Katika mwendelezo wake wa kusaidia uwezeshaji wa kundi la wajasiriamali nchini, Benki ya CRDB leo imesaini hati ya makubaliano ya mkopo wa jumla ya dola milioni 60 na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).
Katika makubaliano hayo na AfDB, Benki ya CRDB itaelekeza dola milioni 50 katika kuimarisha mtaji wake, pamoja na kusaidia mpango wa upanuzi wa kikanda za benki hiyo. Sehemu iliyobaki ya mkopo huo, dola za kimarekeni milioni 10, itaelekezwa katika kusaidia upatikanaji wa fedha kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati nchini Tanzania.
Mkataba huo pia unajumuisha msaada wa kiufundi na mafunzo wenye thamani ya dola 175,000 ili kuimarisha uwezo wa Benki ya CRDB kusaidia wajasiriamali wanawake nchini Tanzania ili waweze kukopesheka zaidi.
Aidha, Mfuko wa Dhamana ya Afrika (AGF) umeboresha mpango wake wa dhamana kwa wa dola milioni 50 kwa Benki ya CRDB kwa ajili ya wajasiriamali nchini. Mpango huo unajumuisha sehemu ya dhamana ya AFAWA ya Ukuaji ili kupunguza hatari ya soko kwa wanawake wajasiriamali na kusaidia zaidi ukuaji wao. Dhamana ya Ukuaji ya AFAWA ni sehemu ya mpango wa Benki ya Maendeleo ya Afrika ambao unalenga kufanya uwezesha wa hadi dola bilioni 5 kwa biashara za wanawake ifikapo 2026.
Ukiwa umesainiwa na Nnenna Nwabufo, Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Afrika Mashariki, Jules Ngankam, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Dhamana Africa, na Abdulmajid Nsekela, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, mkataba huu wa uwezeshaji unaipa Benki ya CRDB uwezo mkubwa wa ufadhili wa kundi la wajasiriamali nchini hususan wanawake na kuibua uwezo wao kamili.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa AGF, Jules Ngankam aliishukuru Benki ya CRDB kwa ushirikiano wake wa muda mrefu na Mfuko wa Dhamana Afrika uhusiano wa ambao umesaidia wajasiriamali katika sekta mbalimbali nchini. "Ni imani yangu kuwa ushirikiano huu wa pande tatu baina ya Benki ya CRDB, AfDB, na AGF, utakuwa na matokeo chanya zaidi hususan katuka kuziba pengo la ufadhili kwa biashara za wanawake."
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Afrika Mashariki, Nnenna Nwabufo alisema kuwa ushirikiano huu, utawezesha wajasiriamali kupata fedha za kukuza na kuboresha biashara zai. Muhimu zaidi inaongeza juhudi za Tanzania kuziba pengo la upatikanaji wa fedha kwa wajasiriamali wanawake ambalo linakadiriwa kufikia dola bilioni 1.6.
“Tumefurahi sana kukamilisha mikataba hii. Mkopo wa dola 50 uliotolewa na AfDB utasaidia kuboresha mtaji wa benki kwa ujumla, kusaidia utekelezaji wa mikakati ya Benki, na upanuzi wa kikanda bila kuhatarisha uwiano wa mtaji. Napenda kuwashukuru washirika wetu AfDB na AGF kwa msaada wao unaoendelea "alisema Abdulmajid Nsekela, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB.
Kwa sasa Benki hiyo ipo katika hatua za mwisho kuingia nchini DRC huku pia ikifikiria kujitanua katika masoko mengine katika ukanda huu wa Afrika ya Mashariki na Kati.
Nsekela pia alieleza kuwa makubaliano hayo na AfDB na AGF yanaunga mkono dhamira ya Benki ya CRDB ya kuwawezesha wajiasiriamali nchini kupitia mikopo nafuu. "Mkopo wa dola milioni 10 na dhamana ya dola milioni 50 itaimarisha uwezo wetu wa kusaidia biashara nyingi zinazomilikiwa na wanawake kupitia mpango wetu wa ‘Women Access to Finance (WAFI)’, unaoendeshwa chini ya mwamvuli wa CRDB Malkia."
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (katikati) akibadilishana mkataba na Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Dhamana Africa, Jules Ngankam kwa ajili ya uwezeshaji wanawake wajasiriamali nchini. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Afrika Mashariki, Nnenna Nwabufo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (katikati) akibadilishana mkataba na Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Afrika Mashariki, Nnenna Nwabufo kwa ajili ya uwezeshaji wanawake wajasiriamali nchini. Kulia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Dhamana Africa, Jules Ngankam akionyesha mkataba ambao mfuko huo umeingia na Benki ya CRDB. Katika mikataba hiyo Benki ya CRDB imepata mkopo wa dola milioni 60 na Benki ya Maendeleo Afrika, na mkataba wa dhamana ya mikopo wa dola milioni 50 na Mfuko wa Dhamana Afrika.
No comments :
Post a Comment