Tuesday, March 14, 2023

TAARIFA KWA UMMA: BENKI KUU YA TANZANIA YAONGEZA MUDA WA USIMAMIZI WA YETU MICROFINANCE BANK PLC


Itakumbukwa  
kwamba, kwa mamlaka iliyopewa chini ya kifungu cha sheria namba 56(1) (g)(iii) cha Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006, Benki Kuu ya Tanzania iliamua kuchukua usimamizi wa Yetu Microfinance Bank Plc kuanzia tarehe 12 Disemba 2022 baada ya kubaini kuwa ilikuwa na upungufu mkubwa wa ukwasi na mtaji kinyume na matakwa ya sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006 na kanuni zake.

Baada ya kuchukua usimamizi wa benki hii, Benki Kuu ya Tanzania ilisitisha shughuli za utoaji wa huduma za kibenki za Yetu Microfinance Bank Plc kwa muda wa siku tisini ili kuipa nafasi Benki Kuu ya Tanzania kutathmini hatua za kuchukua ili kupata ufumbuzi wa suala hili. Benki Kuu ya Tanzania inapenda kuuarifu umma kuwa mchakato wa kutathmini hatua za kuchukua ili kupata ufumbuzi wa matatizo ya Yetu Microfinanc Bank Plc haujakamilika hivyo muda wa usimamizi umeongezwa kwa kipindi cha siku thelathini (30) kuanzia tarehe 12 Machi 2023.

Benki Kuu ya Tanzania inauhakikishia umma kuwa itaendelea kulinda maslahi ya wenye amana katika mabenki kwa lengo la kuleta ustahimilivu katika sekta ya fedha.

GAVANA BENKI KUU YA TANZANIA

No comments :

Post a Comment