Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanikisha ushiriki wa Wajasiriamali zaidi ya 300 katika maonesho ya 22 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Wajasiriamali Wadogo na Wakati maarufu Juakali yanayofanyika katika viwanja vya Uhuru vya Kololo jijini Kampala, Uganda kuanzia terehe 8 - 18 Disemba 2022
Maonesho hayo yanayongozwa na kauli mbiu “Nunua Bidhaa za Afrika Mashariki, ili kujenga Uchumi Stahimilivu na Endelevu wa Afrika Mashariki” yanalenga kutoa fursa kwa Wajasiriamali ya kuonesha huduma na bidhaa mbalimbali wanazozalisha na kubadilishana uzoefu, ujuzi na taarifa na wajasiriamali wenzao katika Jumuiya, sambamba na kukuza wigo wa masoko mapya.
Maonesho hayo ambayo yamevutia Wajasiriamali zaidi 1500 kutoka Nchi zote saba (7) Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, na ikikadiriwa 75% kati yao kuwa ni wanawake, yamesheheni bidhaa mbalimbali zenye asili ya Jumuiya. Kwa upande wa wajisiliamali wa Tanzania miongoni mwa bidhaa na huduma wanazozionesha ni pamoja na mavazi ya asili, bidhaa za baharini, bidhaa za kilimo zilizoongezewa thamani, mashine za kuzalisha bidhaa mbalimbali, madawa ya asili, vito vya thamani na madini, utalii, na bidhaa za ngozi kama vile viatu, mabegi na mikoba
Wakizungumza kwa nyakati tofauti Wajasiliamali wa Tanzania wameonesha kuridhishwa kwao na kupongeza juhudi na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania chini ya Uongozi madhubuti wa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuweka mazingira wezeshi ya biashara ikiwa ni pamoja na kuwawezesha kushiriki katika maonesho hayo.
“Kutokana na gharama kubwa za kusafirisha bidhaa zetu hadi hapa nchini Uganda, wengi wetu tusingeweza kumudu, hivyo tusingeweza kuwa na uwakilishi wa kutosha katika maonesho haya. Hata hivyo kutokana na dhamira ya Serikali ya kutusaidia wajasiriamali kukua kibiashara kupitia kupata masoko mapya ya huduma na bidhaa tunazozalisha na kutuongezea ujuzi na uzoefu imeona ni vyema ituwezeshe katika maeneo mbalimbali ikiwemo kugharamia usafiri wa kutuleta hapa nchini Uganda na kuturudisha nyumbani baada ya maonesho”. Ameeleza Lilian Sambu mjasiliamali.
No comments :
Post a Comment