Monday, November 28, 2022

TUWAJIBIKE KWA PAMOJA KWA MASLAHI YA TAIFA - MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI




Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi akizungumza na Wakurugenzi na Wakuu wa Vitengo (hawapo pichani) kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mashtaka Taifa na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali katika kikao cha pamoja kuhusu majukumu ya Ofisi hizo kilichofanyika jijini Mwanza.


Mkurugenzi wa Mashtaka, Sylvester Mwakitalu akitoa salamu kwa wajumbe wa menejimenti (hawapo pichani) za Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mashtaka ya Taifa na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali katika kikao cha pamoja kuhusu majukumu ya Ofisi hizo kilichofanyika jijini Mwanza.
Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende akiongea na Wakurugenzi na Wakuu wa Vitengo (hawapo pichani) kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mashtaka ya Taifa na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali katika kikao cha pamoja cha kuhusu majukumu ya Ofisi hizo kilichofanyika jijini Mwanza.



Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Sarah Mwaipopo akiongea na Wakurugenzi na Wakuu wa Vitengo (hawapo pichani) kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mashtaka ya Taifa na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali katika kikao cha pamoja cha kuhusu majukumu ya Ofisi hizo kilichofanyika jijini Mwanza.
Baadhi ya Wakurugenzi wakimsikiliza Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi (hayupo pichani) wakati wa kikao cha pamoja cha menejimenti ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mashtaka ya Taifa na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kilichofanyika jijini Mwanza

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi (aliyeketi katikati) akiwa na Mkurugenzi wa Mashtaka, Sylvester Mwakitalu (kushoto), Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende (kushoto) katika picha ya pamoja na baadhi ya Wakurugenzi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali mara baada ya kufungua kikao cha pamoja kilichofanyika jijini Mwanza.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi (aliyeketi katikati) akiwa na Mkurugenzi wa Mashtaka, Sylvester Mwakitalu (kushoto), Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende (kushoto) katika picha ya pamoja na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Evaristo Longopa (wa kwanza kushoto), Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka, Joseph Pande (wa pili kushoto), Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Sarah Mwaipopo (wa pili kulia) na Mwandishi Mkuu wa Sheria (CPD) Onorius Njole (wa kwanza kulia) mara baada ya kufungua kikao cha pamoja kilichofanyika jijini Mwanza.

Na Mwandishi Wetu, OWMS-Mwanza


Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi amezitaka menejimenti za Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mashtaka ya Taifa, Wakili Mkuu wa Serikali na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwa na uwajibikaji wa pamoja kwa kutumia uzoefu na ujuzi wa kila taasisi ili kuongeza thamani na kupata matokeo makubwa kwa maslahi ya Taifa.

Mhe. Dkt. Feleshi ameyasema hayo leo kwenye kikao cha pamoja cha Ofisi hizo kilichofanyika kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mwanza na kuwataka kusimamia uwajibikaji wa pamoja bila kuathiri nani yupo wapi kwa kuwa wote ni familia moja na wanatekeleza majukumu kwa niaba ya Serikali.

“Sisi Wakurugenzi wa Idara mama za Ofisi hizi tatu tunatakiwa kuhakikisha kuwa idara na vitengo vingine saidizi zinafahamu majukumu yetu ili tuwe na uwajibikaji wa pamoja na kutumia uzoefu kwa kujengeana uwezo ili tuweze kupata matokeo makubwa na kuruka vihunzi na vikwazo mbalimbali kwenye taasisi zetu kw amaslahi mapana ya taifa”, amesema Mhe. Dkt. Feleshi.

Amesema kuwa kikao hiki ni tukio la kihistoria kwa kuwa yapata miaka 3 kwa ofisi hizi kuwa na kikao cha pamoja na sisi binadamu tunaishi kwa kujisahihisha ili tuwe na uelewa wa pamoja wa masuala yanayohusu muelekeo, maendeleo na maslahi ya Ofisi hizi na amevutiwa na namna masuala ya sheria yanavyobadilika kila siku na kuona umuhimu wa kutoa mafunzo ya kuendelea kuwajengea uwezo watumishi kwa kuwa Ofisi hizi ni kisima na chemuchemu ya mafunzo kwa Wakili wa Serikali.

