wamo katika uwekezaji katika AI (akili unde), fintech na ‘smart cities’. Mfano, United Arab Emirates (UAE), imeanzisha Wizara Maalum ya AI na ina mkakati wa Taifa wa AI.
Na kwa kutumia teknolojia ya fintech, Mataifa ya Ghuba yanataka kuwa vituo vya kifedha vinavyoshindana na miji kama London au New York.
Wanapanga wawe na malipo kwa simu (digital payments), benki za mtandaoni (online banking), mikopo ya kidijitali, sarafu za kidijitali (digital currencies), yote hayo kupunguza matumizi ya pesa taslimu, kuvutia wawekezaji wa kimataifa na kufanya biashara iwe rahisi na ya haraka.
Pia wamewekeza kwenye michezo na utalii, kwa kuandaa mashindano makubwa ya kimataifa, kuvutia watalii na wawekezaji.
Mradi wa ‘Smart City’ ni kuwa na miji safi kwa kutumia teknolojia kusimamia huduma kama, umeme, maji, usafiri na usalama, kudhiti taka.
SIASA, DIPLOMASIA
Jambo la nne, umuhimu wa Mataifa ya Ghuba, ni kwenye siasa na diplomasia, kutokana na ushawishi wake mkubwa katika zaidi Mashariki ya Kati.
Mataifa hayo pia hushiriki katika upatanishi wa migogoro na ushirikiano wa kiusalama.
AJIRA NA UHAMIAJI
Syala muhimu la tano kwa nchi za Ghuba ni hasa kwenye eneo la ajira, uhamiaji wakipokea wengi kutoka mataifa mbalimbali.
Mamilioni ya wafanyakazi kutoka Asia na Afrika, hufanya kazi huko na hutuma fedha (remittances) nyumbani.
ATHARI
Kukosekana kwa utulivu katika eno zima la Mashariki ya Kati, kumeanza kuathiri uchumi wa dunia.
Tehran imetuhumiwa kushambulia meli katika Ghuba, jambo lililosababisha kufungwa kwa njia muhimu ya bahari ya ‘Strait of Hormuz’, inayopitisha takriban asilimia 20 ya usambazaji wa mafuta na gesi duniani.
Mashambulizi pia yameripotiwa katika vituo vikubwa vya mafuta na gesi, ikiwemo bandari ya kibiashara ya Duqm nchini Oman na kituo cha Fujairah nchini Falme za Kiarabu (UAE).
Mashambulizi hayo yamesababisha baadhi ya wazalishaji wakubwa wa mafuta na gesi duniani kusimamisha uzalishaji, wakiwamo vituo vya gesi asilia iliyoyeyushwa (LNG) vya Qatar na kiwanda kikubwa zaidi cha kusafisha mafuta cha ndani nchini Saudi Arabia.
Bei za mafuta na gesi zimepanda kwa kasi, huku bei ya mafuta ghafi aina ya Brent ikifikia dola 85 (pauni 64) kwa pipa, kwa mara ya kwanza tangu Julai 2024.
*HABARI HII INA VYANZO TOFAUTI KIMATAIFA
No comments :
Post a Comment