Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Benki ya CRDB, Prof. Neema Mori (wakwanza kushoto) akifurahia tuzo ya 'Benki Bora Tanzania' na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, pamoja na Meneja Mipango ya Biashara Benki ya, Masele Msita katika hafla ya kuwashukuru wateja na wadau wa Benki hiyo kwa mafanikio hayo iliyofanyika Makao Makuu ya Benki ya CRDB Jijini Dar es Salaam leo 20 Julai 2022. Jarida maarafu la fedha na uchumi la Euromoney liliitaja Benki ya CRDB kama moja ya benki bora duniani katika hafla ya kukabidhi tuzo kwa benki zilizofanya vizuri iliyofanyika Julai 13 2022 Jijini London nchini Uingereza.
========== ========== ==========
Benki ya CRDB imewashukuru wateja na wadau wake baada ya kutunukiwa tuzo ya “Benki Bora Tanzania” na jarida maarafu la masuala ya fedha na uchumi la nchini uingereza la Euromoney.
Shukrani hizo zimetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Makao Makuu ya Benki ya CRDB na kuhudhuriwa na wajumbe wa bodi, wafanyakazi, na wateja, wa Benki hiyo.
Akizungumza katika mkutano huo uliofanyika Makao Makuu ya Benki hiyo Jijini Dar es Salaam, Nsekela alisema wateja wa benki hiyo wamekuwa sehemu ya mafanikio ya utekelezaji wa mkakati wa mageuzi ya biashara ambao umepelekea kupata tuzo hiyo.
“Niwashukuru wateja, wanahisa, Serikali, Benki Kuu ya Tanzania na washirika wetu wa biashara kwa ushirikiano wanaotupa na kuendelea kutufanya kuwa bora zaidi. Hii sio tuzo ya Benki ya CRDB peke yake, ni tuzo ya Watanzania wote,” alisema Nsekela.
Mwaka 2019, Benki hiyo ilianza ikifanya mageuzi katika biashara yake ambayo yamejikita katika kutengeneza thamani endelevu, kuongeza ujumuishi wa kifedha, na kujenga uchumi jumuishi kupitia bidhaa, huduma, na mifumo bunifu ya utoaji huduma.
“Tuzo ya Euromoney inathibitisha nafasi ya Benki ya CRDB kama ‘Benki Kiongozi’ nchini. Vilevile, inatambua mafanikio ya mageuzi haya ambayo yamepelekea ukuaji endelevu wa Benki yetu na ukinufaisha wateja, wawekezaji na uchumi wa nchi kwa ujumla wake.”
Waandaji wa tuzo hizo pia wametambua mchango wa mageuzi wa kidijitali ambayo yamefanyika ndani ya Benki ya CRDB, ikielezwa kuwa kiasi kikubwa yamesaidia kuchochea ongezeko la ujumuishi wa kifedha nchini.
“Tumekuwa pia tukishiriki kikamilifu katika kusaidia sekta mbalimbali za maendeleo nchini hususani kilimo, na ujusariliamali ambazo zimekuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa Taifa letu,” aliongezea Nsekela huku akibainisha kuwa Benki hiyo ilitoa ahueni kubwa kwa sekta ya biashara nchini katika kipindi ambacho janga la UVIKO-19 limeikumba dunia.
Aidha, alisema Benki hiyo pia imetambuliwa kwa kuwa na uwezo mkubwa katika uwezeshaji wa miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali na sekta binafsi akitolea mfano Mradi wa Umeme wa Maji wa Nyerere na Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR). Nsekela alisema jitihada na mafanikio hayo pia yamekuwa yakijidhihirisha katika matokeo ya kifedha ambayo imekuwa ikiyapata mwaka hadi mwaka.
Benki ya CRDB ndio Benki ya kwanza nchini kutunikiwa tuzo ya ‘Benki Bora Tanzania’ na Euromoney mwaka 2004. Ushindi wa tuzo hiyo mwaka huu unadhihirisha kuimarika kwa utendaji wa Benki siku za hivi karibuni na kutambuliwa kimataifa.
Mwaka jana Benki hiyo ilitajwa kama Benki Bora Tanzania’ na ‘Benki inayoongoza kwa Ubunifu’ na jarida maarufu duniani la masuala ya fedha la ‘Global Finance’, huku Taasisi ya Utafiti wa Ubora barani Ulaya ikiitunikia ‘Tuzo ya Ubora’.
No comments :
Post a Comment