“Sisi ni familia moja tumekutana kama familia tuongee masuala yanayotuhusu kwa mujibu wa majukumu ya msingi ya Ofisi hizi kwa hiyo tujenge uwezo wenye umahiri wa kutumikia taifa hili kwa niaba ya Serikali na wananchi kwa ujumla
Naye Mkurugenzi wa Mashtaka, ndugu Slyvester Mwakitalu amesema kuwa Ofisi hizi tatu ni muhimu sana kwa haki, amani na maendeleo ya taifa letu na Ofisi hizi zikilegea na kuwa na watumishi ambao hawatimizi wajibu wao taifa litapata madhara makubwa na kuwaumiza watanzania.

Ndugu Mwakitalu amesema kuwa Mawakili wa Serikali wasipokuwa na weledi na utaalamu wa kutosha watakuwa na mchango mdogo katika utekelezaji wa majukumu hivyo mafunzo ni muhimu ili kuwa na Mawakili wabobezi hasa kwenye maeneo ambayo tumekuwa tukifanya kazi zetu.

“Ninaamini kuwa tukiwa na vikao hivi mara kwa mara na tukajadili na kupeana majukumu ya kufikisha mwisho haya tunayojadili yatapunguza changamoto zilizopo na kufikiri namna ya kuzitatua ili kupata muafaka wa kila jambo”. Mwakitalu

Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende aamesema kuwa Ofisi hizi zimekasimiwa majukumu makubwa ya kusimamia Sekta ya Sheria na utoaji haki hapa nchini hivyo ni muhimu kuelewa majukumu yetu na kutambua mafunzo yanayotakiwa katika kutekeleza majukumu yetu.

“Taifa hili lipo mabegani mwetu tumelibeba, tunalo jukumu zito linalohitaji kuwa na mifumo mbalimbali ya utekelezaji wa majukumu yetu. Miaka 60 hii ya Uhuru wetu ni vizuri kuelewa nafasi yetu katika majukumu haya tuliyopewa na tunahitaji ushirikiano ambao utatuwezesha kutekeleza majukumu haya kwa ufanisi,” amesema Dkt. Luhende.

Amesema kuwa ni vema kwa Ofisi hizi tatu kuwa na maono ya mbali zaidi ya kwa kufahamu mifumo, kutambua watumishi, aina ya mafunzo, ubobezi unaohitajika kwa Mawakili na utaratibu wa kutoa motisha kwa baadhi ya watumishi wanaotekeleza vizuri majukumu yao ili kuwapa ari ya kuendelea kufanya vizuri zaidi.

Naye Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Sarah Mwaipopo amempongeza Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuwakutanisha wajumbe wa menejimenti wa taasisi hizo na kuwakumbusha kuendeleza umoja wao katika kutekeleza majukumu na chochote kinachotakiwa kufanyika kinapaswa kufanyika kwa pamoja.

Mwaipopo amesema kuwa ni muhimu kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kujenga taswira ya taasisi zetu na kujitafsiri tukijenga na kusomeka vema kwa wadau wetu na tukabaini changamoto na namna ya kuzingatia maadili.

“Ni fursa kubwa sana ambayo leo tunatakiwa tuitendee haki kwa sisi wajumbe wa menejimenti wa hizi Ofisi tatu kwa kuwa na kikao cha pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye ana ndoto ya kuhakikisha Mawakili wa Serikali wanatekeleza majukumu yao ipasavyo na Ofisi hizi zinashirikiana kwa pamoja kusukuma mambo ya taasisi hizi tatu”, amesema Mwaipopo.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Wakuu wa Idara na Vitengo wa Ofisi hizo na wjumbe hao wamedhamiria kuwa na muendelezo wa vikao vya namna hiyo ambavyo vitafanyika angalau mara tatu au nne kwa mwaka ili kutathmini mwenendo wa ushirikiano katika kufanikisha utekelezaji wa majukumu.

No comments :

Post a Comment