Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Kazi, Vijana, Ajira Na Wenye Ulemavu), Mhe. Prof. Joyce Ndalichako, akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari makao makuu ya WCF jijini Dar es Salaam Mei 5, 2022 wakati akitoa tamko hilo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Kazi, Vijana, Ajira Na Wenye Ulemavu), Mhe. Prof. Joyce Ndalichako, akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari makao makuu ya WCF jijini Dar es Salaam Mei 5, 2022 wakati akitoa tamko hilo.
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma akitoa shukrani zake kufuatia tamko la serikali la kutoa msamaha wa riba kwa waajiri wote waliochelewa kuwasilisha michango kwenye Mfuko.
Bw. Joseph Nganga, Mkuu wa Huduma za Ajira, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu akizungumza.
Serikali imetangaza msamaha wa riba kwa waajiri wote waliochelewa kuwasilisha michango katika Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF).
Tamko hilo limetolewa leo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira Na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako wakati wa Mkutano na Waandishi wa Habari uliofanyika katika Ukumbi wa Victoria House, jijini Dar es Salaam.
“Kwa mamlaka niliyopewa chini ya Kifungu 75(5) cha Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi [Sura 263], natangaza msamaha wa riba iliyotozwa kwa kipindi cha kuanzia tarehe,,.
01 Oktoba, 2017 hadi tarehe 31 Agosti 2021 kwa waajiri wote waliochelewa kuwasilisha michango katika Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi kwa kipindi hicho”, amesema Waziri Ndalichako.Amefafanua kuwa waajiri watakao nufaika na msamaha huu ni wale tu waliokwishalipa malimbikizo ya michango wanayodaiwa na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi na wamebakiza deni la riba peke yake.
Amesema hadi kufikia Agosti 2021 takribani waajiri 13,468 wa sekta ya Binafsi na waajiri 191 wa Sekta ya Umma walikuwa kwenye orodha ya madeni ya riba.
Aidha, kwa Waajiri wote watakao lipa malimbikizo ya michango ya miezi ya nyuma wanayodaiwa na Mfuko kabla ya tarehe 30 Juni 2022 nao pia watanufaika na msamaha huu wa ondoleo la riba ya michango kwa miezi tajwa.
Vilevile, Waajiri wote, ambao mpaka sasa hawajajisajili kwenye Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi watakapojisajili na kulipa michango stahiki inayodaiwa kabla ya tarehe 30 Juni 2022 nao pia watanufaika na msamaha wa riba ya malimbikizo ya madeni ya michango.
Wakati huohuo Waziri Ndalichako amewataka waajiri kutumia vizuri msamaha huu uliotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita unaolenga kuongeza kiwango cha utekelezaji wa hiari wa Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi Sura 263 katika kuhakikisha waajiri wote wanajisajili katika Mfuko na kulipa malimbikizo ya michango ya nyuma bila kutozwa riba.
Amefafanua kuwa michango inayotolewa na waajiri inatumika kulipa wafanyakazi fidia pale atakapopata ajali ama ugonjwa kutokana na kazi na iwapo bahati mbaya Mfanyakazi atafariki, fidia hiyo italipwa kwa wategemezi wake.
Waziri Ndalichako pia ameeleza kuwa tangu Julai 2015 hadi kufikia Agosti 2021, michango iliyocheleweshwa ilikuwa ikitozwa riba ya asilimia 10 kwa mwezi. Hata hivyo Serikali iliamua kushusha kiwango cha riba kutoka asilimia 10 hadi kufikia asilimia 2.0 kwa mwezi kuanzia mwezi Septemba 2021, ili kutoa nafuu kwa waajiri na kuweka mazingira rafiki ya biashara na uwekezaji hapa nchini.
Prof. Ndalichako amesisitiza kuwa michango itakayolipwa baada ya kipindi kilichowekwa kisheria kumalizika itatozwa riba.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi Dkt. John Mduma ameishukuru Serikali kukubali kutoa punguzo hilo kwani linarahisisha usimamizi na utekelezaji wa majukumu ya Mfuko huo.
“Tunaishukuru Serikali na tunaamini msamaha huu utasaidia utekelezaji wa majukumu yetu pia kuhamasisha Waajiri kuitikia kwa hiari”, amesema Dkt. Mduma.
Kuhusu viwango vya uchangiaji Dkt. Mduma amefafanua kuwa anayepaswa kujisajili na kuchangia kwenye Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi ni mwajiri pekee yake na viwango vinavyopaswa kuchangiwa ni asilimia 0.6 ya mshahara wa mwezi wa kila mfanyakazi kwa sekta binafsi na asilimia 0.5 kwa Sekta ya Umma.
Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) ni taasisi ya Hifadhi ya Jamii iliyoundwa kwa Mujibu wa Kifungu cha 5 cha Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi, Sura 263 kwa lengo la kushughulikia masuala ya Fidia kwa wafanyakazi walio katika sekta ya Umma na Binafsi Tanzania Bara ambao wataumia, kuugua ama kufariki kutokana na kazi.
No comments :
Post a Comment