Thursday, April 7, 2022

Waziri wa Mifugo azungumzia uhitaji wa maziwa nchini

maziwapicc

By Aurea Simtowe

Dar es Salaam. Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki ameiagiza Bodi ya

Maziwa Tanzania (TDB) kushirikiana na chama cha Wasindikaji wa Maziwa (TAMPA) kutengeneza uhitaji wa maziwa kwa wananchi badala ya kuendelea kutumia nguvu kubwa kwenye kusisitiza uzalishaji na Usindikaji pekee.

Ameyasema hayo kwenye mkutano wake na Chama cha Wasindikaji wa Maziwa nchini.

Ndaki alizitaka pande zote mbili kuhakikisha zinapata suluhu ya changamoto ya kiwango kidogo cha matumizi ya bidhaa hiyo nchini.

"Hebu jiulizeni kwa mfano maziwa yakakosekana siku nzima hapa Tanzania kuna watu wataandamana kama ilivyo kwa bidhaa nyingine? Kwa sababu inawezekana tunatumia nguvu kubwa kusisitiza uzalishaji na usindikaji wakati hakuna uhitaji wa bidhaa hiyo hapa kwetu," amesema Ndaki.

Ndaki amesema nia ya Serikali ni kuhakikisha bidhaa hiyo inawasaidia wafugaji na wasindikaji waliopo hapa nchini kwa kuanza na soko la ndani hivyo ni lazima Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi wahakikishe linakuwa la uhakika.

Msajili wa Bodi ya TDB, Dk George Msalya amekiri kuwa mchango wa tasnia ya Maziwa kwenye pato la Taifa bado upo chini ukilinganisha na nchi nyingine za Afrika Mashariki.

ADVERTISEMENT

"Mpaka sasa Tasnia yetu inakuwa kwa asilimia 2.3 na mchango wake kwenye pato la Taifa ni asilimia 2 kwa mujibu wa takwimu zilizopo wakati wenzetu Kenya wanachangia asilimia 5 na Uganda na Rwanda nao wanakuja kwa kasi kubwa hivyo tuna kazi kubwa ya kufanya,”amesema Dk Msalya.

Awali mmoja wa wasindikaji wa Maziwa nchini kutoka Kiwanda cha Nronga kilichopo Siha Mkoani Kilimanjaro,  Hellen Usiri amesema changamoto kubwa inayowakabili ni uwepo wa wauzaji maziwa wasio rasm.

Wauzaji hao hununua maziwa kwa mfugaji kwa bei kubwa ikilinganishwa na ile inayotolewa na viwanda vya kusindika bidhaa hiyo.

"Hawa wenzetu hawalipi kodi na hawana gharama yoyote ya uchakataji ndio maana wanauza kwa bei wanayotaka wao hivyo nashauri wafanyabiashara hao wa mitaani wajiunge kwenye vyama vya ushirika ili maziwa wanayouza yatoke kwenye vyama hivyo yakiwa salama kabisa tofauti na sasa ambapo maziwa mengi yanayouzwa mtaani si salama,” amesema Usiri.

No comments :

Post a Comment