Afisa Programu Wizara ya Afya, Idara ya Afya ya Uzazi ,Mama na Mtoto, Jackline Ndanshau, akizungumza na watumishi kada ya Afya katika ufungaji wa kikao cha watalaam wa Afya Kanda ya Magharibi inayounda mikoa Tabora ,Katavi na Kigoma cha kujadili mikakati ya kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga.
Muuguzi Mbobezi Idara ya Huduma za Ukunga na Uuguzi ,Wizara ya Afya, Aziza Machenje.
Mganga mkuu mkoa wa Tabora Honoratha Faustine Rutatinisibwa , akizungumza na watumishi kada ya Afya katika ufungaji wa kikao cha watalaam wa Afya Kanda ya Magharibi inayounda mikoa Tabora ,Katavi na Kigoma cha kujadili mikakati ya kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga.
Takwimu za vifo vya watoto wachanga kuanzia siku 0-28 katika Kanda ya Magharibi kwa mwaka 2021 ni watoto wachanga 2,539 walipoteza maisha; ambapo Kigoma vilikuwa ni vifo 1,026, Tabora vifo 954, na Katavi vifo 559 kushindwa kupumua, watoto kuzaliwa njiti,uambukizi kwa watoto wachanga,na kuzaliwa na uzito pungufu.
Katika kiwango cha mimba za utotoni kanda ya Magharibi Mkoa wa Katavi ni 25.2%, Tabora 17% na Kigoma 11.9% na hudhurio la kwanza la wajawazito chini ya wiki kumi na mbili kwa mkoa wa Tabora ni 34.4%, Katavi 41% na Kigoma 54.9% na kiwango cha utumiaji wa njia za kisasa za uzazi wa mpango kwa mkoa wa Katavi ni 41%,Kigoma 46.4%,na Tabora ni 60.1%.
Na Faustine Gimu, Tabora
Rai imetolewa kwa watumishi sekta ya afya kanda ya Magharibi kufanya kazi kwa ufasaha na kwa kutumia lugha zenye staha katika kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga.
Rai hiyo imetolewa mkoani Tabora na Afisa Programu Wizara ya Afya,Idara ya Afya ya Uzazi ,Mama na Mtoto Jackline Ndanshau katika ufungaji wa kikao cha watalaam wa Afya Kanda ya Magharibi inayounda mikoa Tabora ,Katavi na Kigoma cha kujadili mikakati ya kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga katika kanda hiyo.
Ndanshau amesema ni muhimu watoa huduma za afya kuangalia mapema katika ufuatiliaji wa mama mjamzito na mtoto mchanga anapozaliwa katika kuepusha vifo .
“Wizara inategemea mipango kazi tuliojiwekea inakwenda kutekelezwa ,rai yangu kwa watumishi kanda ya magharibi ni kufanya kazi kwa ufasaha na kwa lugha zenye staha katika kuwavusha salama mama wajawazito na watoto wachanga”amesema Ndanshau.
Muuguzi Mbobezi Idara ya Huduma za Ukunga na Uuguzi ,Wizara ya Afya Aziza Machenje amehimiza kwa watumishi wa afya kubadilisha mwenendo na tabia katika kupunguza vifo vya mama na mtoto.
“Tujitahidi kufanya kazi kwa ueledi,tubadilishe tabia na mwenendo na kuwa na ujuzi wa kutosha katika kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga ,na imeonekana kwamba asilimia kubwa ya akina mama wanapoteza maisha kabla na baada ya kujifungua kwa kupoteza damu nyingi sana ikifuatia na kifafa cha mimba au kifafa cha uzazi ,hivyo rai yangu kwa viongozi tuweze kuwajibika kwa wale tunaowaongoza ili kuweza kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga”amesema.
Kwa upande wake Mganga mkuu mkoa wa Tabora Honoratha Faustine Rutatinisibwa amehimiza mpango kazi wa kupunguza vifo vya mama na mtoto kanda ya Magharibi unafika kila ngazi ya utekelezaji huku Mratibu wa Huduma za Uzazi na Mtoto mkoa wa Katavi Elida Machungwa akiahidi kuweka nguvu za pamoja katika utekelezaji wa mpango huo.
Ikumbukwe kuwa takwimu za vifo vya mama wajawazito kanda ya Magharibi zinabainisha kuwa , Mwaka 2019 akina mama wajawazito 210 walipoteza maisha; ambapo, Kigoma vilikuwa vifo 100, Tabora 62 na Katavi 48.
Mwaka 2020 akina mama 235 walipoteza Maisha; ambapo Kigoma vilikuwa vifo 119, Tabora 58 na Katavi 58, na Mwaka 2021 akina mama 174 walipoteza Maisha; ambapo Kigoma vilikuwa vifo 75, Tabora vifo 58 na Katavi vifo 41.
Sababu kubwa zilizosababisha vifo vya wajawazito ni pamoja na Kutokwa damu nyingi baada ya kujifungua,Kifafa cha mimba, Kupasuka mfuko wa Uzazi,Kutokwa na damu nyingi kabla ya kujifungua, Upungufu mkubwa wa damu,Uambukizo wakati na baada ya kujifungua huku hali ya vifo Mwaka 2020 vitokanavyo na uzazi kitaifa vilikuwa 1,640 na Mwaka 2021 vilikuwa 1,588.
Takwimu za vifo vya watoto wachanga kuanzia siku 0-28 katika Kanda ya Magharibi kwa mwaka 2021 ni watoto wachanga 2,539 walipoteza maisha; ambapo Kigoma vilikuwa ni vifo 1,026, Tabora vifo 954, na Katavi vifo 559 kushindwa kupumua, watoto kuzaliwa njiti,uambukizi kwa watoto wachanga,na kuzaliwa na uzito pungufu.
Katika kiwango cha mimba za utotoni kanda ya Magharibi Mkoa wa Katavi ni 25.2%, Tabora 17% na Kigoma 11.9% na hudhurio la kwanza la wajawazito chini ya wiki kumi na mbili kwa mkoa wa Tabora ni 34.4%, Katavi 41% na Kigoma 54.9% na kiwango cha utumiaji wa njia za kisasa za uzazi wa mpango kwa mkoa wa Katavi ni 41%,Kigoma 46.4%,na Tabora ni 60.1%.
No comments :
Post a Comment