Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV - Dodoma
ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mzee Yusuph Makamba ametoa ya moyoni kuhusu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan na Aliyekuwa Katibu Mkuu na Kada mkongwe wa Chama hicho, Ndugu Abdurahman Kinana.
Mzee Makamba ametoa ya moyoni katika mkutano Mkuu maalum wa Chama hicho, uliofanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma ikiwa baada ya kuugua Macho kwa kipindi cha miaka miwili. Amesema anaamini baada ya kufariki Hayati Magufuli, nchi ya Tanzania ipo mikono salama chini ya uongozi wa Mama Samia Suluhu aliyeshika madaraka kwa sasa.
“Ulivyozungumza na Wanawake wa Tanzania, nilikusikia ukisema bado hamjachaguliwa Rais Mwanamke katika taifa hili. Ulisema Rais Mwanamke atachaguliwa mwaka 2025, mimi nasema Mgombe Mwanamke ni wewe Mama Samia na sio Mwanamke mwengine yeyote”, amesema Mzee Makamba.
Kuhusu uongozi wa Rais Samia, Mzee Makamba amesema anaamini ataweza kuliongoza taifa la Tanzania kwa ukamilifu kama alivyofanya Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete na watangulizi wengine waliopita katika nafasi hiyo.
“Tumezoea kusema mzigo mzito mpe Mnyamwezi, lakini hata Mkwere aliwahi kuubeba mzigo huu. Kama Mkwere amebeba mzigo huu, kwa nini Mzanzibar ashindwe?”, amehoji Mzee Makamba.
“Nyuki wameingia kwenye Mzinga wa Bibi, na kule visiwani Zanzibar wameingia kwenye Mzinga wa Babu, sasa tunaona Watanzania wanavyokula Asali kwa sasa, hii ni kwa sababu ya mambo mazuri yanayofanyika katika Sekta mbalimbali katika taifa hili la Tanzania”, ameeleza
KUHUSU ABDULRAHMAN KINANA
Mzee Makamba amesema Chanda chema, huvikwa Pete, amemuasa Katibu Mkuu huyo wa zamani kumsaidia Rais wa Tanzania kuongoza vyema, akiwa kama msaidizi wake katika majukumu ya Chama.
“Nakumbuka Ukumbi huu wa Mikutano ulitakiwa kuitwa jina la Kinana, lakini ukapewa jina la Rais Mstaafu Jakaya Kikwete. Kumbe Halmashauri Kuu na Kamati Kuu ya Taifa inamtafutia Umakamu Mwenyekiti wa Chama”, amesema Makamba.
Amesema amefanya kazi na Kinana katika nyakati tofauti na anamjua vizuri katika utendaji kazi wake, wakifanya kazi kwenye raha na shida kuhakikisha maendeleo ya Chama yanapatikana na taifa kwa ujumla.
“Tuliwahi kufikishwa kwenye Kamati Maadili ya Chama, nakumbuka tukasamehewa wote wawili, na wewe Kinana samehe yameisha hayo, watu dhaifu hawawezi kusamehe”.
No comments :
Post a Comment