Monday, April 25, 2022

TRA YATOA MSAMAHA WA RIBA NA ADHABU KWA WAMILIKI WA VYOMBO VYA MOTO VILIVYOINGIZWA NCHINI KINYUME CHA SHERIA

 Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi Bw. Richard Kayombo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa ya msamaha wa riba na adhabu ya kodi kwa wamiliki wa vyombo vya moto vilivyoingizwa nchini bila kufuata taratibu za forodha. Kushoto ni Meneja Msaidizi wa Udhibiti Bw. John Micah.


Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi Bw. Richard Kayombo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa ya msamaha wa riba na adhabu ya kodi kwa wamiliki wa vyombo vya moto vilivyoingizwa nchini bila kufuata taratibu za forodha. Kushoto ni Meneja Msaidizi wa Udhibiti Bw. John Micah na kulia ni Afisa Forodha Mkuu Bw. Michael Kasongwa Pamoja na Afisa Msimamizi wa Kodi Bi. Julieth Kidemi.


Baadhi ya waandishi wa habari wakifuatilia taarifa ya msamaha wa riba na adhabu ya kodi kwa wamiliki wa vyombo vya moto vilivyoingizwa nchini bila kufuata taratibu za forodha iliyotolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi Bw. Richard Kayombo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Na Mwandishi wetu,Dar es Salaam.


Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetoa msamaha wa riba na adhabu ya kodi kwa wamiliki wa vyombo vya moto vilivyoingizwa nchini bila kufuata taratibu za forodha kuanzia leo tarehe 25 Aprili hadi Juni 30, 2022.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi Bw. Richard Kayombo amesema kwamba, vyombo hivyo vinahusisha vile vilivyoingizwa kwa njia za magendo, vilivyokusudiwa kwenda nchi jirani lakini vikaingizwa nchini kinyume na taratibu, vilivyoingizwa nchini kwa muda na kuzidisha muda wa kukaa nchini na vilivyotumia msamaha wa kodi kinyume na sheria au kubadilishwa umiliki bila kufuata taratibu.

“Lengo la msamaha huu ni kutoa unafuu kwa wamiliki wa vyombo hivyo vya moto vyenye madeni ya kodi na adhabu kwa kulipa kodi waliyokadiriwa tu bila adhabu na riba,” Amesema Mkurugenzi Kayombo.

Amelitaja lengo lingine la msamaha huo kuwa ni kujenga ushirikiano na uhusiano mwema kati ya TRA na wamiliki hao, kuwapa motisha ya kulipa kodi kwa hiari na wakati pamoja na kuweka kumbukumbu au taarifa sahihi za umiliki wa vyombo hivyo.

Mkurugenzi Richard Kayombo ametoa wito kwa wamiliki hao wa vyombo vya moto kujitokeza ndani ya muda wa msamaha uliotolewa na Kamishna Mkuu ili waweze kulipa kodi halisi inayodaiwa na hatimaye kukomboa vyombo yao.

“Nachukua fursa hii kutoa wito kwa wamiliki wote wa vyombo vya moto vilivyoingizwa nchini kwa njia nilizozitaja, kuchangamkia msamaha huu ili waweze kukomboa vyombo vyao kwa kulipia kodi halisi isiyokuwa na riba wala adhabu,” alieleza.

Mamlaka ya Mapato Tanzania imetoa msamaha huu kwa mujibu wa kifungu cha sheria namba 70 (2) cha Sheria ya usimamizi wa Kodi ya mwaka 2015, kama ilivyofanyiwa marekebisho na Sheria ya Fedha ya mwaka 2021 pamoja na kifungu cha 249 cha Sheria ya Usimamizi wa Ushuru wa Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2004 ambazo zinampa Kamishna Mkuu wa TRA mamlaka ya kusamehe riba na adhabu.

No comments :

Post a Comment