Na Edmund Salaho/MLIMA KILIMANJARO
Wapagazi na waongoza watalii zaidi ya 180, kutoka makampuni mbalimbali yanayopandisha watalii katika Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro leo wameanza zoezi la usafi katika Hifadhi hiyo, zoezi ambalo litachukua takribani siku saba.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa zoezi hilo Mkuu wa Idara ya Utalii Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro, Charles Ngendo alisema
“Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro ina utaratibu wa kushirikiana na wadau wote wa Mlima Kilimanjaro kwa ajili ya kufanya maandalizi ya msimu mpya wa utalii na mwaka huu msimu wa utalii utaanza mapema , hii ni habari njema sana kwani kampuni nyingi zimetoa taarifa kwamba wanawageni hivyo zoezi hili ni kujiweka tayari kupokea wageni “ alisema Ngendo.
Kwa upande wake Afisa Uhifadhi Mwandamizi kutoka Idara ya Mawasiliano, Catherine Mbena alisema
“TANAPA kwa ujumla tumeendelea kufanya maandalizi kuwakaribisha wageni katika Hifadhi zetu za Taifa ambapo kwa mujibu wa takwimu msimu huu tutakuwa na wageni wengi sana na kama ilivyo katika Hifadhi zingine tumeendelea na maandalizi ya miundombinu ya usafiri yaani Barabara, Viwanja vya ndege, Maeneo ya kupumzikia wageni pamoja na miundombinu ya malazi na leo tumekutana hapa ikiwa ni muendelezo wa maandalizi hayo”
Pia niwapongeze wadau kwa kushirikiana nasi katika kuhakikisha mazingira ya hifadhi za Taifa yanakuwa safi na salama
Naye, muwakilishi wa wapagazi kutoka Kampuni ya Nature Discovery, Edson Herman alisema
“Tunaamini mlima ni ofisi kama zilivyo ofisi zingine na sisi tunapenda ofisi yetu iendelee kuwa safi kwani ndivyo wageni huvutiwa na kuja kutembelea kwa wingi na sisi kuendelea kufaidika na ofisi yetu” alisema Edson
Zoezi la kufanya usafi katika Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro linafanyika katika njia zote saba zinazotumika na wageni kupanda Mlima Kilimanjaro
No comments :
Post a Comment