NA MWANDISHI WETU
SERIKALI imetoa maelekezo ya kisheria (Compliance Order) ili kuwataka waajiri kote nchini kutoa Mikataba kwa wafanyakazi madereva.
Maelekezo hayo ya serikali yametangazwa jijini Dar es Salaam Julai 22, 2022 na Naibu Waziri wa Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi kufuatia hoja na malalamiko yaliyowasilishwa na viongozi wa vyama vya wafanyakazi madereva na wamiliki wa vyombo vya usafirishaji nchini.
“Katika kushughulikia malalamiko na hoja hizo,tulikutana na Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi Madereva kwa lengo la kusikiliza hoja na malalamiko yao tarehe 24 Aprili, 2022, baada ya kupokea hoja hizo, Serikali iliahidi kuzifanyia kazi katika kipindi cha siku 90 na kutoa taaarifa rasmi ambayo ndiyo hii tunayoitoa kwa umma.” Alifafanua Mhe. Katambi.
Alisema ifikapo mwishoni mwa mwezi Agosti, 2022 Serikali itaanza kuwachukulia hatua waajiri ambao watabainika kukaidi maelekezo ya Serikali. Alisema katika kuhakikisha Madareva wanapatiwa Mikataba ya Kazi, Serikali inaendelea na zoezi la kufanya kaguzi zinazoshirikisha wadau wanaoguswa na sekta hii na tayari kaguzi zilifanyika katika Mikoa ya Dar es salaam, Arusha, Mwanza, Pwani na Mbeya ambapo Jumla ya Kampuni 73 zilikaguliwa na kubaini baadhi ya waajiri hawajatoa mikataba kwa Madereva.
Mhe. Katambia pia alisema kupitia kaguzi zinazoendea kufanyika katika maeneo ya kazi, Serikali itasimamia suala la Madereva kupatiwa hati za malipo ya mshahara (salary slip) kama inavyoelekezwa kwenye Sheria.
Aidha Serikali inawashauri Madereva kufanya makubaliano na waajiri wao kuhusu utaratibu gani utumike kuwalipa mishahara kwani Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, Sura 366 imeruhusu mwajiri na mfanyakazi kukubaliana namna ya kulipana mshahara ama kupitia benki, fedha taslim au hundi, alisema
Aidha Sheria inawataka waajiri wote kuwasajili na kuwachangia wafanyakazi wao katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (NSSF na WCF) wakiwemo wafanyakazi Madereva.
“Katika ukaguzi uliofanyika awali ilibainika kuwa baadhi ya waajiri hawajawasajili Madereva wao katika Mifuko hiyo, hivyo maelekezo ya kisheria yametolewa. Serikali itaendelea kufuatilia waajiri hao ili kuhakikisha wanatekeleza Sheria ipasavyo.” Alisema.
No comments :
Post a Comment