Wednesday, September 28, 2022

Watu 791 Wafanyiwa Uchunguzi Na Matibabu Kambi Maalum Ya Matibabu Ya Moyo Inayofanyika Mkoani Arusha

2 Mkuu  wa idara ya utafiti na mafunzo ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Peter Kisenge akimpima kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography) mwananchi aliyefika Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo. Wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa ALMC wanafanya kambi maalum ya siku tano ya matibabu ya magonjwa ya moyo kwa wakazi wa  mkoa wa Arusha na mikoa Jirani.

Mkuu  wa kitengo cha  utafiti kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Pedro Pallangyo akiangalia dawa za moyo anazotumia mwananchi  aliyefika Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo. Wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa ALMC wanafanya kambi maalum ya siku tano ya matibabu ya magonjwa ya moyo kwa wakazi wa mkoa wa Arusha na mikoa Jirani.

Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Mohamed Aloyce akizungumza na mwananchi  aliyefika Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo. Wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa ALMC wanafanya kambi maalum ya siku tano ya matibabu ya magonjwa ya moyo kwa wakazi wa mkoa wa Arusha na mikoa Jirani

 Na Mwandishi maalum – Arusha .

Watu 791 wamefanyiwa uchunguzi na kupata matibabu katika kambi maalum ya matibabu ya moyo inayofanyika katika hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) ambapo wengi wao wamekutwa na matatizo mbalimbali ya moyo huku asilimia 25 wakiwa na tatizo la shinikizo la juu la damu.
Kambi hiyo ya siku tano iliyoanza tarehe 26 na itamalizika tarehe 30 mwezi huu inafanywa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Arusha Lutheran Medica Centre.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Arusha mkuu wa idara ya utafiti na mafunzo ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Peter Kisenge alisema kufanyika kwa kambi hiyo ya matibabu ni mojawapo ya maadhimisho ya siku ya moyo duniani itakayofanyika tarehe 29 mwezi huu.
“Katika kambi hii wananchi wanapimwa vipimo mbalimbali vya moyo ikiwa ni pamoja na urefu, uzito, kuangalia uwiano baina ya urefu na uzito, kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography) na mfumo wa umeme wa moyo (Electrocardiography). Wengine kwa mara ya kwanza wamegundulika kuwa na matatizo ya moyo ikiwa ni pamoja na kutanuka na kuziba kwa mishipa ya damu ya moyo ambapo asilimia 5 tumewapa rufaa ya kuja kufanyiwa vipimo zaidi katika Taasisi yetu”.
“Tumewafanyia pia uchunguzi watoto ambapo wengine tumewakuta na matatizo ya valvu za moyo na matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo ambayo ni matundu na mishipa ya damu ya moyo kutokukaa katika mpangilio wake hawa nao tumewapa rufaa ya kuja kutibiwa JKCI”, alisema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge aliwaomba wananchi kuepuka tabia hatarishi zinazoweza kuharibu mioyo yao hii ikiwa ni pamoja na uvutaji wa sigara na unywaji wa pombe uliokithiri.
“Ili kuepuka kupata magonjwa yasiyo ya kuambukiza ikiwa ni pamoja na magonjwa ya moyo ni muhimu watu wakafuata mtindo bora wa maisha hii ikiwa ni pamoja na kufanya mazoezi na kula vyakula bora”, alisema Dkt. Kisenge.

Mkuu huyo wa idara ya utafiti na mafunzo alisema Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete itaendelea kuwasogezea wananchi huduma za kibingwa za matibabu ya moyo kwa kuwafuata mahali walipo na kuwajengea uwezo wataalamu wa afya wa jinsi ya kutambua na kutibu magonjwa ya moyo kwani Serikali imenunua mashine za kisasa za kuchunguza moyo na kuzisambaza katika Hospitali mbalimbali hapa nchini.
Kwa upande wake mganga mkuu msaidizi wa Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya ndani Wailesy Adam alisema kufanyika kwa kliniki ya pamoja kati ya hospitali hiyo na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kumeweza kuwasogezea huduma karibu wakazi wa Arusha na mikoa ya jirani.
‘Kitu kikubwa walichokiona ni muitikio mkubwa wa watu na tumeona wagonjwa wengi na bado kuna wengine ambao hawajapata nafasi ya kuonwa hivyo basi wataonwa siku mbili zilizobaki. Watu wengi wanamatatizo ya moyo lakini wanakosa nafasi ya kukutana na madaktari bingwa wa moyo, kuwepo kwa wataalamu hawa kumewasaidia wananchi kupata huduma ya matibabu kirahisi”,

na magonjwa yasiyoambukiza mwananchi aliyefika Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo. Wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa ALMC wanafanya kambi maalum ya siku tano ya matibabu ya magonjwa ya moyo kwa wakazi wa mkoa wa Arusha na mikoa jirani.

No comments :

Post a Comment