Mkurugenzi wa Bodi ya Usimamizi wa Mfumo wa stakabadhi ghalani nchini Asangye Bangu akiwa na wanachama wa Chama cha Msingi cha Ushirika Ligunga Wilaya ya Tunduru alipokutana na wakulima wanaotumia mfumo wa stakabadhi ghalani katika kijiji cha Ligunga Tunduru.
Mkurugenzi wa Bodi ya Usimamizi wa Mfumo wa stakabadhi ghalani nchini Asangye Bangu akizungumza na wanachama wa Chama cha Msingi cha Ushirika Ligunga Wilaya ya Tunduru kuhusiana na mpango wa kuanzisha pensheni ya uzeeni kwa wakulima.
Mkurugenzi wa Bodi ya Usimamizi wa Mfumo wa stakabadhi ghalani nchini Asangye Bangu akizungumza na wanachama wa Chama cha Msingi cha Ushirika Ligunga Wilaya ya Tunduru kuhusiana na mpango wa kuanzisha pensheni ya uzeeni kwa wakulima.
WAKULIMA wanaouza mazao yao kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani wanatarajia kuanza kupata pensheni ya uzeeni.
Mkurugenzi wa Bodi ya Usimamizi wa Mfumo wa stakabadhi ghalani nchini Asangye Bangu Akizungumza na vyama vya Ushirika vya Msingi vya Ligunga,Namatili na Mtetesi katika Wilaya Tunduru,amesema,serikali imedhamiria kuhusisha Mfumo wa stakabadhi ghalani na pensheni kwa wakulima ili wakulima waweze kumudu kuendesha maisha yao wanapokuwa wazee.
Amesema uwezo wa kufanya kazi kwa wakulima wakiwa vijana ni tofauti na wanapofikisha miaka 60 hivyo wakulima watakaokuwa wanauza kwenye Mfumo wa stakabadhi ghalani michango yao kidogo kidogo itafanyika kwenye mfumo ili kujiwekea pensheni uzeeni.
"Nguvu zinapokuwa zimepungua,mashamba bado unayo hivyo pensheni itawawezesha wakulima wazee kuendelea kupata fedha za kuwalipa vibarua watakaokuwa wanawafanyia kazi za kilimo",alisisitiza Bangu.
Hata hivyo amesema pensheni hiyo kwa wakulima itaunganisha na mambo mengine muhimu kwa wazee kama Bima za Afya na mikopo.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo,serikali ipo katika hatua za awali za kuhakikisha kuwa suala la pensheni kwa wazee linafanikiwa.
Bangu amebainisha kuwa wataalam watapita kwa wakulima ambao watapenda kujiunga kwenye mfumo huo ili kutoa elimu ya uelewa kabla ya kuanza utekelezaji wake.
Amesema licha ya kwamba pensheni kwa wakulima ni jambo geni lakini litakuwa msaada mkubwa kwa wakulima na kwamba litaongeza hamasa kwa vijana ambao bado wana nguvu lakini baada ya miaka kadhaa watafikia uzeeni.
Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Tunduru TAMCU Musa Manjaule ameutaja mfumo wa stakabadhi ghalani kuwa una faida nyingi kwa mkulima.
Manjaule amesema wakulima wa Tunduru walianza kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani tangu msimu wa mwaka 2015/2016 hali inayowawezesha wananchi kuendelea kupata bei nzuri ya mazao.
Amewataja mazao ambayo yapo kwenye mfumo wa stakabadhi ghalani Wilaya ya Tunduru kuwa ni korosho,ufuta na mbaazi na kwamba wakulima wanafurahia mfumo huo ambao umeboresha maisha yao kwa sababu wanalipwa kwa wakati.
"Sisi kama wakulima wa Tunduru ukituambia tusitumie mfumo wa stakabadhi ghalani hatukuelewi kwa sababu tunajua uzuri wa Mfumo wa stakabadhi ghalani na ubaya wa ununuzi wa mazao kwa mfumo holela ",alisema.
Kwa upande wake mkulima khadija Rajabu wa kijiji cha Ligunga Wilaya ya Tunduru amesema licha ya wakati mwingine kujitokeza changamoto ya kuchelewa kwa malipo bado mfumo wa stakabadhi ghalani ndiyo mkombozi wa mkulima kwa sababu unalinda haki ya mapato ya mkulima.
No comments :
Post a Comment