SAKATA la kikokotoo cha mafao kwa wastaafu, limeibuka tena bungeni huku Mbunge wa Viti Maalum, Ester Bulaya, akisema bado ni janga.
Kutokana na hali hiyo, ameiomba serikali kukaa meza moja na wadau ili kujadili namna bora ya kuwapa mafao yao kutoka asilimia 33 iliyopo sasa hadi 50 kwa mafao ya mkupuo.
Akichangia jana Taarifa ya Mapitio ya Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa mwaka 2023/2024 na Mwelekeo wa Kazi zake kwa mwaka 2024/25 bungeni, jijini hapa, Bulaya alisema: “Sote tunajua kikokotoo bado ni janga na hii haijaisha mpaka iishe kwani bado kuna manung’uniko kwa watumishi. Nikiwaonyesha meseji zangu kutoka kwa walimu, maaskari, madaktari na wengine ni shida. Mtu anastaafu anapewa Sh. milioni 17 hajajenga.
“Inajulikana kuwa watumishi hao wanafanya kazi kwenye mazingira yapi, hivyo kuteleza siyo kuanguka. Turudi tukae tuwasikilize kwani hiyo fedha ni yao, serikali inaweka. Wapeni mafao kwa mkupuo wa asilimia 50, hizo zingine muwape kidogo kidogo.”
Alisema fedha za mafao ya mkupuo ndizo zinazowasaidia wala si hizo za kila mwezi kwa kuwa wakishaweka misingi kupitia fedha hizo, mambo mengine yatakwenda kama kawaida. Alisema madhara hayo yanasabashwa na kupitishwa kwa sheria hiyo kwa lazima.
“Leo mifuko yetu ina shida lakini mimi nazungumzia mfuko mmoja tu hapa wa wawatumishi wa serikali (PSSSF) kwani Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii inatakiwa iwe japo asilimia 40. Kwa nini ripoti ya CAG (Mdhibniti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali) ionyeshe kila mwaka uko asilimia 20?,” alihoji.
Alidai kuwa serikali inachukua fedha kwenye mfuko na kuenda kuwekeza lakini hailipi, akitolea mfano wa mwaka 2020/21 alisema serikali ililipa kwa ‘non cash bond’ zaidi ya Sh. trilioni 2.1 na kuahidi kuwa mwaka unaofuata ingelipa Sh. trilioni 2.4 ambayo hadi sasa haijalipwa.
“Sasa hii mifuko itawezaje kuwa ‘stable’ (imara)? Nikianza kwa takwimu za Juni, 2020 tunaona michango ya wanachama kwenye mfuko ilikuwa Sh. bilioni 1.364 na mahitaji ya mafao yalikuwa Sh. bilioni 1.554. nyongeza waliyochukua kwenye vyanzo vingine ilikuwa Sh. milioni 190,” alisema.
Pia alisema kwa mwaka jana, michango ya wanachama kwenye mfuko ilikuwa Sh. bilioni 1.526 wakati mahitaji ya mafao yalikuwa Sh. bilioni 1.567 nyongeza waliyochukua kwenye vyanzo vingine ilikuwa Sh. milioni 171.
Kwa mwaka huo, alisema uwekezaji ulikuwa Sh. milioni 587 na kwamba mfuko huo kuwa ndio unaotegemewa na watumishi Pamoja na serikali ambayo inakopa kuwekeza katika maeneo mbalimbali lakini inapata hasara katika uwekezaji husika.
Mbunge wa Sumve (CCM), Kasalali Mageni, alisema suala la kikokotoo lina hoja kutokana na madai kuwa watumishi wa serikali wana uwezo mdogo wa matumizi na utunzaji fedha, hivyo wakipewa fedha hawatazitumia vizuri, hivyo serikali iwatunzie na kuwapatia kidogo kidogo.
“Naomba tujadiliane suala hili kwa kuwa hawa watumishi ndio leo wako kwenye ofisi, wametuletea makabrasha yote tunayojadili bajeti hii na wamepanga kila kitu. Wanalinda na kufanya shughuli zote muhimu nchini. Lakini wakija kustaafu licha ya uzoefu wao wote, eti wakishazeeka tunaona hawawezi kutunza fedha zao wenyewe. Hili si jambo jema,” alisisitiza
Alisema licha ya serikali kuliona jambo hilo ni zuri, mitaani bado halijawaingia wahusika akilini na hawalielewi huku wale ambao wamelazimika kuingia kwenye kikokotoo, wengi wao limewachanganya wengine hadi kufariki dunia kwa mawazo.
Naye Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Janejelly James, aliiomba serikali kuongeza kasi ya kulipa maslahi ya wastaafu hususani walimu. Alisema katika kada hiyo kuna kilio kikubwa licha ya kutegemgewa zaidi katika kulijenga taifa kielimu.
“Hakuna Waziri ambaye hakufundishwa na walimu wala hakuna mbunge ambaye hakufundishwa na mwalimu. Malalamiko ni makubwa zaidi hata leo Waziri Jenesta (Mhagama- Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge) nikikuletea ujumbe niliopokea hapa uone wanavyolalamika zaidi,”alisema.
Alisisitiza pia juu ya umuhimu wa watumishi kufikishiwa elimu ya kikokotoo ipasavyo kwa kuwaambia faida na hasara zake kwa kuwa bado wako kwenye giza hawaelewi kile wanacholipwa ni nini na kwa nini.
No comments :
Post a Comment